Aug 23, 2016 09:10 UTC
  • Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah (13)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Hii ni sehemu ya 13 ya kipindi cha Ufufuo na Safari ya Kurejea kwa Allah. Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulizungumzia hakika ya mauti.

Awamu ya mwisho ya maisha ya mwanadamu duniani na hatua ya kwanza ya maisha ya Akhera huwa ni kipindi cha Ihtidhar na sakaratul maut. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia dakika za mwisho za uhai wa mwanadamu hapa dunia yaani Ihtidhar na lahadha za sakartul mauti.

<<<<<  >>>>

Ihtidhar katika istilahi ina maana ya kuhudhuria mauti na roho ya mwanadamu kuanza kuhama dunia hii kuelekea ulimwengu mwingine au Akhera. Mtu anayekuwa katika hali hii huitwa "Muhtadhar". Katika kipindi hicho mwanadamu huona vitu visivyokuwa vya kimaada kama Malaika wa Mauti na kukata kbisa matumaini ya maisha ya dunia. Hata hivyo kuona huko si kwa kutumia jicho kiungo ili watu wengine wanaomzunguka muhtadhar nao waweze kumuona Malaika wa Mauti, la hasha. Kuona huko kunashabihiana kwa namna na kiwango fulani na kuona vitu katika ndoto kunakomtokezea mwanadamu wakati wa usingizi. Katika kipindi hicho mwanadamu huwa na hali makhsusi. Kwa upande mmoja huumizwa na kutengana na ndugu, jamaa na marafiki zake na kila kitu alichokusanya katika kipindi chote cha maisha yake, na wakati huo ndipo anapoelewa vyema maana ya maneno yanayosema, dunia hii si ya kudumu wala kubakia. Na katika upande mwingine makucha ya mauti na kifo yanamvuta polepole wakati huo huanza kusahau taratibu dunia na watu wake kutokana na mashaka na machungu ya mauati. Katika hali hiyo kwa mara nyingine tena hujiona akiwa katika dunia hii hii. Hali hii ya aina mbili za kukabiliana na dunia hii na lahadha nyingine kukabiliana uso kwa uso na kuona baadhi ya mambo ya ulimwengu ule, huitwa sakaratul maut. Kipindi hiki huwa kigumu sana na kichungu kupita kiasi kwa kila mwanadamu. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema kuhusu mashaka ya sakaratul maut na kipindi cha kutokwa na roho kwamba:

وَإِنَّ لِلْمَوْتِ لَغَمَرَات هِیَ أَفْظَعُ مِنْ أَنْ تُسْتَغْرَقَ بِصِفَة، أَوْ تَعْتَدِلَ عَلَى عُقُولِ أَهْلِ الدُّنْیَا..  

"Hakika mauti yana mashaka makubwa yasiyoweza kufikirika wala kufahamika kwa kutumia akili ya watu wa dunia hii.." (Nahjul Balagha, hotuba 220)

Qur'ani tukufu pia inawakumbusha wanadamu kipindi cha sakaratul mauti na kukata roho na kuwaambia kwamba wote watapitia kipindi hicho. Aya ya 19 ya Suratul Qaaf inasema:

وجَاءَتْ سَكْرَةُ الْمَوْتِ بِالْحَقِّ ذَلِكَ مَا كُنتَ مِنْهُ تَحِيدُ

"Na uchungu wa kutoka roho utamjia kwa haki. (wakati huo mwanadamu ataambiwa): Hayo ndiyo uliyokuwa ukiyakimbia".

Wakati wa kufariki dunia mwanadamu, pazia huondolewa hatua kwa hatua mbele ya macho yake. Wakati huo mwanadamu huelewa hakika ya amali na matendo yake, mtazamo na uwezo wake wa kuona huwa mpana zaidi na huanza safari ya kupitia matendo yake aliyotenda katika kipindi cha umri wake. Wakati huo huanza kujuta na kusikitika sana kwa aliyoyafanya lakini kwa bahati mbaya huwa hana tena fursa ya kubadili chochote, na makucha ya mauti huendelea kumyatia polepole.

