Jun 17, 2024 02:32 UTC
  • Jumatatu, tarehe 17 Juni, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Dhulhija 1445 Hijria sawa na tarehe 17 Juni 2024.

Leo tarehe 10 Dhilhaji ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja kati ya sikukuu kubwa za Kiislamu.

Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka huchinja mnyama kutekeleza amri ya Mola kwa ajili ya kujikurubisha kwake na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii adhimu, Ibrahim (as).

Mwenyezi Mungu SW alijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mtoto wake kipenzi, Ismail (as), naye akatii na kujitayarisha kuitekeleza. Alimlaza chini na kuanza kukata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja; ndipo Mwenyezi Mungu alipomtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanawe, Ismail.

Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawafunza wanaadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu SW. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa. 

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita sawa na tarehe 17 Juni 1925, ulitiwa saini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za vijidudu na kemikali mjini Geneva Uswisi.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utumiaji vitani wa aina yoyote ya silaha za vijidudu, gesi zinazoua, sumu za kemikali na nyinginezo kama hizo ulipigwa marufuku. Licha ya kufikiwa makubaliano hayo, lakini baadhi ya nchi bado ziliendelea kutumia silaha hizo zilizopigwa marufuku duniani. Ujerumani ilitumia silaha za kemikali katika Vita vya Kwanza vya Dunia, Marekani katika vita vya Vietnam na utawala wa zamani wa Iraq kutumia silaha hizo wakati wa vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, wakazi wa kisiwa cha Iceland walifanikiwa kupata uhuru wao kutoka mikononi mwa Denmark.

Kisiwa cha Iceland kiligunduliwa tarehe 10 Julai 874 Miladia na kuanzia wakati huo, ndipo wahajiri wa Norway, Scotland na Ireland wakaanza kuishi katika kisiwa hicho. Hadi kufikia karne ya 13 Miladia ilikuwa ni nchi huru hata hivyo muda baadaye iliunganishwa na Norway na kisha Denmark. Mwaka 1874 Denmark iliruhusu kuundwa baraza la watunga sheria (yaani bunge) katika kisiwa hicho cha Iceland.

Aidha serikali ya ndani ya kisiwa hicho iliendelea kufuatilia haki zake zaidi ingawa bado kiliendelea kutambuliwa kuwa sehemu ya Denmark, hadi tarehe 17 Juni 1944 ambapo kulitangazwa kuvunjwa muungano huo baada ya kurejelewa maoni ya wakazi wa Iceland. Kuanzia wakati huo, wakakazi wa Iceland wanaitambua siku kama ya leo kuwa siku ya kitaifa.

Na tarehe 10 Dhulhija miaka 9 iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na uzembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia.

Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 7 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.   

Maafa ya Mina

 

Tags