Jul 13, 2025 02:38 UTC
  • Jumapili, 13 Julai, 2025

Leo ni Jumapili 17 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na 13 Julai 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1961 iliyopita, moto mkubwa ulitokea huko Roma mji mkuu wa utawala wa kifalme wa Roma. Sehemu kubwa ya mji wa kihistoria na mkongwe wa Roma iliungua na wakazi wengi wa mji huo walipoteza maisha yao kutokana na moto huo. Moto huo ulikuwa kisingizio tosha kwa Nuren mtawala mmwagadamu wa Kirumi ambaye aliwauwa kwa umati watu zaidi ya laki moja na baadaye kuwatuhumu Wakristo kuwa ndio walioanzisha moto huo. ***

 

Miaka 625 iliyopita katika siku kama ya leo, liliundwa jeshi la kale zaidi duniani nchini Uswisi. Jeshi hilo la kale zaidi duniani hadi hii leo limebakia kama lilivyokuwa na hata mavazi ya wanajeshi wake hayajabadilika. Idadi ya wanajeshi wa jeshi hilo dogo lakini lenye nidhamu kubwa ni watu 83. Jeshi hilo ambalo wanachama wake daima huwa raia wa Uswisi, liliundwa kwa ajili ya kulinda viongozi wa Kikatoliki wa wakati huo na hii leo baada ya kupita zaidi ya miaka zaidi ya 600 tangu liundwe, jeshi hilo lina jukumu la kumlinda Papa wa Kanisa Katoliki huko Vatican.  ***

 

Siku kama hii ya leo miaka 549 iliyopita Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa zaidi wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria alifariki dunia katika mji wa Harat katika Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran.  Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Silsilatu al Dhahab", Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharestan." 

Mahali alipozikwa Nuruddin Abdulrahman Jami

 

Siku kama ya leo miaka 494 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebanon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni Jame Abbasi na Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrihul Aflak na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan, Iran. 

Sheikhh Bahai

 

Katika siku kama ya leo miaka 254 iliyopita, baharia na nahodha mashuhuri wa Kiingereza aliyejulikana kwa jina la James Cook alikamilisha safari yake ya kitafiti na kielimu ya kuelekea The Great Southern Continent. Safari hiyo ilikuwa imeanza tarehe 26 Julai mwaka 1768. Safari hiyo ndefu iliishirikisha pia timu ya watalaamu wa elimu ya Sayansi Asilia au Natural Science kwa kimombo. Wataalamu hao walikuwa na nia ya kufanya utafiti wa kielimu kuhusiana na mimea pamoja na viumbe wanaopatikana katika maeneo hayo. ***

James Cook

 

Miaka 34 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 22 Tir 1370, Hijria Shamsia aliaga dunia, Allamah Sayyid Tahir Sayyidzadeh Hashemi, mmoja wa wanafikra wa Kiirani. Aliaga dunia katika viunga vya mjii wa Kerman ulioko magharibi mwa Iran. Katika kipindi chote cha maisha yake, Sayyyidzadeh Hashemi alijishughulisha na uenezaji na usambazaji wa maarifa ya Kiislamu kupitia kufundisha na kulea wanafunzi wa masomo ya dini, kutoa mawaidha na kuandika vita.  Kwa hakika alimu huyu ametoa huduma kubwa katika uwanja huu. Allamah Sayyidzadeh Hashemi alikuwa ametabahari pia katika fani ya hati. Alimu huyo alikuwa akizifahamu vizuri na kikamilifu lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kikurdi na alikuwa mahiri pia katika utunzi wa mashairi na ameacha athari nyingi katika uwanja huo kwa lugha hizo tatu.

Allamah Sayyid Tahir Sayyidzadeh Hashemi

 

Na tarehe 13 Julai ni siku ya kumbukumbu ya  Romania kujipatia uhuru kutoka kwa Utawala wa Othmania. Kijiografia Romania ipo kusini mashariki mwa Ulaya na magharibi mwa Bahari Nyeusi. Romania ina zaidi ya wakazi milioni 22 na dini rasmi ya nchi hiyo ni Ukristo na madhehebu ya Othodox ndiyo yenye wafuasi wengi. Nchi hiyyo ilikuwa chini ya utawala wa Othmania kuanzia karne yay 15. Hata hivyo mwaka 1877 Romania ikaungana na Russia katika vita dhidi ya utawala wa Othmania. Hatimaye katika siku kama ya leo Romalia ikajipatia uhuru na miaka mitatu baadaye ikawa imepata uhuru kamili.

Bendera ya Romania