Aug 24, 2016 16:36 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (15)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 15 ya mfululizo huu.

Kwa wale wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mtakuwa mnakumbuka kuwa baada ya kuzungumzia misingi mitatu ya kifikra ya Usekulari, yaani Umwanadamu (Humanism), Usayansi (Scientism) na Urazini (Rationalism) na kubainisha mitazamo ya Uislamu kuhusiana na kila moja kati ya misingi hiyo, katika kipindi kilichopita tulianza kutupia jicho msingi wa nne wa kifikra wa Usekulari ambao ni Uliberali au Uhuria, kwa kimombo Liberalism. Pamoja na mambo mengine tukaeleza kuwa Uliberali maana yake ni kupigania kuwa huru au kuwa asili kwa uhuru. Uhuru uliokusudiwa na Uliberali una sifa zake maalumu ikiwemo ya nadharia hiyo kujikita kupindukia kwenye nafasi ya mtu binafsi. Na tukabainisha kuwa kwa hakika Ubinafsi, kwa maana ya Individualism ndiyo kiini hasa cha Uliberali. Hata hivyo Usekulari umekosolewa katika hali na sura tofauti. Sehemu moja ya ukosoaji huo ambao umekuwa na taathira umefanywa na wanafikra wenyewe wa Magharibi. Kwa mfano “Ubinafsi wa kufurutu mpaka” kwa kimombo Extreme Individualism ambao una nafasi kuu katika Uliberali umekosolewa na wanafalsafa na wataalamu wengi wa Elimu Jamii. Wataalamu hao wanaitakidi kuwa Ubinafsi ni moja ya matokeo ya hali isiyoweza kuepukika ya kukwepa majukumu ya nadharia ya Ubinafsi wa Kufurutu Mpaka, ambao unatishia mno sifa za upendo kwa wengine, kutakia kheri wengine na utangamano wa kijamii. Aidha kulingana na mtazamo wa nadharia ya Ubinafsi aina yoyote ya tendo la pamoja ambalo halimfikishii manufaa mtu binafsi litachukuliwa kuwa limekengeuka lengo lililokusudiwa. Kwa mintaarafu ya hayo ubinafsi na umimi wa mtu binafsi hushamiri na kuongezeka na dhamira ya pamoja na akhlaqi za kijamii hufifia na kutoweka.

Kundi jengine la wanafikra linaitakidi kuwa kutokana na Uliberali kuegemea kwenye “utashi” na “akili ya kiuwenzo” ya mtu, na kujali uhuru usio na mipaka na kukwepa kuwajibika unasababisha kutoweka sifa njema za kiakhlaqi na mlingano katika akhlaqi. Wanafikra hao wanaamini kwamba kulifanya jambo la binafsi thamani za kiakhlaqi na kujipa uhuru wa kujivua na kila kitu husababisha fujo na hali ya mchafukoge wa kiakhlaqi na maingiliano holela ya kijamii. Miongoni mwao, wanafikra hao wanaitakidi kuwa hima na jitihada zote za wanadamu zimekuwa ni kupigania kuwepo sifa bora za kiakhlaqi na kuielekeza jamii katika kuzielewa sifa hizo, lakini Uliberali umetumia upanga wake wa makali ya pande mbili za Ubinafsi na Uhuru kuzitoa kafara sifa zote njema za kiakhlaqi.

Tunapotupia jicho vipimo na vigezo vya Kiislamu na kuvilinganisha na vya Uliberali, tunabainikiwa na nukta nyingi za kutafakari na zenye kutupa mguso mkubwa. Katika mtazamo wa Uislamu juu ya Ulimwengu, mwanadamu anatambulika kuwa kifitra ni kiumbe huru na mwenye hiyari; na uhuru na mamlaka ya kujiamulia mambo yake vinapewa hadhi na heshima ya kupigiwa mfano. Kwa mujibu wa Qur’ani tukufu, tofauti baina ya njia ya haki na njia ya batili iko wazi kabisa; na kila mtu yuko huru kuchagua njia anayotaka, na wala hakuna mtu awezaye kumlazimisha na kumpeleka kwa nguvu mtu mwengine kwenye njia ya haki. Tab’an yeye mwanadamu mwenyewe aliye na hiyari ya kuchagua, anabeba mas-ulia pia ya uchaguaji wake.

