Apr 21, 2024 13:57 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (48)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi na karibuni katika sehemu hii ya 48 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 48 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 40 na 41.

لِسَانُ الْعَاقِلِ وَرَاءَ قَلْبِهِ، وَ قَلْبُ الْأَحْمَقِ وَرَاءَ لِسَانِهِ

Ulimi wa mwenye akili uko nyuma ya moyo (na mantiki) yake, na moyo (na mantiki) ya ahmaq na zumburukuku iko nyuma ya ulimi wake.

Hikma za 40 na 41 za Nahjul Balagha zinatufungua macho na kutueleza ukweli muhimu sana katika kalibu ya vifungu viwili. Katika hikma hii ya 40, Imam Ali AS anasema Ulimi wa mwenye hikma uko nyuma ya moyo, na moyo wa mpumbavu uko nyuma ya ulimi. Ulimi wa mwenye hikma uko nyuma ya mantiki na akili yake kwa sababu hatumii ulimi wake kabla ya kushauriana kwanza na moyo na akili yake. Lakini kwa mtu ahmaq na mpumbavu, hali ni kinyume chake kabisa, hutumia kwanza ulimi wake kabla ya kushauriana na akili yake na matokeo yake siku zote ni kusababisha madhara kwake na kwa wenzake.

Amma katika hikma ya 41, Imam Ali AS anasema:

قَلْبُ الْأَحْمَقِ فِی فِیهِ، وَ لِسَانُ الْعَاقِلِ فِی قَلْبِهِ

Imam anatuchorea picha ya kutuonesha kuwa, moyo wa mpumbavu uko usoni mwake lakini ulimi wa mwenye hikma uko moyoni mwake. Au tuseme hivi, moyo wa mpumbavu uko kinywani mwake, lakini ulimi wa mwenye hikma uko moyoni mwake.

Imam Ali AS anatupa somo kubwa na muhimu sana katika hikma hizi mbili za 40 na 41 ya kwamba, wale wanaozungumza kwa uangalifu na kufikiri kwanza kabla ya kutamka neno lolote, hao ndio wenye hikma na waliofaulu. Lakini anasema kitu kwanza halafu ndipo anafikiri amesema nini, huyo si mpumbavu na mjinga.

Naam!  Miongoni mwa tofauti kubwa zilizopo baina ya mtu mwenye hikma na yule asiye na hikma ni katika mazungumzo yao. Mwenyezi hikma huwa makini sana katika kuzungumza na haropoki. Hasemi ila anapolazimika kusema na anaposema hushauriana kwanza na moyo na akili yake ndipo baadaye huuruhusu ulimi wake utamke alichokusudia kusema. Na hiyo ni neema kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mtu kupewa uwezo wa kufikiri kwanza kabla ya kutenda jambo lolote ikiwemo kutamka neno lolote. Lakini mtu mpumbavu huwa amenyimwa neema hiyo ya kutumia vizuri akili na fikra zake na ndio maana ulimi wake siku zote unakuwa uko mbele ya akili na moyo wake. Mtu wa namna hiyo huwa maarufu kwa kusema uongo, lakini pia hukosa soni za kutamka jambo lolote baya bila ya kujali matokeo yake. Kwake yeye huwa si muhimu analolisema ni la kweli au ni la uongo, ni baya au ni zuri, litawakera watu wengine au halitowake, litawaudhi wengine au la, litasababisha mabalaa au hapana, yote kwake si muhimu mtu mpumbavu. 

Marhum Sayyid Sharif al Razi, khatibu maarufu na mashuhuri wa Waislamu wa madh'hab ya Kishia, anayejulikana kwa jina maaruru la "Khatib Masri" na ambaye ndiye aliyekikusanya kitabu cha Nahjul Balagha ameandika hivi kuhusu hikma hizi za 40 na 41. Maneno haya yana maana na hikma ya hali ya juu. Amma tunachojifunza hapa ni kwamba, kama mtu anataka awe ni mwenye busara basi ni lazima kwake atafakari kwamba kabla ya kutamka neno lolote. Ajiulize kwanza, je hili ninalotaka kulisema ni sahihi au si sahihi. Lina faida au halina faida. Halina madhara kwa yeyote? Ndipo atamke. 

Hata wakati tunapotaamali na kuangalia kwa mazingatia makubwa matendo ya ibada, kumtii Mwenyezi Mungu, tunapoangalia kwa kina madhambi na mambo maovu tutaona kuwa, sehemu kubwa ya ibada inafanyika kwa ulimi na sehemu kubwa ya madhambi pia inafanyika kwa ulimi. Wakati mtu anaposhindwa kudhibiti ulimi wake, husababisha mabalaa makubwa na kinyume chake ni hivyo hivyo, wakati mtu anapokuwa na nguvu za kudhibiti ulimi wake, huwa chemchemu ya baraka na mambo mengi ya kheri. 

Katika khutba ya 176 ya Nahjul Balagha, Imam Ali (AS) anasisitiza wajibu wa kudhibiti mtu ulimi wake. Kudhibiti ulimi ni hatua ya awali ya kujijenga mtu katika maadili mema. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. 

Tags