Jumatatu tarehe 24 Machi 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 23 Ramadhani 1446 Hijria sawa na Machi 24 mwaka 2025.
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu.
Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta zinazopatikana katika kitabu hicho.
Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 na alitumia karibu muda wa miaka 30 katika uandishi wake na kupewqa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Kipindi cha maisha yake kulitawaliwa na hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu.
Miaka 119 iliyopita katika siku kama leo, alifariki dunia mwandishi wa hadithi wa Kifaransa Jules Verne akiwa na umri wa miaka 77.
Verne alizaliwa Februari mwaka 1828 na alifanikiwa kuandika vitabu vingi na vya kuvutia vya hadithi ambapo ndani yake alielezea utabiri wake kuhusu ustawi wa sayansi ya mwanadamu.
Miongoni mwa athari hizo ni pamoja na vitabu alivyoviita Twenty Thousand Leagues Under the Sea, A Journey to the Center of the Earth na Around the World in Eighty Days.
Ni vyema kuashiria hapa kwamba, filamu mbalimbali zenye kutoa mafunzo kwa watoto na vijana zilitengenezwa kwa mujibu wa baadhi ya hadithi hizo za Jules Verne. ****
Leo ni siku ya kimataifa ya kupambana na maradhi ya kifua kikuu au Tuberculosis.
Tarehe 24 Machi mwaka 1882 daktari Robert Koch daktari na mtafiti wa Kijerumani alieleza uvumbuzi wake wa ugonjwa wa kifua kikuu katika mkutano uliofanyika Berlin Ujerumani na kwa mnasaba huo siku hii ya tarehe 24 Machi inatambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na maradhi ya Kifua Kikuu. ****
Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan.
Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini sana za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.
Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania. ****
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, Msikiti Mkuu wa mji wa Ganja ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Jamhuri ya Azerbaijan ulikarabatiwa na kufunguliwa upya baada ya kufungwa kwa miaka 70.
Msikiti huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1920 na kufunguliwa tena katika muongo wa 80 katika hafla iliyofanyika sambamba na kuswaliwa Swala ya jamaa.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, makumi ya misikiti ilikarabatiwa na kutumiwa na Waislamu kufuatia matukio ya kisiasa yaliyotokea Urusi ya zamani na katika jamhuri zake na pia kutokana na matakwa ya Waislamu wote wa Jamhuri ya Azerbaijan. ***