Uliberali unauchukulia uhuru wa mtu binafsi kuwa ndio ‘lengo’; lakini kwa mtazamo wa mafundisho ya Uislamu, uhuru wa binafsi sio ‘lengo’ kwa mwanadamu bali ni ‘wenzo’ na suhula ya kufikia lengo linalolingana na hadhi na utukufu wa kiumbe huyo. Kwa mtazamo wa Uislamu kuridhisha matamanio na kukidhi matashi ya binafsi sio lengo kwa mwanadamu, bali lengo la ustahiki wa kiumbe huyo ni kufikia ukamilifu wa kiutu na saada ya milele. Kwa hivyo uhuru wa binafsi ni utangulizi wa ukamilifu wa mtu, si ukamilifu wenyewe. Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu kwa namna ambayo anatakiwa aitumie njia ya uhuru wa binafsi na hiyari ya kuamua ili kufikia kwenye ukamilifu wake wa kiutu. Kwa hivyo Uislamu unautafsiri uhuru wa binafsi kulingana na lengo hilo.

Nukta nyengine muhimu ni kwamba japokuwa katika Uislamu uhuru una hadhi na nafasi ya juu lakini si tunu na thamani ya juu kabisa, bali kuna thamani nyengine kuu za msingi kama uadilifu ambayo ina hadhi na nafasi ya juu zaidi ya uhuru. Amirul Muuminin Ali bin Abi Talib (AS) ameuzungumzia umuhimu na nafasi ya uadilifu kwa kusema: “Mwenyezi Mungu aliyetukuka ameufanya uadilifu msingi wa kusimamia watu, nguzo yao ya maisha, sababu ya kujisafisha na dhulma na madhambi na mwanga wa taa ya Uislamu”. Uliberali wapenzi wasikilizaji unaufanya uadilifu wenzo wa kuutumikia uhuru; lakini Uislamu umeuweka uadilifu katika nafasi ya juu zaidi na kuufanya mstari mwekundu wa kutovukwa na uhuru wa mtu binafsi.

 

Tofauti nyengine iliyopo kuhusu uhuru wa mtu binafsi katika Uislamu na uhuru huo unavyotazamwa katika Uliberali ni kwamba katika mtazamo wa Uislamu, pamoja na mwanadamu kuwa huru lakini wakati huohuo ana mas-ulia pia; kwa hivyo ana majukumu na wajibu pia mbele ya wanadamu wenzake; na muhimu zaidi ya yote, mbele ya Muumba wake. Utekelezaji wa majukumu hayo una athari za moja kwa moja kwa kufuzu au kuharibikiwa kwake. Qur’ani tukufu inaizungumzia nukta hiyo katika aya ya 6 ya Suratu Tahrim kwa kusema:” Enyi mlioamini! Ziokoeni nafsi na za watu wenu na Moto; ambao kuni zake ni watu na mawe”. Uislamu haukubaliani na Ubinafsi wa Kufurutu Ada wa Uliberali wala Ujamii wa Kupindukia Mpaka wa Ukomunisti. Kulingana na mafundisho ya Uislamu, haki za mtu binafsi ni kitu chenye kuheshimiwa; lakini wakati huo huo maslahi ya jamii yanapasa kuzingatiwa. Kwa hivyo kadiri itakavyowezekana kuyalinda mawili yote hayo kwa pamoja, Uislamu haulitoi mhanga na kulifanya kafara moja kwa ajili ya jengine; lakini pale unapotokea mgongano baina ya matakwa ya mtu binafsi na maslahi ya jamii nzima na ikashindikana kuyakidhi yote mawili, kwa kawaida hutanguliza kwanza maslahi muhimu zaidi ya jamii.

Uislamu wapenzi wasikilizaji haukubaliani na uhuru mutlaki wa mtu binafsi; kama ambavyo nadharia zilizobuniwa na wanadamu pamoja na dini nyengine za mbinguni pia hazikubali uhuru huo kuwa mutlaki. Kwa mtazamo wa akili yoyote timamu uhuru mutlaki wa mtu binafsi ni jambo lisilowezekana kivitendo, bali huishia kuzusha fujo na mchafukoge. Tofauti iliyopo baina ya nadharia mbalimbali ni kuhusu vipimo na vigezo vinavyotumiwa na kila nadharia kuainisha mipaka ya uhuru wa watu. Kwa upande wa Uliberali, kuhatarisha uhuru binafsi wa mtu mwengine ndicho kizuizi na mpaka pekee unaowekewa uhuru binafsi wa mtu. Lakini akhlaqi, uadilifu na thamani nyenginezo za kiutu na kidini hazina nafasi yoyote ya kuainisha mpaka wa uhuru wa mtu binafsi. Katika suala hilo kuna tofauti ya msingi baina ya Uislamu na Uliberali.

Inshallah katika kipindi kijacho tutazungumzia uhuru binafsi kwa mtazamo wa Uislamu ili tuweze kuelewa kwamba dini hiyo sio tu si kizuizi cha uhuru wa mtu binafsi bali njia pekee ya kufikia uhuru wa kweli ni kufuata mwongozo uliowekwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya maisha ya mwanadamu. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kheri na fanaka maishani.

Tags