Kipindi hiki cha mazonge ya kutokwa roho mwanadamu huwa anaangalia yanayojiri kandokando yake, na wakati huo huo hupewa uwezo wa kutupia jicho upande ule anakoelekea. Miongoni mwa mambo anayoyaona mtu aliyeko katika kipindi cha kukata roho ni nafasi yake katika Pepo au Jahannam ya ulimwengu wa Barzakhi. Imepokewa kutoka kwa Imam Ja'far Swadiq (as) kwamba amesema: Muumini anayekuwa katika sakaratul mauti anapooneshwa mafasi yake katika pepo ya Barzakhi, humwambia Malaika wa Mauti kwamba, niruhusu niwaeleze watu wa familia yangu kuhusu ninayoyaona. Malaika huyo humwambia kwamba, hana tena fursa ya kufanya hivyo.

Miongoni mwa mambo anayoyaona muhtadhar au mtu aliyeko katika hali ya kukata roho ni Malakul Maut yaani Malaika wa Mauti au wasaidizi wake. Imepokewa kwamba, iwapo mtu huyo atakuwa miongoni mwa waumini basi atapewa bishara njema na Malaika wa Rehma na kukaribishwa kwa muamala na mwenendo mzuri. Na kama atakuwa miongoni mwa watu waovu na wa motoni, basi huanza kupata adhabu na machungu kutokana na muamala mbaya anaokumbana nao.

Katika kipindi hiki cha Ihtidhar na kutokwa roho, mwanadamu huona matukio yote ya kipindi cha umri wake kama mkanda wa video na filamu. Hufurahi na kughiriki katika furaha kwa kushuhudia matendo na amali zake njema kwa kiasi ambacho si rahisi kwa watu wengine kukielewa. Kinyume chake, hupatwa na majonzi, simanzi na machungu kupita kiasi pale anaposhuhudia amali mbaya na madhambi yanayoakisi kipindi cha giza cha umri wake hapa duniani.

Ni vyema kusema hapa kuwa, wakati huu wa lahadha na kipindi cha sakaratul maut mwanadamu huona na kushuhudia amali zake kubwa na ndogo, mienendo yake hata nia na aliyoyakusudia moyoni.

Yumkini ikaulizwa hapa kwamba, inawezekana vipi kwa mwanadamu kushuhudia na kuona mambo yote makubwa na madogo aliyofanya katika kipindi chote cha umri wake katika dakika chache tu za kipindi cha kutokwa na roho? Kwa maneno mengine ni kuwa, mwanadamu anahitaji miaka 70 kwa mfano ili kuweza kushuhudia matendo na amali zote alizofanya katika kipindi cha miaka 70 ya umri wake.

Jibu la swali hili ni kuwa, zaman a wakati katika ulimwengu wa Barzakhi na Akhera unatofautiana na wakati wa dunia hii. Qur'ani tukufu inanukuu maneno yatakayosemwa na baadhi watu Siku ya Qiyama pale watakapoulizwa: Mumekuwa huko kwa muda gani? Watajibu: Kwa siku moja tu au sehemu ya siku moja. Aya za 112 na 113 za Suratu Muuminun zinasema:

 

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ * قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلْ الْعَادِّينَ

"Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka? Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanaoweka hisabu".

Kwa msingi huo inawezekana matukio ya kipindi cha miaka 70 duniani ukayaona katika lahadha ya muda mchache tu katika kipindi cha Ihtidhar na kutoka kwa roho.

Mandhari nyingine inayoshuhudiwa na mtu anayekuwa katika sakaratul maut na kutokwa roho ni kuwaona mashetani. Kwa kutilia maana kwamba, muhtadhar na mtu anayefariki dunia yuko katika dakika zake za mwisho duniani na kwamba baada ya mauti, shetani hataweza tena kumuona na kukutana naye, mashetani hufanya jitihada kubwa za kutaka kumshawishi katika dakika hizo za mwisho na kutia shaka katika imani na itikadi zake. Shetani ambaye haachi kufanya kila linalowezekana katika umri wake wote kwa ajili ya kumpotosha muumini na kuharibu imani yake, anatambua kwamba iwapo mwanadamu huyo atafariki dunia akiwa na imani na itikadi zake sahihi wakati wa Ihtidhar na kutokwa na roho, juhudi zake zote zitakuwa zimeambulia patupu. Kwa sababu hiyo hufanya jitihada za mwisho za kuteteresha na ikiwezekana kuondoa imani yake. Hata hivyo iwapo mwanadamu atakuwa ameimarisha ipasavyo imani yake moyoni wakati wa maisha yake hapa duniani, basi shetani hataweza kufanya lolote katika dakika hizo za mwisho. Ama iwapo imani yake haina misingi imara na ilikuwa ikitetereka na hata kutupiliwa mbali kwa mbinyo au jambo dogo tu katika maisha yake ya dunia, basi shetani atafanikiwa kumshawishi na kumteka katika dakika hizo za mwisho wa umri. Mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Swadiq (as) anasema: Mtu yeyote anapokuwa katika dakika za mwisho za uhai wake Iblisi humtumia mmoja kati ya mashetani ili amvute na kumuingiza katika ukafiri na kutia shaka katika imani yake. Mtu ambaye ni muumini wa kweli huwa haathiriki na njama hizo za shetani".

