Dec 06, 2016 10:59 UTC
  • Familia Salama (16)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia Salama. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Makala yetu ya leo itaangazia nafasi ya baba katika familia.

Baba na mama wana nafasi muhimu katika familia. Katika kila nyumba, mama huwa na jukumu la kusimamia familia kwa matazamo wa kihisia huku baba akiwa ni kiongozi na mkurugenzi wa nyumba. Watoto humtizama baba kama nembo ya uwezo, nguvu na tegemeo la wanafamilia wote.

Kutokana na harakati zake katika jamii, baba huwa na jukumu la kuweka msingi sahihi wa kielimu na ujuzi katika familia na yeye huwa ndiye mwenye kufuatwa na kutegemewa na watoto wanapotaka kuimarisha uwezo wao wa kielimu, ujuzi na pia muelekeo wa kimaisha.

Mama katika familia

Mtume Mtukufu wa Uislamu, Muhammad SAW anasema hivi kuhusu jukumu zito la baba: "Baba analazimika kuhakikisha kuwa anawapelekea watoto wake nyumbani riziki takasifu na ya halali."

Baba ana jukumu muhimu sana  la kulinda heshima yake na kuwa na maadili bora pamoja na hulka njema. Baadhi ya kinababa huwa na dhana potofu kwamba wanapokuwa na jukumu la kusimamia familia wanapaswa kutumia mabavu na ubabe katika kuamiliana na wanafamilia. Hii ni katika hali ambayo nguvu na uwezo wa mwanaume katika familia ni kwa ajili ya kuwaongoza wanafamilia na kudhamini utulivu ndani ya nyumba na katika familia.

Baba ambaye hutumia mabavu na ubabe mbele ya familia yake hapaswi kutegemea kuwaona watoto wake wakiwa ni warehemevu na wenye tabia njema na mapenzi kwa wazazi na katika jamii nzima kwa ujumla. Watoto wenye uhusiano mzuri na unaofaa na baba zao katika maisha yao ya usoni huwa ni watu wenye shakhsia ya kijamii na wenye mafanikio.

Aghalabu ya kinababa hutumia wakati wao mwingi wakiwa nje ya nyumba au mbali na wanafamilia kutokana na majukumu yao ya kikazi au kutafutia familia riziki na hivyo baadhi hughafilika kuhusu hali ya mke au wake na watoto. Kutokana na hali hiyo, wataalamu wa malezi wanasisitiza kuhusu kudumishwa uhusiano baina ya baba na wanafamilia wengine ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ukuruba na mapenzi miongoni mwa wanafamilia.

Mama katika familia

 

Utafiti umebaini kuwa, watoto wa kiume wanapofika katika umri wa miaka mitatu huanza kuiga tabia za baba. Kwa msingi huo kinababa wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kuwa na tabia na maadili mema ambayo yanaweza kuigwa na watoto. Katika kipindi hiki baba anapaswa kuwa ni mwenye kuzungumza kwa kauli nzuri na hata mavazi yake yanapaswa kuwa yanayofaa ili mtoto wa kiume aweze kuinukia na maadili mema. Katika kipini hiki baba anapaswa kuwa na uhusiano mzuri na amuonyeshe upendo mwanae wa kiume ili aweze kumsaidia kifikra na mtoto aweze kuhisi kuwa ana nguzo imara katika baba yake.

Uhusiano wa baba na watoto wa kiume na kike ni muhimu sana. Baba anapaswa kumuonyesha binti yake mahaba na upendo na kubainisha wazi hilo. Mahaba kama hayo kwa mtoto huwa na nafasi muhimu katika mustakabali hasa wakati binti anapofikia umri wa kuolewa. Mtume SAW anasema hivi kuhusu udharura wa baba kumzingatia na kumuonyesha mahaba binti yake: "Katika kuwapa zawadi watoto, wasichana wanapaswa kupewa kipaumbele."

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, baba ana nafasi muhimu katika familia na anaenziwa na kupewa hadhi kubwa. Mtume SAW anasema:

"Kumtii baba ni kumtii Mwenyezi Mungu na kumuasi baba ni kumuasi Mwenyezi Mungu."

Mtume SAW katika hadithi nyingine amesema kuwa: "Dua ya baba kwa mtoto wake ni kama dua ya mtume kwa umma wake."

Mafundisho ya dini ya Kiislamu pia yanasisitiza kuwa kumtendea wema na ihsani mama na baba huwa sababu ya kurefushwa umri wa mwanadamu hapa duniani na kughufiriwa madhambi huko Akhera. Imepokewa kwamba Sabaha Ibn Mas'ud alimuuliza Mtume (saw): Ni ipi amali inayopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu? Alisema Swala katika wakati wake. Nikamuuliza baada ya Swala? Akasema: Kuwatendea wema wazazi wawili. Nikasema: Baada ya hilo? Akasema: Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu..

Mama katika familia

 

Wapenzi wasikilizaji tunamaliza kwa kukumbusha kuwa, kuwaheshimu na kuwakirimu baba na mama na suala la kulea vyema watoto ni miongoni mwa mambo yaliyotiliwa mkazo sana katika aya za Qur'ani Tukufu na sira ya Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu. Umuhimu wa kuwaheshimu na kuwakirimu baba na mama unaonekana wazi zaidi pale tunapoelewa kwamba, suala hilo limewekwa sambamba na itikadi ya Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu ambapo ndiyo nguzo na msingi wa dini ya Uislamu. Katika aya za Qur'ani Tukufu Mwenyezi Mungu SW baada ya kuwaamuru wanadamu kumshukuru Yeye, anasisitiza juu ya udharura wa kuwaheshimu na kuwafanyia ihsani wazazi wawili. Aya za 14 na 15 za Suratu Luqman zinasema: "Na tumemuusia mwanadamu kuhusu wazazi wake wawili, mama yake amebeba mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu na akamwachisha ziwa baada ya miaka miwili, kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako, marejeo ni kwangu Mimi. Na kama wakikushikilia kunishirikisha Mimi na yale ambayo huna ilimu nayo basi usiwatii na kaa nao kwa wema duniani..."

 

 

Tags