Dec 02, 2016 02:30 UTC
  • Ijumaa, tarehe Pili Disemba, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe Pili Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1438 Hijria sawa na tarehe Pili Disemba 2016.

Tarehe Pili Disemba kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa kote duniani. Japokuwa utumwa umefutwa katika maeneo mengi ya dunia lakini suala hilo lingali linashuhudiwa duniani katika kalibu ya utumwa mambo leo.

Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita kombora la kwanza la balestiki lililotengenezwa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilifanyiwa majaribio kwa mafanikio wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi hicho ambapo Iran ilikuwa chini ya vikwazo vikali vya nchi za Magharibi huku ikipigana na adui kulinda ardhi yake, awamu ya kwanza ya majaribio ya kombora hilo ilifanyika kwa mafanikio na uzalisahji wake ukaanza wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. 

Kombora la kwanza la balestiki la Iran

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipasishwa kwa wingi wa kura za wananchi. Katiba hiyo inasisitiza juu ya kuzingatiwa thamani za Kiislamu, uadilifu wa kijamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, katika mwaka 1368 Hijria Shamsiya, kipengee cha ziada kiliongezwa kwenye katiba hiyo, baada ya kupasishwa na Baraza la Wataalamu linalomteuwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuidhinishwa pia na wananchi. Kwa mujibu wa kipengee hicho cha nyongeza, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina vipengee 14 na vifungu 177.

Miaka 45 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Umoja wa Falme za Kiarabu ulipata uhuru kutoka Uingereza na kila inapowadia siku kama hii ya leo nchi hiyo huiadhimisha kama siku ya taifa. Ni vyema kutaja hapa kuwa tawala za kifalme za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza tangu mwaka 1920 Miladia. Uingereza iliasisi vituo vingi vya kijeshi katika eneo hilo, hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nchi hiyo ilidhoofika na ikaliweka katika ajenda yake suala la kuondoka katika Ghuba ya Uajemi.

Bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, hayati Fidel Castro alianzisha harakati ya kuikomboa nchi yake ya Cuba. Castro akiwa na lengo la kupambana na dikteta Fulgencio Batista, alianzisha mapambano ya silaha akiwa pamoja na wenzake kwa kuishambulia kambi ya kijeshi ya Moncada. Hata hivyo vikosi vya dikteta Batista viliikandamiza vibaya harakati hiyo na kumtia mbaroni Fidel Castro na kumfunga jela. Baada ya muda Castro alipelekwa uhamishoni. Hata hivyo baadaye aliunda kundi jingine la wapiganaji na kurejea Cuba alikoanzisha mapambano mapya. Hatimaye wanamapinduzi hao wa Cuba walifanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo hali iliyomfanya dikteta Fulgencio Batista akimbilie katika kituo cha kijeshi cha Marekani na baadaye kutoroka nchi hiyo.

Kiongozi wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro

Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, Laos ilipata uhuru kamili. Uhuru wa nchi hiyo ulipasishwa katika mkutano uliofanyika Geneva mwaka 1945 kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo na serikali kubwa duniani. Laos ilikuwa chini ya uongozi rasmi wa Ufaransa tangu mwaka 1893. Na ilipofika mwaka 1949, Ufaransa ililazimika kuipatia Laos uhuru wa kiasi fulani katika fremu ya Umoja wa Kifaransa, kufuatia mapambano ya ukombozi yaliyoanzishwa katika eneo la India na China.

Bendera ya Laos

Siku kama ya leo miaka 808 iliyopita, aliaga dunia Ibn Athir Jazari, mwanahistoria, mtaalamu wa fasihi na mpokezi mkubwa wa hadithi. Ibn Athir alizaliwa mwaka 555 Hijria huko Iraq na kujifunza taaluma mbalimbali. Alipata umashuhuri katika masuala ya lugha na fasihi ya Kiarabu. Kitabu maarufu zaidi cha Ibn Athir ni al Kamil fi Tarikh. Kitabu kingine cha mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ni Usdul Ghabah Fi Ma'rifatis Sahabah ambacho kinaeleza wasifu wa masahaba 7500 wa Mtume Muhammad (saw).

 

Tags