Shetani, wapenzi wasikilizaji, hutumia vibaya udhaifu wa imani za watu kwa ajili ya kuwapotosha. Aina yoyote ile ya upotofu katika itikadi na imani za hurafa huwa njia ya shetani kuweza kuingia katika moyo wa mwanadamu na kutia shaka katika imani na itikadi zake. Kwa msingi huo tunapaswa kufanya jitihada kubwa za kuimarisha imani na itikadi zetu na kuziba myanya yote inayoweza kutumiwa na shetani mlaaniwa. Mtume Muhammad (saw) amesema katika hadithi iliyoandikwa kwenye kitabu cha Kanzul Ummal kwamba: Simameni kandokando ya jamaa zenu wanaofariki dunia na wafanyieni talqini ya "Laa Ilaha illallah"; wapeni bishara ya kuingia peponi, kwa sababu hata wanaume na wanawake wenye subira na uvumilivu mkubwa huchanganyikiwa wakati huo, na katika kipindi hiki shetani humkurubia zaidi mwanadamu anayekata roho kuliko wakati wowote mwingine".

Sifa na tabia mbaya za mwanadamu zinatambuliwa kuwa miongoni mwa njia za shetani kumkurubia na kumteka mwanadamu. Sifa na tabia chafu kama ubakhili, husuda, kuwadhania watu vibaya, kiburi na kadhalika huwa barabara na njia za shetani kuingia katita roho ya mwanadamu.

Madhambi ni miongoni mwa nukta za udhaifu na myanya inayotumiwa na shetani kumteka mja hususan pale mwanadamu anaposhikilia tabia ya kutenda na kukariri dhambi hiyo. Kuiashiki na kuipenda sana dunia na vilivyomo pia ni miongoni mwa njia na mitego inayotumiwa na shetani  kumteka na kumpotosha mwanadamu. Shetani hutumia suala hilo kama nukta ya udhaifu na mtego wa kumteka na kumdhibiti mtu. Kwa mfano tu pale mwanadamu anapompenda mwanaye kupita kiasi na mapenzi yake hayo yakazidi hata mapenzi yake kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, shetani humwendea wakati anapokuwa katika hali ya kukata roho na kumtisha kwamba, kama hakukufuru atamuua mwanaye.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu zinatuhimiza kuwalakini na kuwasomea shahada mbili watu wanaokuwa katika hali ya Ihtidhar na kukata roho. Vilevile tumehimizwa kuwasomea Suratu Yaasi, Swaaffat, Ahzab, Ayatul Kursi bali sura nyingine za Qur'ani tukufu.

Ni jambo la dharura kwa muumini kuwa na hali zote mbili za hofu na matarajio ya hatima njema maadamu yu hai. Anapaswa kuwa na hofu kuhusu adhabu ya Mwenyezi Mungu na Akhera yake kutokana na amali na matendo yake, na wakati huo huo kuwa na matarajio ya rehma zisizo na kikomo za Mwenyezi Mungu Rahima.

Vilevile imepokewa katika hadithi kwamba, Mtume na Ahlibiti zake watoharifu huhudhuri kandokando ya muumini anayekata roho na kumsaidia katika kipindi hicho kigumu cha mauti na kufariki dunia. Suala hilo sambamba na kuwepo malaika wa rehma kandokando yake humpa faraja na matumaini muumini anayekuwa katika hali ya kukata roho. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.  

<<<<<   >>>>>               

 

 

Tags