Alkhamisi, Oktoba 10, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria sawa na tarehe 10 Oktoba mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1321 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20.
Hisham aliyekuwa mtawala dikteta, alizaliwa mwaka 72 Hijria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijria. Hisham alikuwa mashuhuri kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlulbait wa Mtume (saw). Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Muhammad (saw) na alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake. Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati ya Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo.
Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-Malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah. ****
Siku kama ya leo miaka 630 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz.
Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi.
Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantwiq" na "Sharhu Mawaaqif Qadhi Adhdud-Diin Iji." ***
Siku kama ya leo miaka 594 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuthani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ibn Eyas, mwanahistoria mashuhuri wa Misri.
Ebn Iyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye taaluma ya lugha ya Kiarabu.
Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ibn Eyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiuz-Zuhuur fii Waqaaiul-Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake.
Aidha alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma.
Miaka 293 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko katika mji wa Nice Ufaransa, Henry Cavendish mwanafalsafa na tabibu wa Kiingereza.
Cavendish alikuwa mwalimu wa masomo ya fikizikia na kemia. Henry Cavendish alikuwa mtu wa kwanza aliyethibitisha kuwa gesi ya hyadrogen ni nyepesi zaidi kuliko hewa ya kawaida. Cavendish aliaga dunia mwaka 1810. ***
Tarehe 10 Oktoba miaka 143 iliyopita, kuliundwa muungano wa nchi tatu za Austria, Ujerumani na Italia. Kabla ya Italia kujiunga na muungano huo, awali kulikuwa na muungano wa mihimili miwili kati ya Austria na Ujerumani.
Moja ya vipengee vya muungano huo kilikuwa na kusaidiana nchi wanachama pindi mmoja wao atakaposhambuliwa. Muungano huo ulikuwa ukiongezewa muda kila baada ya miaka mitano. ***
Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, mfumo wa Jamhuri nchini China ulichukua hatamu baada ya kuangushwa mfumo wa Kifalme.
Katika kipindi cha kati ya mwaka 1907 na 1911 kulitokea uasi mara tano nchini China dhidi ya familia ya Kifalme ya Manchu. Uasi wote huo chimbuko lake kwa namna moja au nyingine lilikuwa ni fikra za kimapinduzi za Sun Yat-Sen mwanamapambano mashuhuri wa China.
Hata hivyo uasi wa tano ambao ulianza tarehe 9 Oktoba mwaka 1911 ulipelekea kutokea ukandamizaji mkubwa, kutiwa mbaroni watu na mamia ya wengine kunyongwa hali ambayo ililipua ghadhabu na hasira za watu. ***
Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, nchi ya Fiji ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na siku kama hii husherehekewa nchini humo ikijulikana kama siku ya taifa.
Fiji ilikuwa koloni rasmi la Uingereza tangu mwaka 1874 na Uingereza iliendelea kuukoloni muungano wa visiwa vya Fiji na ukoloni huo uliendelea kwa zaidi ya miaka 90.
Mwaka 1965 katiba mpya ilianza kutekelezwa huko Fiji ambapo sheria zilibuniwa kwa ajili ya kupigania mamlaka ya kujitawala nchi hiyo. ***
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Haji Mirza Khalil Kamarei, mfasiri wa Qur'ani Tukufu na mhadhiri wa chuo kikuu.
Ayatullah Kamarei alijifunza elimu za fiqih, usul-fiqih na masomo mengine ya kidini katika Hauza ya kielimu ya mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baadaye alianza kufundisha falsafa. Haji Kamarei ameandika vitabu vingi kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu.
Miongoni mwa vitabu hivyo ni tafsiri ya Qur'ani, sherhe ya Nahjul Balagha na kitabu cha maisha ya Imam Hussein (as) na mashahidi wengine wa Karbala. ***
Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa amri ya Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchini Iran kuliundwa Jumuiya ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu.
Kabla ya hapo taasisi hiyo ilikuweko katika zama za Ayatullah Burujerdi na kwa ajili ya kunufaika na mambo ya pamoja Madhehebu za Kiislamu, alikuwa akituma jumbe mbalimbali huko Cairo Misri ambazo zilikuwa zikikutana na kufanya mazungumzo na wasomi na wanazuoni wakubwa wa Kisuni. Safari na mazungumzo hayo yalikuwa na matokeo mazuri ambapo katika zama za Sheikh Shaltut akiwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha al-Azhar, maulamaa wa Kisuni katika chuo kikuu hicho waliyatambua rasmi Madhehebu ya Kishia.
Duru mpya ya jumuiya hii imeandaa uwanja wa kukurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu katika uga wa kiitikadi, kifikra, kifikihi na kielimu.