Sura ya Al-A'nkabut, 46-49 (712)
Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 46-49 (Darsa ya 712)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 712, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 46 ambayo inasema:
وَلا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلاَّ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلاَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ وَقُولُوا آمَنَّا بِالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْنَا وَأُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَهُنَا وَإِلَهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ
Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale walio dhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.
Katika aya zilizotangulia iliashiriwa namna ya kujadiliana na washirikina na makafiri wanaomkana Mwenyezi Mungu. Lakini aya hii tuliyosoma inazungumzia jinsi ya kujadiliana na Ahlul Kitab kama Wakristo na Wayahudi. Kwanza aya inazungumzia usuli na kanuni jumla kwa kusema: Katika mazungumzo na Ahlul Kitab wapeni heshima, na tumieni maneno na lugha ya murua na ya kirafiki. Zungumzeni kwa hoja na mantiki wala msitake kujikweza na kujifanya bora kuliko wao. Kwa njia hiyo ndipo maneno yenu yatawaathiri; na wale wanaotafuta na wenye kiu ya kuijua haki wataweza kuvutiwa na Uislamu. Tab'an kaida na kanuni hii haiwahusu wale ambao wanapozungumza na nyinyi hawatumii lugha ya heshima na adabu kama mnavyofanya nyinyi; na wala haipasi mwenendo na muamala wenu wa heshima mnaowafanyia watu wenye kiburi na ghururi uwe sababu ya kujidunisha nyinyi na kuwa dhalili mbele yao. Kisha aya inaendelea kwa kuashiria ulazima wa kuzingatia mambo yanayoziunganisha pamoja dini za mbinguni za tauhidi na kueleza kwamba: Badala ya kuanzia kwenye mambo mnayotafautiana jaribuni katika mazungumzo yenu muanzie kwenye nukta za umoja na za pamoja baina ya wafuasi wa dini za Mwenyezi Mungu ambazo ni kumwamini Yeye Allah na vitabu vya mbinguni alivyoteremsha. Waiteni Ahlul Kitab katika suala la nyote pamoja kumtii Mwenyezi Mungu na kusalimu amri kwa maamrisho yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba katika kuzungumza na wasio Waislamu haifai kutumia lugha ya matusi, kejeli na maneno machafu. Mazungumzo hayo inapasa yasimame juu ya msingi wa hoja na mantiki na kwa nia ya kujenga na kurekebisha. Ni wazi kwamba tunapozungumza na Waislamu wenzetu pia misingi hii yote tunapaswa kuizingatia. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuzungumza na kubadilishana mawazo kwa njia sahihi wafuasi wa dini za tauhidi, na kufanya hivyo katika masuala yanayoziunganisha pamoja ni jambo lililousiwa na Uislamu. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba kumwamini Allah na Mitume wake tu hakutoshi bali tunapaswa kuwatii na kusalimu amri mbele ya maamrisho yao.
Ifuatayo sasa ni aya ya 47 ambayo inasema:
وَكَذَلِكَ أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ فَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَمِنْ هَؤُلاء مَن يُؤْمِنُ بِهِ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلاَّ الْكَافِرُونَ
Na namna hivi tumekuteremshia Kitabu (cha Qur'ani). Basi wale tulio wapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur'ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakao iamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa makafiri.
