Dec 06, 2016 10:25 UTC
  • Familia Salama (15)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k.

Katika makala yetu ya leo tutaangazia cheo na hadhi ya mama katika familia. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki.

Mama ni neno maridadi na linalopendeza zaidi miongoni mwa kaumu na mataifa yote duniani. Mama ni siri katika siri za maumbile na uwepo wa dunia. Mwenye kufika katika cheo cha mama hupata hisia ya kipekee ya kuleta kiumbe duniani.

Mwenyezi Mungu SWT katika aya kadhaa za Qur'ani Tukufu amesisitiza kuhusu ulazima wa kuwatendea wema na ukarimu wazazi. Katika aya ya 23 ya Surat Israa, Allah SWT anasema:

"Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima."

 

Kwa kawaida kinamama ni maarufu kwa subira na kujitolea muhanga. Mama huacha raha na starehe zake na kujitolea kuwalea watoto na kuhakikisha wanapata utulivu. Mama kwa kawaida hufanya kila awezaleo ili kuwalea kwa njia sahihi watoto na kuwapa mafunzo ya kuwasaidia katika maisha.

Kwa hakika kazi ya mama mlezi ni muhimu sana yenye kuhitajia ujuzi na maarifa na iwapo kutafanyika kosa au uzembe katika malezi basi jambo hilo hupelekea kuharibika kizazi. Tabia na nyendo zote za mama huwa ni somo kwa mtoto.

Kwa muda mrefu, mtoto mchanga aghalabu huwa anakumbatiwa na mama tu na hata akiwa mkubwa kidogo na kuweza kutembea, wakati mwingi huupitisha akiwa na mama na kwa hivyo, mama huathiri pakubwa mtazamo na tabia za mtoto.

Wadhifa muhimu zaidi wa kina mama ni kuwapenda na kuwaonyesha mahaba watoto sambamba na kumlea mtoto ambaye atakuwa shakhsia  asiye na ubinafsi na uroho bali awe ni mwenye kushikamana, kuwa na urafiki na kushirikiana na wanadamu wengine katika jamii.

Kina mama wana wadhifa wa kuunga mkono, kuchunga, kuongoza, na kujenga shakhsia ya mtoto.

Kwa kawaida watoto huwa wategemezi na wenye kumfuata mama. Ukamilifu na sifa nyingine nyingi za mtoto akishafikia umri  juu ni kiashirio cha namna alivyokuwa mtegemezi kwa mama.

Aghalabu ya watu ambao katika zama za utotoni hawakuzingatiwa na mama na wala hawakupata fursa ya kukumbatiwa na mama kutokana na kutengana kwa sababu yoyote ile, hukabiliwa na hatari ya kukumbwa na mfadhaiko wa nafsi au msongo wa mawazo kuliko watu wengine.

 

Kuchukua mkondo potofu maishani, tabia mbaya, matatizo ya kinafsi na kijamii aghalabu hushuhudiwa miongoni mwa watu ambao katika zama za utotoni walitengana na mama zao au kwa bahati mbaya hawakupata mama mwenye huruma na mahaba. Aghalabu ya watoto waliopata malezi hayo yenye upungufu tuliotaja huwa ni watu wenye upungufu wa huruma wanapofikia umri wa juu na jambo hilo yamkini likaacha athari mbaya katika maisha yao.

Mama ana nafasi muhimu katika kumfunza mtoto kuhusu jamii na kuongoza fikra zake. Kutokana na kuwa mtoto huwa ni mwenye kuamini haraka na kufuata kikamilifu anachoambiwa katika miaka ya kwanza ya maisha, huwa anafuata kirahisi fikra za mama. Kwa msingi huo, katika malezi, mama anapaswa kuwa na lengo maalumu.

Mama anaweza kumuonyesha mtoto njia ya haki na sahihi kwa maneneo na kwa vitendo au tabia. Hii ni kati ya nukta asili na muhimu zaidi katika malezi.

Tunaweza kusema ufafanuzi wa wazi na bora zaidi katika kubainisha wadhifa na majukumu ya mama na haki ambayo mama anapaswa kumpa mtoto wake unapatikana katika maneneo ya Imam Sajjad AS, Imam wa Nne wa Mashia ambaye katika kitabu cha Risalatul Huquq kinachozungumzia haki za watu amebainisha haki ya mama ifuatavyo:

Tukizijia haki za ndugu, ni haki ya mama yako kuwa ni lazima utambue vyema kuwa alikuchukua kwa kiasi ambacho hakuna mtu yeyote yule anayeweza kumchukua mwingine zaidi ya hapo (yaani katika tumbo lake la uzazi), na kukulisha matunda ya moyo wake ambayo hakuna mtu yeyote yule mwingine amlishaye mwingine kwayo na akakuhifadhi (wakati wa ujauzito) kwa masikio yake, macho yake, mikono yake, miguu yake, nywele zake, viungo vyake, (kifupi ni kuwa alikulinda) kwa uwezo wake wote tena kwa furaha, kwa moyo mkunjufu na kwa uangalifu; akizivumilia hofu zote. Maumivu yote, shida zote na huzuni zote za (ujauzito), mpaka mkono wa Mwenyezi Mungu ulipokuondoa katika mwili wake, na kukuleta katika ulimwengu huu. Hapo alifurahi sana akikulisha wewe (na kuisahau njaa yake), akikuvika (japo kuwa yeye mwenyewe hakuwa na nguo), akikunyonyesha maziwa na maji (bila ya kujali kiu yake yeye mwenyewe). Akikuweka kivulini, (japo kuwa ilimbidi yeye mwenyewe kutaabika kwa joto la jua), akikupa kila faraja kwa taabu zake yeye mwenyewe, akikuweka ulale na yeye mwenyewe akibakia kuwa macho.

 

Na (kumbuka kuwa) tumbo lake la uzazi lilikuwa maskani yako, na mapaja yake yalikuwa makimbilio yako, na matiti yake yalikuwa chombo cha kukulishia na uzima wake wote ni hifadhi yako; ndiye yeye, wala si wewe, aliyekuwa na moyo wa ushujaa katika kuupoza huu ulimwengu ili kupata usalama. Hivyo basi, ni lazima ubakie kuwa mwenye shukrani kwake kwa ajili hiyo na huwezi kumshukuru ila kwa msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu."

Wapenzi wasikilizaji hiyo ilikuwa sehemu ya kitabu cha Imam Sajjad AS cha Risalatul Huquq au Haki ya Mtu kwa Watu ambapo hapo imebainishwa haki na hadhi ya mama.

Makala yetu ya familia salama inafikia tamati hapa kwa leo na ni matumaini yangu kuwa umeweza kufaidika na hivyo usikose kujiunga nasi katika makala yetu ijayo panapo majaliwa yake Mola.