Jul 17, 2025 04:23 UTC
  • Jumatano, tarehe 16 Julai, 2025

Jumatano tarehe 20 Muharram 1447 Hijria, sawa na Julai 16 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea.

Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili.

Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.   

James Parkinson

Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni.

Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani.

Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliopangwa kukabidhiwa katika operesheni hiyo waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Hizbullah.

Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantar ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.   

Na katika siku kama hii ya leo miaka 10 iliyopita alifariki dunia qarii mashuhuri wa Misri, Sheikh Sayyid Mutawalli Abdul Aal.

Alizaliwa Aprili 1947 katika familia ya wachamungu nchini Misri na aliweza kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu akiwa na umri wa miaka 12.

Alianza kujifunza qiraa ya Qur'ani Tukufu kwa kuiga mitindo ya maustadhi bingwa kama vile Sheikh Abdulbasit Abdusamad na Sheilh Mustafa Ismail.

Katika umri wake uliojaa baraka za Qur'ani, Sayyid Mutawalli Abdul Aal alitembelea nchi nyingi duniani kama qarii na pia jaji wa mashindano ya Qur'ani. Alifariki dunia Julai 16, 2015 akiwa na umri wa miaka 68.

Sayyid Mutawalli Abdul Aal