May 20, 2025 03:49 UTC
  • Jumanne, tarehe 20 Mei, 2025

leo ni Jumanne tarehe 22 Dhulqaada 1446 Hijria sawa na Mei 20 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1038 iliyopita yaani tarehe 22 Dhulqaada mwaka 408 Hijria Qamaria, alizaliwa Khoja Nizam al-Mulk, msomi na shakhsia muhimu wa kisiasa na kiutamaduni wa karne ya tano Hijiria mjini Tus, moja ya miji ya kaskazini mashariki mwa Iran.

Nizam al-Mulk alikuwa mmoja wa wasomi ambao walikuwa na taathira kubwa katika mabadiliko ya kisiasa na kiutamaduni katika karne hizo. Katika kipindi cha silsila ya utawala wa Masaljuki, Khoja Nizam al-Mulk aliteuliwa kushika wadhifa wa uwaziri ambapo aliendelea kujishughulisha na masuala ya uongozi kwa kipindi cha miaka 30 na kufanikiwa kuiletea Iran ya wakati huo, maendeleo makubwa hususan katika uga wa utamaduni.     

Miaka 910 iliyopita katika siku kama ya leo  yaani tarehe 22 Dhulqa'da mwaka 536 Hijria Qamaria, kazi ya kuandika tafsiri mashuhuri ya Majmaul Bayan ilimalizika.

Kitabu hicho kiliandikwa na Sheikh Tabarsi mmoja wa wafasiri wakubwa wa Qur'ani Tukufu na miongoni mwa maulamaa mashuhuri wa Iran aliyekuwa mashuhuri kwa jina la Aminul Islam kutokana na uaminifu na uchamungu wake. Kitabu hicho ni miongoni mwa tafsiri mashuhuri za Qur'ani kutokana na mbinu yake ya kuvutia katika mtazamo wa fasihi.

Tafsiri hiyo imechapishwa mara kadhaa katika nchi za Iran, Lebanon na Misri.

Miaka 519 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 20 Mei mwaka 1506 aliaga dunia baharia mashuhuri wa Kiitalia Christopher Columbus.

Columbus alizaliwa Septemba 21 mwaka1 451 huko kusini mwa Italia. Mwezi Agosti mwaka 1492 Christopher Columbus alianza safari yake kuelekea Bahari ya Atlantiki. Watu wengi wanamtambua Columbus kuwa mtu wa kwanza kutoka Ulaya aliyevumbua bara la America. Tangu wakati huo historia ya bara hilo iliandikwa kwa mujibu wa matakwa ya wazungu na wahamiaji wapya.

Historia hiyo iliambatana na machungu ya ukoloni kutoka maeneo tofauti ya dunia dhidi ya wakazi asili wa ardhi hiyo, huku ubaguzi ukiwa mhimili wa siasa kuu iliyotekelezwa na wahamiaji wazungu. 

Siku kama ya leo miaka 219 iliyopita alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mwanauchumi wa Uingereza.

Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa bunge la Uingereza kwa duru moja.

Vitabu muhimu vya mwanauchumi huyo wa Kiingereza John Stuart Mill ni vile alivyoviita "Principals of Political Economy" na "Principals of Political Science". Mill aliaga dunia mwaka 1873. 

John Stuart Mill

Katika siku kama hii ya leo miaka 123 iliyopita Cuba ilitangazwa kama jamhuri huru, na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo.

Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba.   

Katika siku kama ya leo miaka 91 iliyopita Yemen ilishindwa mwishoni mwa vita vilivyojiri kati yake na Saudi Arabia baada ya nchi mbili hizo kuhitilafiana juu ya suala la mpaka na kupelekea kusainiwa makubaliano ya Ta'if kati ya Imam Yahya wa Yemen na Mfalme Abdulaziz wa Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Yemen iliikabidhi Saudia maeneo ya Najran, Jizan na Asir kwa muda wa miaka 40. Saudia ilianzisha vita vipya dhidi ya Yemen mwezi April 2015 kwa ajili ya kuyadhibiti zaidi maeneo hayo. 

Miaka 65 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo.

Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru.   

Siku kama ya leo, miaka 62 iliyopita, mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 1963, kongamano la kihistoria la nchi za Afrika lilifanyika huko Addis Ababa, Ethiopia.

Madola mengi ya Kiafrika yalijinyakulia uhuru katika miaka ya 60 na 70, na katika kipindi hicho hayakuwa na uhusiano baina yao. Ili kuunda jumuiya ya kwanza iliyokusudiwa kuzikurubisha pamoja nchi za Afrika, kongamano la kwanza la nchi hizo lilifanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa tarehe kama ya leo. Kongamano hilo ilikuwa hatua ya kwanza ya kuasisiwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU.

Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao uliundwa mwaka 1963 kwa shabaha ya kusimamia maslahi ya nchi wanachama, kuhamasisha maendeleo ya bara hilo na kutatua migogoro kati ya nchi Afrika.

Tarehe 30 Ordibehesht mwaka mmoja uliopita Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi, aliyekuwa Rais wa Iran, aliaga dunia katika ajali ya helikopta. 

Ayatullah Ebrahim Raisi, alizaliwa mwaka 1339 Azar huko Mash'had, katika familia ya masharifu. Alipata elimu ya msingi na chuo cha kidini huko Mash'had na kisha akaenda kwenye Hauza ya Qum kuendelea na masomo ya juu. Alihesabiwa kuwa miongoni mwa wanafunzi hodari wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu na katika maandamano dhidi ya utawala wa kifalme wa Pahlavi.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Raisi aliendelea na shughuli za kiutendaji katika Idara ya Mahakama na aliteuliwa kuwa afisa katika Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Karaj akiwa na umri wa miaka 20. Nyota yake ilipanda haraka na kuwa mwendesha mashtaka katika mahakama za Karaj na baadaye Hamedani. Baada ya kusuluhisha kwa mafanikio kesi tata za kimahakama, Imam Ruhullah Khomeini (RA) alimteua yeye pamoja na Hujjatul Islam Nayyeri, kushughulikia matatizo ya kijamii katika mikoa mbalimbali.

Ayatullah Raisi aliwahi kuwa Mwendesha Mashtaka wa Tehran na kisha Mkuu wa Shirika la Ukaguzi Mkuu, na katika nafasi hii alifanya kazi ya kusasisha muundo ya taasisi hiyo. Mnamo 1394 Hijria Shamsia, alirudi Mash'had na, baada ya kifo cha Ayatullah Vaez Tabasi, alishika wadhifa wa kusimamia Haram ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Ridha (as). Wakati huo, alifanya mabadiliko makubwa katika muundo wa Haram ya Imam Ridha.

Mnamo 1400, Ayatullah Raisi alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mnamo Mei 19, 2024, aliaga dunia katika ajali ya ndege alipokuwa akirejea kutoka kwenye sherehe ya uzinduzi wa Bwawa la Giz Galasi huko Azarbajani Mashariki, akiwa pamoja na maafisa kadhaa wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Hossein Amir-Abdollahian.