Mar 30, 2025 02:26 UTC
  • Jumapili, tarehe 30 Machi, 2025

Leo ni Jumapili tarehe 29 Ramadhani 1446 Hijria sawa na 30 Machi 2025.

Tarehe 29 Ramadhani miaka 798 iliyopita alizaliwa Jamaluddin Hassan bin Yusuf aliyepea laqabu ya Allamah Hilli, alimu, mtaalamu wa Hadithi na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu.

Awali Jamaluddin alisoma elimu mbalimbali kama fiq’hi, usulul fiq’hi na hadithi kwa baba yake na kufikia daraja za juu katika nyanja hizo. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi vya thamani kama “Tadhkiratul-Fuqahaa”, “Irshaadul-Adh’haan" na "Kashful Murad.”     

Siku kama ya leo miaka 639 iliyopita, alifariki dunia Nasiruddin Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn Furat, faqih, mwanahistoria na mhadhiri wa nchini Misri.

Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, kitabu ambacho kina historia na matukio ya karne ya sita Hijria.   

Katika siku kama ya leo miaka 158 Russia iliiuzia serikali ya Marekani ardhi yenye utajiri ya Alaska inayopatikana huko kaskazini magharibi mwa Canada na katika pwani ya bahari za Pacific na Arctic.

Russia iliiuza ardhi ya Alaska kwa Marekani kwa thamani ya dola milioni saba na laki mbili kutokana na mahitaji ya kifedha iliyokuwanayo.

Alaska ni jimbo la 49 la Marekani lenye ukubwa wa kilomita mraba zaidi ya milioni moja. Jimbo la Alaska pia lina thamani kubwa za kiuchumi kutokana na kuwa na maliasili nyingi za madini, khususan mafuta na dhahabu pamoja na mapato yanayotokana na uvuvi wa samaki.   

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, alifariki dunia mwanachuoni mkubwa wa Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Hussein Tabatabai Burujerdi, mmoja wa wasomi mashuhuri wa Iran.

Baada ya kumaliza masomo yake ya awali, alielekea mjini Najaf Iraq na kupata kusoma kwa walimu wakubwa wa kidini wa mji huo, kisha akarejea nchini Iran. Ayatullah Burujerdi kwa kushirikiana na wanachuoni wengine wakubwa wa Kiislamu alianzisha Umoja wa Ukurubisho wa Madhehebu ya Kiislamu.

Ayatullah Burujerdi licha ya kuandika vitabu kadhaa, alijenga misikiti kadhaa ndani na nje ya Iran, ukiwemo Msikiti wa Hamburg nchini Ujerumani.   

Miaka 49 iliyopita katika siku kama ya leo, maandamano makubwa ya "Yaumul Ardh" au Siku ya Ardhi yalifanyika huko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa tarehe 18 Oktoba mwaka 1975 mkutano wa kutetea ardhi ulifanyika katika eneo la Jalil kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Katika azimio la kwanza la mkutano huo, washiriki walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya utawala wa Kizayuni ya kughusubu ardhi za raia wa Kiarabu wa Palestina na kulaani vikali hatua hiyo.

Mkutano wa Jalil ulisisitiza kuwa, siasa za utawala wa Israel unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu zinakiuka haki za wananchi Waislamu wa Palestina katika ardhi zao na kwamba, utawala wa Kizayuni umepuuza wazi wazi hati ya haki za binadamu na misingi ya demokrasia na usawa. 

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kulianza kufanyika kura ya maoni ya nchi nzima kwa lengo la kuainisha mfumo utakaotawala hapa nchini.

Kura hiyo ya maoni ya kihistoria ilifanyika kwa muda wa siku mbili kutokana na kupokelewa kwa wingi na wananchi wa Iran. Asilimia 98.2 ya wananchi Waislamu wa Iran, walipiga kura ya kutaka mfumo wa Kiislamu utawale hapa nchini.