Kama ambavyo Allah SW alimteremshia Nabii Musa Taurati na Nabii Isa Injili alimtuma Bwana Mtume Muhammad SAW pia na Kitabu cha Qur'ani; na asili ya vitabu vya Mitume wote ni maneno ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo hakuna mgongano baina yao; na kama ambavyo Waislamu wanaviamini vitabu vya Mitume waliotangulia inatarajiwa kwamba wafuasi wa dini nyinginezo nao pia wakiamini na kukiheshimu kitabu cha Qur'ani. Kwa sababu katika misingi mikuu, mafundisho yake yanawiyana na mafundisho ya vitabu vya Mitume waliotangulia. Kisha aya inaendelea kwa kueleza kwamba: si Ahlul Kitab peke yao bali hata washirikina na waabudu masanamu wenye kiu ya kujua ukweli nao pia wanaiamini Qur'ani na huamua kuufuata Uislamu. Ni wale makafiri wakaidi tu ambao haki wameitambua, lakini kwa sababu tofauti hawako tayari kuikubali, hao ndio wanaoikana na kuikadhibisha. Na hilo tab'an haliutii doa lolote ukweli wa Qur'ani. Ni sawa kabisa na mtu anayetia pazia la kitambaa kizito kwenye dirisha la chumba chake ili kuzuia mwangaza wa jua usiingie chumbani mwake humo. Kwa kufanya hivyo huwa halipunguzii chochote jua adhama yake, isipokuwa anajikosesha yeye mwenyewe tu nuru iangazayo ya mwangaza huo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba sambamba na Qur'ani kuviheshimu vitabu vya Mitume waliopita, inawalingania wafuasi wa dini nyingine kufuata Uislamu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa mtu huwa amejisalimisha kikweli kwa Mwenyezi Mungu kwa kutokuwa na taasubu na dini fulani tu; bali anapokuja Mtume anayefuatia humwamini yeye na Kitabu anachokuja nacho na si kung'ang'ania na kuwa na taasubi na dini ya Mtume aliyetangulia.
Darsa ya 712 ya Qur'ani inahatimishwa na aya ya 48 na 49 ambazo zinasema:
وَمَا كُنتَ تَتْلُو مِن قَبْلِهِ مِن كِتَابٍ وَلا تَخُطُّهُ بِيَمِينِكَ إِذًا لّارْتَابَ الْمُبْطِلُونَ
Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingeli kuwa hivyo wangeli fanya shaka wabatilifu.
بَلْ هُوَ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ فِي صُدُورِ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ وَمَا يَجْحَدُ بِآيَاتِنَا إِلاَّ الظَّالِمُونَ
Bali hii (Qur'ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya walio pewa ilimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipo kuwa wenye kudhulumu.
Mbali na aya za Qur'ani kukubaliana na vitabu vilivyotangulia vya mbinguni aya ya 48 inaashiria ishara nyingine ya ukweli wa kitabu hicho na kueleza kwamba: Kabla ya kuteremshwa Qur'ani, Bwana Mtume SAW hakuwahi kwenda kwa mwalimu yeyote, hakupelekwa kwenye chuo au madrasa yoyote wala hakusoma kitabu au maandiko yoyote yale ili wale wanaotaka kuukadhibisha wito wake wasije wakapata kisingizio cha kuzusha shaka na kusema: Hii Qur'ani imetokana na kutalii na kudurusu vitabu vilivyopita, na yeye anayedai kuwa amepewa Utume anasema uongo. Hii kwamba mtu ambaye hakusoma wala hajakwenda kwa mwalimu yeyote ameweza kuja na mafundisho adhimu ambayo hayakuwa na mfano wake kwa waarabu wa zama zile, na hata katika mambo mengi ameleta mafundisho ambayo yanakinzana na mila, desturi na utamaduni uliokuwa umezoeleka na kutawala katika zama zile, yenyewe ni moja ya hoja za kuthibitisha kuwa Qur'ani ni muujiza utokao kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo aya inamalizia kwa kusema: Ishara za ukweli wa Kitabu hiki zimejificha ndani ya aya zake; na wajuzi na wenye elimu wanalitamabua hilo; na wala hawazikani aya hizo ila watu wanaojidhulumu wenyewe nafsi zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya wakati, kwa irada ya Allah mtu ambaye hakusoma huubadilisha utamaduni na ustaarabu wa wanadamu; na si hasha watu waliosoma wanaokanusha umaanawi wa kidini huwa sababu ya kupotoka jamii za wanadamu. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa inapasa tuwe na hadhari tusije tukawapa maadui fursa ya kutumia jambo vibaya au kupata kisingizio cha kukadhibisha haki. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba wale ambao ni watu wa elimu na utambuzi kwa maana halisi wanauelewa barabara ndani ya nafsi zao ukweli wa Qur'ani. Wapenzi wasikilizaji, kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuoneshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuoneshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/