Jul 01, 2024 06:02 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (55)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 55 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 55 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 48.

الظَّفَرُ بِالْحَزْمِ، وَ الْحَزْمُ بِإِجَالَةِ الرَّأْیِ، وَ الرَّأْیُ بِتَحْصِینِ الْأَسْرَارِ

Ushindi hupatikana kwa kuangalia mbali, kuangalia mbali kunakuja kwa kutumia vizuri fikra na fikra sahihi hupatikana kwa kulinda siri.

Kila mtu huwa anapigania kupata ushindi na mafanikio katika nyuga tofauti za maisha yake. Hikma hii ya 48 ni moja ya hikma bora na nzuri kabisa zilizomo kwenye kitabu cha Nahjul Balagha. Hikma hii inamhusu kila mtu awe mwanamme awe mwanamke, awe mtoto mdogo awe mtu mzima, awe Muislamu asiwe Muislamu, kila mtu ambaye anataka afanikiwe katika maisha yake basi ana wajibu wa kuzingatia mambo hayo. Ana wajibu wa kuwa na mtazamo wa mbali; mtazamo wa mbali nao unapatikana kwa kutumia vizuri fikra na akili, na fikra nayo hupatikana kwenye kulinda na kuficha siri.

 

Kawaida wanadamu huwa na wasiwasi sana na mustakbali wao kwa sababu hawana elimu yoyote kuhusu watakayokutana nayo sekunde moja tu baadaye. Lakini kama watu watakuwa na tadibiri na mtazamo wa mbali, bila ya shaka yoyote hupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Kuangalia mbali kwenye kila jambo kuna nafasi muhimu katika ubora na hatima ya jambo hilo kiasi kwamba, kama mwanadamu atakaa na kutafakari kuhusu matokeo na matunda ya jambo analotaka kulifanya huweza kujua kwa asilimia kubwa hasara na faida za jambo hilo na wakati huo huwa na nafasi ya kujipanga vizuri kukabiliana na hali hiyo. Anapozungumzia suala la kuangalia mbali, Imam Ali AS anasema, muono wa mbali ni kuangalia matokeo ya jambo ulilokusudia kulifanya na kushauriana na watu wenye hikma na busara kuhusu jambo hilo.

Inasikitisha kuona kuwa baadhi ya watu wana mtazamo finyu na usio sahihi kuhusu suala la kuangalia mbali na wanadhani ni kufanya mambo kwa woga na tahadhari ya kupita kiasi, wakati uhakika wa mambo ni kwamba kuwa na mtazamo wa mbali ni katika masharti ya lazima na ya kimsingi ya maamuzi yote ya kiakili na kimantiki.

Katika kipande cha pili cha hikma hiyo, Imam Ali AS anasema: Kuangalia mbali sharti lake ni kutumia vizuri fikra. Maana yake ni kwamba anayetumia vizuri fikra ni kama mpanda farasi ambaye hukagua kila shibri ya medani ya mapambano kabla ya kuanza vita ili kutathmini nukta zote za udhaifu na za umadhubuti. Hutafakari na kuangalia kwa kina pande zote za suala fulani, ubaya na uzuri wake ili awe na uwezo wa kuchukua maamuzi sahihi.

 

Katika hadithi yake moja, Imam Sadiq AS anasimulia kwa kusema, siku moja mtu mmoja alikwenda kwa Bwana Mtume Muhammad SAW na kumuomba ampe nasaha. Bwana Mtume alimuuliza, je una kifua cha kupokea nasaha ili nikunasihi? Yule bwana alijibu ndio. Hapo Mtume SAW alimwambia, basi nakuusia unapodhamiria kufanya jambo lolote lifikirie mwisho wake, ukiona lina manufaa endelea nalo na ukiona lina madhara, achana nalo.

Baadhi ya wakati na kwa ajili ya kupata ushindi na mafanikio, mtu hulazimika kutumia mipango mizito na tata na kwa sura tofauti na hulazimika kufanya siri kubwa katika jambo hilo kwani adui yake akitambua anaweza kuvuruga mipango yake yote. Ndio maana hapa Imam Ali katika sehemu ya mwisho ya hikma hii ya 48 anasema, fikra sahihi sharti lake ni kuhifadhiwa, ni kufanywa siri na kutotangazwa kwa kila mtu.

Ni vyema tuseme hapa kwamba, baadhi ya wakati mtu anaweza kuwa na siri yake, akaamua kumpa siri hiyo rafiki yake anayemwamini mno. Lakini huwa anasahau kwamba huyo rafiki yake naye anaweza kuwa na mtu mwingine anayemwamini mno hivyo humfichulia siri yake kwa rafiki yake mwingine anayemwamini mno tahamaki utaona siri hiyo imeenea midomoni mwa watu na si siri tena. Ndio maana pia Imam Sadiq AS akanukuliwa katika hadhiti nyingine akisema, usimfichulie rafiki yako siri zako zote na siri yako nzima, bali weka mipaka katika kufichua siri zako kwa kadiri ambayo iwapo adui ataamua kukudhuru asiweze kukudhuru kwa siri yako hiyo. Vile vile rafiki yako kuna wakati anaweza kugeuka na kuwa adui yako, ikiwa atakuwa anajua kwa undani kila siri yako, rafiki yako huyo wa zamani anaweza kuwa adui mbaya mno kwako hivi sasa. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.