May 17, 2025 02:18 UTC
  • Jumamosi, 17 Mei, 2025

Leo ni Jumamosi 19 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria mwafaka na 17 Mei 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 728 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Kamaluddin Farsi mwanahisabati mashuhuri wa Kiirani. Kamaluddin Farsi aliyekuwa amebobea pia katika elimu ya fizikia, alifanya safari wakati wa ujana wake katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutafuta elimu. Licha ya kuwa umri wake hapa duniani ulikuwa mfupi, lakini ameacha athari zenye thamani kubwa katika elimu ya hisabati na utambuzi wa nuru. Kitabu cha Tadhkirat al-Ahbab ndio kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu. ***

Kamaluddin Farsi

 

Miaka 277 iliyopita, katika siku kama hii ya leo alizaliwa Edward Jenner, tabibu wa Kiingereza aliyegundua chanjo ya ndui yaani (small pox). Tabibu huyo alifanikiwa kugundua chanjo ya ndui tarehe 14 Mei mwaka 1796 akiwa na umri wa miaka 45 wakati alipoelekea nchini India. Baada ya hapo ugonjwa huo wa ndui ulitibiwa kwa kutumia chanjo hiyo. Maradhi hayo ambayo wakati huo yalikuwa yakichukua roho za watu bila ya huruma, yalitokomezwa kabisa duniani mwaka 1979. 

Edward Jenner

 

Miaka 160 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kimataifa katika uwanja wa mwasiliano huko Paris Ufaransa. Utiaji saini huo ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 20 duniani. Kwa utaratibu huo kukawa kumepasishwa hati ya kuasisiwa Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana siku hii ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Mawasiliano. Mwaka 1932 kwa mujibu wa maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano wa Madrid Uhispania, jina la Muungano wa Kimataifa wa Telegrafu au Internatioanl Telegraph Union lilibadilishwa na kuwa, Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano au  International Telecomunication Union (ITU) na vipengee pamoja na sheria za jumuiya hiyo zikapitiwa upya. Kuanzia mwaka 1947, taasisi hiyo ikawekwa rasmi katika faharasa ya asasi zilizoko chini ya Umoja wa Mataifa. 

 

Katika siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, dola la Uingereza ambalo Palestina ilikuwa chini ya mamlaka yake, lilitoa kitabu kilichopewa jina la "Kitabu Cheupe" (The White Paper) na hivyo kukawa kumepigwa hatua nyingine katika njia ya kuasisiwa utawala ghasibu wa Israel. Wapalestina ambao walikuwa wakifahamu vyema himaya ya Uingereza kwa Wazayuni, waliukataa mpango uliokuwa umependekezwa katika kitabu hicho kwa ajili ya kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.   

 

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita mwafaka na tarehe 27 Ordibehesht mwaka 1388 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Muhammad Taqi Bahjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatullah Muhammad Taqi Bahjat Foumani