Jan 16, 2017 09:46 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 14-18 (Darsa ya 705)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 705, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 14 na ya 15 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَى قَوْمِهِ فَلَبِثَ فِيهِمْ أَلْفَ سَنَةٍ إِلاَّ خَمْسِينَ عَامًا فَأَخَذَهُمُ الطُّوفَانُ وَهُمْ ظَالِمُونَ

Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka khamsini. Basi tufani liliwachukua, hali ya kuwa wao ni madhaalimu. 

فَأَنجَيْنَاهُ وَأَصْحَابَ السَّفِينَةِ وَجَعَلْنَاهَا آيَةً لِّلْعَالَمِينَ

Tukamwokoa yeye na watu wa safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote. 

Aya hizi na nyengine kadhaa zitakazofuatia zinazungumzia habari za yaliyojiri kwa watu wa kaumu zilizopita ambao waliishi katika zama za Mitume kama Nabii Nuh, Nabii Ibrahim na Nabii Musa (AS) na kubainisha jinsi watu hao walivyowaamini na kuwa pamoja nao Mitume hao au walivyowakadhibisha na kuupa mgongo wito wao. Kwa mujibu wa aya tulizosoma, japokuwa Nabii Nuh alitumia karibu miaka elfu moja kuwalingania watu wake tauhidi na kuwapa miongozo na indhari lakini ni wachache miongoni mwao waliomwamini; badala yake akthari ya watu hao walikhitari kufuata njia ya inadi na ukafiri. Kwa hivyo kwa amri ya Allah SW adhabu kali ya gharika ya mafuriko na tufani iliteremshwa, na wale wote walioipinga na kuikadhibisha haki waliangamizwa; na wale walioamini na kuifuata haki ndio waliookoka ili hilo liwe ibra na zingatio kwa kaumu zilizofuatia na kuzifanya zitambue kwamba ikiwa umma wa watu utafuata dhulma na kusimama kukabiliana na haki hatima yake itakuwa ni kuangamia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuamini na kukufuru kuna taathira kwa maangamizi na uokovu wa kaumu za watu papa hapa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kwa mtazamo wa Qur'ani kuishi umri mrefu wa miaka elfu moja ni jambo linaloyumkinika. Kwa hivyo ni jambo linalowezekana kwa mtukufu Imam Mahdi (AS) kuwa hai tangu miaka elfu moja na mia mbili iliyopita hadi sasa. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba subira na istiqama ni mambo ya lazima katika kazi ya tablighi na utangazaji dini, na wala mtu asiwe na matarajio ya akthari ya watu kuiamini na kuifuata haki.

Zifuatazo sasa ni aya za 16 na 17 za sura yetu hii ya al-A'nkabut ambazo zinasema:

وَإِبْرَاهِيمَ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاتَّقُوهُ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

Na Ibrahim pale alipo waambia watu wake: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo kheri yenu, ikiwa nyinyi mnajua.

إِنَّمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ أَوْثَانًا وَتَخْلُقُونَ إِفْكًا إِنَّ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّهِ لا يَمْلِكُونَ لَكُمْ رِزْقًا فَابْتَغُوا عِندَ اللَّهِ الرِّزْقَ وَاعْبُدُوهُ وَاشْكُرُوا لَهُ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ

Hakika nyinyi mnaabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawakumilikiini riziki yoyote. Takeni riziki kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndio mtarudishwa. 

Baada ya Nabii Nuh (AS), Nabii Ibrahim (AS) ni mtume wa pili kati ya mitume watano Ulul-'azm, ambaye aliwapa indhari na kuwahadharisha watu wake na kuabudu masanamu na kuwalingania imani na ibada ya Mungu Mmoja tu wa haki. Mtukufu huyo alilielezea hitajio la mali la watu kuwa moja ya sababu za msingi za kuabudu masanamu; hivyo aliwahutubu watu hao kwamba: ikiwa mnayaabudu masanamu haya kwa sababu ya umasikini na uhitaji, jueni kwamba masanamu haya hayana nafasi wala mchango wowote katika maisha yenu wala uwezo wa kukidhi mahitaji yenu. Lakini kama mtamwabudu Allah na mkawa washukurivu kwa neema zake, mtakuwa mumekomboka kuwa watumwa wa masanamu haya yasiyo na uhai na vilevile mtakuwa mumemsujudia yule ambaye ndiye anayekuruzukuni riziki yenu hapa duniani, na baada ya kifo pia, mwisho wenu na marejeo yenu ni kwake Yeye. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba ibada haiwezi kuwa na athari bila ya kuwa na taqwa na kujiepusha na madhambi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wale wanaoitakidi kwamba badala ya Mwenyezi Mungu kuna mwengine mwenye taathira katika maisha yao ya kimaada wametumbukia kwenye lindi la shirki. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kama ambavyo dini inawataka watu wajitume na kufanya bidii ili kuweza kujidhaminia mahitaji yao ya kimaada na kuishi maisha mazuri na ya raha inawataka pia wawe washukurivu kwa neema za Allah na wamwabudu Yeye Mola tu.

Darsa yetu ya leo inahatimishwa na aya ya 18 ambayo inasema:

وَإِن تُكَذِّبُوا فَقَدْ كَذَّبَ أُمَمٌ مِّن قَبْلِكُمْ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلاَّ الْبَلاغُ الْمُبِينُ

Na kama mkikadhibisha, basi zimekwisha kadhibisha umma kabla yenu. Na si juu ya Mtume ila kufikisha Ujumbe waziwazi.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia kwa kunukuu maneno ya Nabii Ibrahim (AS) kwa waabudu masanamu wa kaumu yake alipowaambia: mimi sina matarajio ya kuona watu wote wanaiamini dini ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu tajiriba ya kaumu zilizopita inaonesha kuwa watu wengi waliwakadhibisha Mitume na hawakuukubali wito waliowafikishia. Wajibu wangu na Mitume wengine wote wa Allah ni kufikisha wito wa Mola, na wala sina dhima yoyote katika kuukubali au kuukataa watu wito huo. Mimi nitapaswa kuwajibika kwa mas-ulia niliyonayo ambayo ni ya tablighi na kuwafikishia watu wito wa Allah. Lakini hata kama watu wote watakufuru na kuikana haki sitokuwa na dhima yoyote juu ya hilo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba Mitume hawakuwa wakiwalazimisha watu waiamini haki kwa nguvu kwa sababu walikuwa wakijua kwamba wajibu na jukumu lao wao ni kufikisha si kuteza nguvu na kulazimisha. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa waumini wasitarajie kwamba watu wote watamwamini Mwenyezi Mungu kama walivyo wao. Kama wao watatekeleza jukumu lao la tablighi na kufikisha ujumbe wa Uislamu kwa watu hawatokuwa na dhima wala mas-ulia yoyote kuhusiana na makafiri. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 705 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na atupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/