Jun 06, 2025 02:18 UTC
  • Ijumaa, Juni 6, 2025

Leo ni Ijumaa 10 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria mwafaka na 6 Juni 2025 Milaadia.

Leo, tarehe 10 Dhilhaji, ni sikukuu ya Idul Adh'ha, moja kati ya sikukuu kubwa za Kiislamu.

Katika siku hii mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu waliokwenda Makka huchinja mnyama kutekeleza amri ya Mola kwa ajili ya kujikurubisha kwake na kuhuisha kumbukumbu ya Nabii adhimu, Ibrahim (as).

Mwenyezi Mungu SW alijaribu imani na ikhlasi ya Nabii huyo kwa kumwamuru amchinje mtoto wake kipenzi, Ismail (as), naye akatii na kujitayarisha kuitekeleza. Alimlaza chini na kuanza kukata shingo yake lakini kisu kilikataa kuchinja; ndipo Mwenyezi Mungu alipomtumia mnyama wa kuchinja badala ya mwanawe, Ismail.

Tukio hili lenye ibra na mafunzo tele linawafunza wanaadamu somo la kujitoa mhanga, kujisabilia kwa ajili ya Allah, kushinda matamanio na matakwa ya nafsi na kusalimu amri mbele ya amri za Mwenyezi Mungu SW. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii kubwa.   

Siku kama ya leo, miaka 226 iliyopita, alizaliwa Alexander Pushkin, malenga na mwandishi mkubwa wa Urusi mjini Moscow.

Pushkin, alipata umaarufu mkubwa mwaka 1820, baada ya kusambaza majmui ya kitabu kilichosheheni mashairi. Muda mfupi baadaye malenga huyo akatunga shairi lililohusu uhuru, suala lililopelekea kubaidishwa kwake.

Katika shairi hilo Alexander Pushkin alielezea kwa kina umuhimu wa uhuru.   

Alexander Pushkin

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi dhidi ya ardhi ya Lebanon.

Katika uvamizi huo, jeshi la Israel liliuvamia na kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Bairut. Aidha askari hao wa utawala haramu wa Kizayuni, waliharibu miundombinu, viwanda na viunga vya mji huo, sanjari na kutekeleza jinai mbalimbali dhidi ya wakazi wake.

Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa Wazayuni huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Mwezi Septemba mwaka huo huo, jeshi hilo likatekeleza mauaji ya umati dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika kambi mbili za sabra nashatila karibu na mji mkuu wa Lebanona, Bairut. Hata hivyo mwezi Mei mwaka 2000, kufuatia ushindi wa wanamapamgano wa Hizbullah, wanajeshi vamizi wa Israel walilazimika kuondoka kwa madhila katika maeneo yote ya Lebanon waliyokuwa wameyakalia kwa mabavu. 

Mauaji ya Sabra na Shatila

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 6 Juni 1984, jeshi la India lilishambulia hekalu kubwa la Masingasinga lililojulikana kama Hekalu la Dhahabu katika mjini wa Amritsar makao makuu ya jimbo la Punjab, magharibi mwa India na kuua waasi wa Kisingasinga wasiopungua 1,000.

Serikali ya India ilidai kuwa shambulio hilo lilifanywa baada ya kupatikana habari za kufichwa silaha nyingi kwenye hekalu hilo, kwa shabaha ya kuanzisha uasi na mashambulizi dhidi ya serikali kuu.

Masingasinga hao nao walilipiza kisasi kwa kumuuwa Indira Ghandi, Waziri Mkuu wa India mwaka huohuo, kiongozi ambaye ndiye aliyetoa amri ya kushambuliwa hekalu hilo.   

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita tarehe 16 Khordad 1368 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 6 Juni, mwaka 1989 mamilioni ya wananchi wa Iran waliokuwa na huzuni kubwa waliuzika mwili wa Imam Khomeini (MA) Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, karibu na makaburi ya mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran ya Kiislamu, ya Behesht Zahra (as), pambizoni mwa mji wa Tehran.

Zaidi ya wananchi na Waislamu milioni kumi kutoka miji mbalimbali hapa nchini na nje ya nchi walishiriki kwenye mazishi hayo ya kihistoria. Kabla ya hapo wananchi wa Iran, waliuaga mwili wa Imam Khomeini, katika eneo la Musalla hapa mjini Tehran, na baadaye walielekea eneo la Behesht Zahra kwa ajili ya mazishi.

Na tarehe 10 Dhulhija miaka 10 iliyopita katika sikukuu ya Idil Adh'ha ardhi tukufu ya Mina huko Saudi Arabia ilikuwa machinjio ya maelfu ya mahujaji wa Nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu kutokana na uzembe wa maafisa na wasimamizi wa Hija wa Saudia.

Siku hiyo ilishuhudia tukio baya zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 3 asubuhi wakati baadhi ya mahujaji walipokuwa wakielekea eneo la Jamarat kumpiga mawe Shetani. Ghafla maafisa wa Saudi Arabia walifunga barabara za kuelekea eneo hilo na kukatokeo msongamano mkubwa kupita kiasi wa maelfu ya mahujaji, suala lililosababisha vifo vya zaidi ya mahujaji 7 kutoka nchi mbalimbali duniani.

Mahujaji 464 wa Iran pia waliaga dunia katika tukio hilo ambazo lilidhihirisha tena uzembe na kutokuwa na uwezo wa kusimamia vyema ibada ya Hija wa serikali ya Saudia.