Apr 21, 2024 13:55 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (46)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 46 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 46 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 38. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Katika Hikma ya 38 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatupa hazina nane zenye thamani kubwa kwa kutumia maneno mafupi lakini yenye ufasaha na balagha ya hali ya juu. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia hazina nne za mwisho za hikma hiyo ya 38 ya Nahjul Balagha ambazo zinazungumzia wajibu wa kujiepusha kufanya urafiki na makundi manne ya watu wenye tabia mbaya. 

Baada ya Imam Ali AS kutoa miongozo muhimu kuhusu akili, upumbavu, majivuno , na tabia njema, hapa sasa anazungumzia nukta nyingine nne muhimu ambazo zinamuongoza mtu kucha kufanya urafiki na kila mwenye mambo hayo manne mabaya. Anamkhutubu mwanawe wa kwanza yaani Imam Hasan AS akimwambia:

یَا بُنَیَّ إِیَّاکَ وَ مُصَادَقَةَ الْأَحْمَقِ، فَإِنَّهُ یُرِیدُ أَنْ یَنْفَعَکَ فَیَضُرُّکَ؛ وَ إِیَّاکَ وَ مُصَادَقَةَ الْبَخِیلِ، فَإِنَّهُ یَقْعُدُ عَنْکَ أَحْوَجَ مَا تَکُونُ إِلَیْهِ؛ وَ إِیَّاکَ وَ مُصَادَقَةَ الْفَاجِرِ، فَإِنَّهُ یَبِیعُکَ بِالتَّافِهِ؛ وَ إِیَّاکَ وَ مُصَادَقَةَ الْکَذَّابِ، فَإِنَّهُ کَالسَّرَابِ یُقَرِّبُ عَلَیْکَ الْبَعِیدَ وَ یُبَعِّدُ عَلَیْکَ الْقَرِیبَ

Ewe mwanangu jiepushe kabisa na kufanya urafiki na mtu ahmaq na mjinga, kwani huweza kutaka kukufanyia jambo la kukunufaisha, lakini badala yake akakudhuru. Jiepushe na kufanya urafiki na bakhili kwani hukunyima kitu ambacho unakihitajia mno. Jiepushe kufanya urafiki na mtu fasiki na mchafu kwani anaweza kukuuza kwa thamani ndogo kabisa. Na jiepushe kabisa kufanya urafiki na mtu muongo kwani yeye ni kama mazigazi, mbali hukwambia ni karibu, na karibu hukwambia ni mbali. 

 

Marafiki wana athari kubwa katika maisha ya watu. Mtu anayefanya urafiki na mtu mpumbavu na ahmaq (na tulitoa ufafanuzi kwenye vipindi vilivyoopita kuhusu neno ahmaq) basi kwa hakika atapata hasara. Kwa sababu mtu mpumbavu huwa anatumbukia kwenye makosa makubwa kutokana na upumbavu wake. Huwa anafikiri jambo ni zuri, lakini kumbe ni la hatari na baya mto. Ndio maana mtu ahmaq utamuona anamlazimisha rafiki yake kufanya jambo ambalo linamtumbukiza kwenye majanga na halina mwisho mwema. Na wakati mwingine utamuona anamzuia rafiki yake kufanya jambo zuri na kumtia hasa kwa kupoteza fursa ya kufanya jambo hilo lenye manufaa. Vishawishi vya rafiki ahmaq na mpumbavu, humtia hasa mtu na kumuathiri katika maamuzi na matendo yake, kutaka asitake. 

Imam Ali AS anasema katika sehemu inayofuata kwamba: Jihadhari na kufanya urafiki na mtu bakhili, kwa sababu atakutupa na kukutelekeza wakati unapomhitaji zaidi. Ni ukweli usiopingika kwamba watu mabakhili hawako tayari kuwasaidia kwa dhati wengine na wala hawapenzi wengine wanufaike na neema waliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu.

Mtu wa tatu ambaye Imam Ali AS anatukata kufanya urafiki na usuhuba naye ni mtu mchafu na fasiki na mchafu. Imam anasema: "Jiepushe kufanya na urafiki na mtu fasiki, kwa sababu atakuuza kwa thamani duni kabisa." Wanacho jali watu kama hao ni maslahi yao binafsi tu na kushibisha hawaa na matamanio ya nafsi zao. Ni kwa sababu hiyo ndio utamuona wakati wote anatafuta fursa za kunufaika zaidi kutoka kwa mwengine na hata mwamana wala urafiki wa kuaminika. Ni mtu hatari sana. 

Katika indhari yake ya mwisho hapa, Imam Ali (AS) anasema: “Jihadhari na kufanya urafiki na mtu mwongo, kwa sababu yeye ni kama sarabi na mazigazi. Ni mdanganyifu. Hukuonesha kilichoko mbali kuwa kiko karibu na kilichoko karibu kiko mbali na unapokifia kitu hicho unaambulia patupu.

Tags