Jumapili, 23 Novemba, 2025
Leo ni Jumapili mwezi Pili Mfunguo Tisa Jamadithani 1447 Hijria ambayo inasadifiana na 23 Novemba 2025 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, "Kamati ya Kitaifa ya Ulinzi" ya Iran iliundwa katika mji wa Qom Iran wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya jeshi la Urusi ya zamani kuivamia Iran wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na kusonga mbele hadi maeneo ya karibu na Tehran na kulivunjwa Bunge la Taifa, idadi ya wabunge, maulama wa ngazi za juu na wafanyabiashara kutoka Tehran waliondoka mji mkuu kuelekea Qom na kuanzisha Kamati ya Ulinzi ya Taifa huko Qom. Katika hali hii, amri ya jihadi dhidi ya Warusi ilitolewa na wanazuoni. Ni katika siku hizo ambapo, vikosi vya jeshi la Urusi viliuteka mji wa Saveh na kusonga mbele kuelekea Qom. Wanachama wa Kamati ya Ulinzi ya Taifa walielekea Isfahan na kisha kuelekea Kermanshah. Baada ya kuiteka Saveh, vikosi vya Urusi viliikalia kwa mabavu miji ya Qom na Kashan na kuelekea Kermanshah kukabiliana na kamati hiyo. Kamati hii iliunda serikali ya muda huko Kermanshah na kuingia vitani na Warusi. Baada ya mapigano kadhaa kati ya vikosi vya Urusi na Uingereza na Kamati ya Ulinzi ya Taifa, kamati hii ililazimika kubadilisha eneo lake na kukaa kwa muda huko Qasr Shirin na Mosul huko Iraq, kabla ya hatimaye kwenda Istanbul. Kamati hii na serikali ya muda ilitangaza kuwepo kwake mwezi Mei mwaka uliofuata chini ya jina tofauti, lakini hatimaye ilivunjwa baada ya kumalizika kwa vita.

Katika siku kama ya leo miaka 88 iliyopita Jagadish Chandra Bose, msomi mtajika wa Bangladesh alifariki dunia. Jagadish alizaliwa Novemba 30 mwaka 1858 katika moja ya maeneo ambayo ni viungwa vya mji mkuu Dhaka. Miongoni mwa elimu alizokuwa amebobea Jagadish nii fizikia, sayansi ya mimea na akiolojia. Hata hivyo umashuhuri wa Jagadish Chandra Bose unatokana na kuvumbua kwake Radio na tanuri ya miale (Microwave).

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha hati ya kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.

Miaka 49 iliyopita katika kama ya leo, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.
