Jul 25, 2024 04:35 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 25 Julai, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hjria sawa na Julai 25 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein AS na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya Bani Umayyah.

Msafara huo uliokuwa ukiongozwa na Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib AS ulifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala.

Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad SAW huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyyah wakitanguliwa na kichwa kilichotenganishwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein AS.   

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina.

Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China.

Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa. 

Vita vya China na Japan

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, Wapalestina 62 wasio na hatia  waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina.

Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina.   

Miaka 80 iliyopita katika siku kama ya leo, Reza Pahlavi maarufu kwa jina la Rezakhan mwasisi wa silsila ya Pahlavi nchini Iran alifariki dunia nchini Afrika Kusini baada ya kukalia kiti cha usultani kwa miaka 16 na kuwa uhamishoni kwa miaka mitatu.

Rezakhan alizaliwa mwaka 1257 Hijria Shamsiya sawa na mwaka 1878, katika mojawapo ya vijiji vya kaskazini mwa Iran. Mwaka 1299 Hijria Shamsiya, sawa na mwaka 1920, Miladia Rezakhan alipewa amri na Uingereza ya kufanya mapinduzi nchini Iran ili kulinda maslahi ya serikali ya London, wakati alipokuwa afisa wa jeshi la Iran. Baadaye akawa Waziri wa Ulinzi na kisha Waziri Mkuu.

Hatimaye mwaka 1304 Hijria Shamsiya sawa na mwaka 1925, Rezakhan alianzisha utawala wa silsila ya Qajar na kukalia kiti cha usultani nchini Iran licha ya kupingwa na wanazuoni na wanasiasa wapigania uhuru.   

Maiti ya Reza Pahlavi

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga na baharini huko kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.     

Na miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, kiwanda kikubwa zaidi cha kusafishia mafuta mazito ya matumizi ya vyombo vya moto kilifunguliwa katika mji wa Bandar Abbas kusini mwa Iran. Kiwanda hicho kikubwa zaidi cha aina hiyo duniani kilitengenezwa na wataalamu wa Iran. Kiwanda hicho ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi na muhimu ya mafuta nchini Iran. 

 

Tags