Jumamosi, 24 Mei, 2025
Leo ni Jumamosi 26 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria, mwafaka na 24 Mei 2025 Miladia.
Miaka 724 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa faqihi, mfasiri, mtaalamu wa teolojia na mwanafasihi wa Kiislamu, Mas'ud bin Omar Taftazani huko Quchan, Kaskazini mwa Iran. Kwa kipindi kirefu cha umri wake, Taftazani alifanya safari katika miji ya Khorasan na Asia ya Kati kwa lengo la kutafuta elimu. Allamah Taftazani alianza kuandika vitabu akiwa bado kijana kutokana na uhodari na umahiri wake, na baadhi ya vitabu vya msomi huyo mkubwa wa Kiislamu vingali vinafundishwa hadi hii leo. Miongoni mwa vitabu hivyo ni al Mutwawwal, al Irshad na Mukhtasarul Maani.

Siku kama ya leo miaka 482 iliyopita, aliaga dunia mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus akiwa na umri wa miaka 70. Alizaliwa mwaka 1473 ambapo awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake. Inafaa kuashirikia hapa kuwa, karne kadhaa kabla ya Corpenicus, mnajimu na msomi maarufu Muirani, Abu Raihan Biruni alikuwa tayari ameshavumbua ukweli kuwa sayari ya dunia huzunguka jua. Katika moja ya vitabu vyake, Corpenicus ameashiria ukweli huo.

Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita, nchi ya Ecuador ilipata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Muhispania. Ecuador ni moja ya nchi za Amerika ya Kusini ambayo kupitia uongozi wa Simón Bolívar mwanamapinduzi maarufu wa Venezuela, ilifanikiwa kuwa huru na kujiunga na umoja wa Colombia Kubwa. Hata hivyo umoja huo ulisambaratika haraka na kufanya nchi wanachama wa umoja huo ikiwemo Ecuador kuasisi mfumo wa jamhuri.

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane. Uvamizi dhidi ya mji huo ulijiri mwanzoni mwa vita vya miaka minane vya kulazimishwa Iran na Iraq. Siku hii inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuwa, "Siku ya Muqawama na Ushindi".

Katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, nchi ya Eritrea iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika ilijitenga na Ethiopia na kujitangazia uhuru. Mwaka 1936 Miladia Italia iliikalia kwa mabavu Eritrea iliyokuwa ikihesabiwa katika zama hizo kuwa sehemu ya ardhi ya Ethiopia. Mwaka 1953, Italia iliirejeshea Ethiopia ardhi hiyo. Hata hivyo wananchi wengi wa nchi hiyo waliokuwa wakitaka uhuru walianzisha harakati za ukombozi dhidi ya serikali ya Ethiopia. Mwaka 1991, Harakati ya Ukombozi wa Eritrea ikisaidiana na wanamapinduzi wa Ethiopia walihitimisha utawala wa kidikteta wa Mfalme Mengistu Haile Mariam, na wakakubaliana kuanishwa mustakbali wa Eritrea mwaka 1993 kupitia kura ya maoni. Washiriki wengi wa kura hiyo ya maoni walipiga kura ya kutaka kujitawala Eritrea.

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, vikosi vya utawala dhalimu wa Israel vililazimika kuondoka kwa madhila katika eneo la kusini mwa Lebanon baada ya kulikalia kwa mabavu eneo hilo kwa muda wa miaka 22. Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya wananchi wa kusini mwa Lebanon. Mwaka 1982, majeshi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalishambulia Lebanon na kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Beirut. Hata hivyo kutokana na wananchi hao kuathirika na mafunzo ya kutokubali dhulma hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, nchini Lebanon kulianzishwa harakati za mapambano ya Kiislamu dhidi ya majeshi vamizi ya utawala haramu wa Israel. Harakati ya Hizbullah ilikuwa na nafasi muhimu na ya kuzingatiwa mno katika kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon toka katika makucha ya utawala dhalimu wa Israel.
