Jumatano, tarehe 23 Aprili, 2025
Leo ni Jumatano tarehe 24 Shawwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Aprili mwaka 2025.
Siku kama ya leo tarehe 3 mwezi Ordibehesht katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi Sheikh Bahauddin Muhammad Amili, maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, mwanazoni mkubwa wa taaluma mbalimbali za Kiislamu. Sheikh Bahai ambaye alikuwa ametabahari katika elimu nyingi kama fiqhi, nujumu, Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 953 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu zaidi ya mia moja ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Siku kama ya leo miaka 697 iliyopita alifariki dunia Ibnu Labban faqihi, mpokeaji hadithi, mfasiri wa Qur'ani na mwandishi wa Kiislamu.
Alizaliwa mwaka 679 Hijria katika mji wa Damascus na kupitisha kipindi cha ujana wake katika mji huo. Ibnu Labban alipata elimu za fiqih, usul-fiqih na Hadithi kutoka kwa walimu na maulamaa wakubwa wa zama hizo. Mbali na masomo hayo, Ibnu Labban alikuwa mahiri pia katika kutunga mashairi.
Msomi huyo wa Kiislamu alijishughulisha vilevile na kufundisha, kutoa waadhi na kufasiri Qur'an Tukufu. Kitabu pekee kilichochapishwa cha mwanazuoni huyo ni tafsiri ya Qur'ani Tukufu.

Katika siku kama ya leo miaka 409 iliyopita, aliaga dunia William Shakespeare, mshairi na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza wa Uingereza.
Shakespeare alianza kazi zake za usanii sambamba na kushiriki katika michezo ya kuigiza. Alipata umashuhuri mkubwa katika taaluma hiyo. Kazi zake za kisanii zilikuwa mchanganyiko wa sanaa iliyoakisi majonzi na vichekesho.
Miongoni mwa kazi maarufu zaidi za Shakespeare ni Romeo and Juliet, Hamlet, King Lear na The Merchant of Venice.

Miaka 167 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa mwanafizikia Max Plank wa Ujerumani ambaye pia alikuwa mtaalamu wa hisabati aliyebuni Nadharia ya Kwanta katika elimu ya fizikia.
Mwaka 1918 Max Plank alitunukiwa tuzo ya fizikia ya Nobel kwa kugundua nadharia ya kwanta. Plank ambaye alikuwa mpinzani mkubwa wa dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler, alifanya utafiti mkubwa katika nyanja za mwendojoto (sayansi ya uhusiano wa joto na kazi za mitambo), fizikia nadharia, joto, mnururisho na nuru na kuandika vitabu kadhaa katika medani hiyo.

Tarehe 3 Ordibehest miaka 41 iliyopita utawala wa Kibaath wa Iraq ulianzisha vita na mashambulizi dhidi ya meli za kubeba mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maji ya Ghuba ya Uajemi.
Baada ya kupita karibu miaka minne tangu Saddam Hussein aivamie ardhi ya Iran, Iraq ikisaidiwa na madola makubwa, ilichukua hatua ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran kwa kutumia wenzo wa kuzuia uuzaji nje mafuta ya Iran na badala yake wazidishe uzalisha wa mafuta katika nchi za Kiarabu ili kufidia nakisi ya mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa. Kwa misingi huo walianza kushambulia meli za kubeba mafuta za Iran na bandari za kupakia bidhaa hiyo hapa nchini.
Siku hiyo Iraq ikisaidiwa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ilitumia ndege za kivita za Super Standard za Ufaransa kushambulia kisiwa cha Khark na meli zilizokuwa zimebeba mafuta za Iran.

Katika siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Aprili 1992, alifariki dunia Satyajit Ray mwandishi na mtengeneza filamu mashuhuri wa India.
Satyajit Ray alizaliwa mwaka 1921, na filamu zake za kijamii ziligusa zaidi hisia za jamii ya wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kupendwa zaidi na wananchi wa India.

Na tarehe 23 Aprili miaka 30 iliyopita Shirika la Sayansi, Elimu na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) liliitangaza siku hii ya kuwa Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki za Mwandishi.
Lengo la kutangazwa siku hiyo ni kuonesha umuhimu wa kitabu na haki za waandishi wa vitabu, kuhamasisha watu kusoma vitabu, kuwapongeza watu wanaoandika vitabu kwa ajili ya kukuza na kustawisha utamaduni wa jamii ya mwanadamu na vilevile kuunga mkono na kusaidia ustawi wa sekta ya kusambaza vitabu.
Utamaduni wa kusoma vitabu umeshamiri zaidi katika dunia ya sasa hususan miongoni mwa tabaka la vijana kutokana na kusambaa zaidi vitabu vya elektroniki kupitia mitandao ya intaneti.
