Jumanne, 17 Disemba, 2024
Leo ni Jumanne tarehe 15 Mfunguo Tisa Jamadithani 1446 Hijria mwafaka na tarehe 17 Disemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1410 iliyopita yaani tarehe 15 Jumadithani mwaka 36 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilitokea vita vya Jamal baina ya jeshi la Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kundi la waasi waliozusha vurugu na fitina.
Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahamili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia na kiapo chao cha utiifu.
Viongozi wa kundi hilo ambalo lilijulikana kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair, ambapo waliamua kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu.

Tarehe 15 Jumadithani mwaka 771 katika siku kama ya leo miaka 675 iliyopita, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu.
Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake.
Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.

Miaka 245 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza.
Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia.
Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama "electrochemical", aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 121 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Disemba mwaka 1903, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa.
Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur na Orville Wrights na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani.
Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipatwa na shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Dakta Muhammad Mufatteh alimu, mwanaharakati na mwanamapambano wa Kiirani aliuawa shahidi na makundi ya kigaidi.
Baada ya kumaliza masomo yake ya kimsingi alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Qum. Sambamba na kusoma masomo ya dini, Muhammad Mufatteh alikuwa akisoma pia katika Chuo Kikuu cha Tehran na kufanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika falsafa yaani PHD.
Baada ya kupata shahada hiyo akaanza kufundisha kama mhadhiri huku akiendesha harakati za mapambano dhidi ya utawala dhalimu wa Shah uliokuwa ukitawala hapa nchini Iran.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, sawa na tarehe 17 Disemba mwaka 1992 utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kisingizio cha kuuawa polisi wake mmoja wa mpakani, uliwabaidisha kusini mwa Lebanon viongozi 415 wa harakati ya Jihadul Islam na Hamas kutoka Palestina.
Baada ya serikali ya Lebanon kupinga hatua hiyo isiyo ya kibinadamu na kukataa kuwapokea Wapalestina hao, hasira na upinzani wa ulimwengu wa Kiislamu ulilifanya Baraza la Usalama kupitisha azimio nambari 977 lililolaani hatua hiyo ya Tel Aviv na kutaka kurejeshwa Wapalestina hao waliobaidishwa nchini kwao.

Tarehe 17 Disemba miaka 14 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia aliyejulikana kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliotawala kwa kipindi cha nusu karne.
Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.
Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya Chuo Kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin.
