Jumatatu tarehe 3 Machi 2025
Leo ni Jumatatu tarehe Pili Ramadhani 1446 Hijiria, sawa na tarehe 3 Machi 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 1106 iliyopita alifariki dunia Abdur Rahman Zujaji Nahavandi aliyekuwa mwanafasihi, mtaalamu wa lugha na faqihi wa karne ya 4 Hijria katika mji wa Damascus.
Alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa zama zake kama Ibn Dorayd na akafanikiwa kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa katika elimu hizo.
Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni "al Idhah".

Miaka 322 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uingereza.
Hooke alizaliwa mwaka 1635 huko kusini mwa nchi hiyo. Alifanya utafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia.
Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini yake na kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli.
Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa.

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, utawala wa Othmaniya na Russia zilisaini mkataba katika eneo lilopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano.
Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan.

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina.
Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa na kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ilikuwa ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan.

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Gujarat nchini India.
Serikali ya India ilitangaza kuwa, Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji hayo, lakini vyombo vingine huru vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ilikuwa ni zaidi ya 2000.
Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi lililokuwa limebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji hayo dhidi ya Waislamu.
