Jumatano 24 Agosti 2016
Leo ni Jumatano tarehe 21 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na tarehe 24 Agosti 2016.
Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas yalianza. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad (saw) wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Mi'iraj na kwa sababu hiyo eneo hilo likawa na umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano hayo ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao taratibu walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina kwa kuungwa mkono na Uingereza, walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina wenye hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni hao maghasibu. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina.
Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo vikosi vya waitifaki viliikalia kwa mabavu Iran wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kusonga mbele haraka jeshi la Ujerumani ya Kinazi katika ardhi ya Urusi ya zamani kulizitia wasiwasi mkubwa Marekani, Ufaransa na Uingereza. Hii ni kwa sababu maslahi ya Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati na ya Mbali yangekuwa hatarini iwapo Ujerumani ingefanikiwa kuikalia kwa mabavu Urusi ya zamani, suala ambalo pia lingezidisha uwezekano wa Urusi kushinda vita. Kwa sababu hiyo nchi hizo tatu zilichukua uamuzi wa kutumia ardhi ya Iran kwa ajili ya kutuma misaada ya silaha na chakula huko Urusi. Kwa msingi huo mapema asubuni tarehe 3 Shahrivar mwaka 1320 Hijria Shamsia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini magharibi na jeshi la Uingereza kutokea kusini vilifanya mashambulizi ya anga, baharini na nchi kavu dhidi ya Iran. Baada ya majeshi hayo ya kigeni kushinda jeshi dhaifu la Shah yaliuteka na kuukalia kwa mabavu mji wa Tehran.
Na siku kama leo miaka 25 iliyopita, Ukraine ilipata uhuru toka kwa Umoja wa Kisovieti. Russia ilianza kuikalia kwa mabavu Ukraine ambayo wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland, katikati mwa karne ya 17. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo iliunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ilipatia uhuru wake.