Jan 16, 2017 11:58 UTC

Sura ya Al-A'nkabut, aya ya 67-69 (Darsa ya 716)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 716, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 29 ya Al-A'nkabut. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 67 ambayo inasema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا جَعَلْنَا حَرَمًا آمِنًا وَيُتَخَطَّفُ النَّاسُ مِنْ حَوْلِهِمْ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَةِ اللَّهِ يَكْفُرُونَ

Je! Hawaoni kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wa pambizoni mwake wananyakuliwa? Je! Wanaamini batili na kuzikataa neema za Mwenyezi Mungu?

Katika zama ambapo unyang'anyi na uporaji yalikuwa mambo yaliyozagaa na kuzoeleka katika jamii za Waarabu huku watu wa kabila moja wakiwavamia na kuwashambulia watu wa kabila jingine na kuwaua baadhi yao na kuwakamata wengine mateka, Mwenyezi Mungu aliufanya mji wa Makka kuwa mji wa salama na amani ili wakaazi wake wawe watu wenye kuheshimika na ili mtu yeyote yule asithubutu kuushambulia mji huo. Kama ambavyo katika kadhia ya shambulio lililotaka kufanywa na jeshi lililojizatiti barabara la Abraha la askari waliopanda ndovu, ambapo kwa muujiza wa Allah kabla ya washambuliaji hao hawajaingia ndani ya mji wa Makka walishambuliwa na kuangamizwa na ndege waliotokea mbinguni. Kutokana na hayo, aya hii tuliyosoma inawahutubu washirikina wa Makka ya kwamba: Kwa kuzingatia kuwa Mwenyezi Mungu amekuneemesheni kwa neema hii kubwa na kuweza kuishi kwa amani na utulivu, kwa nini tena mnayaabudu masanamu; na badala ya Mwenyezi Mungu mnaielekea miungu hiyo bandia? Haya mnayoyafanya ni kitu kingine ghairi ya kukufuru neema za Mwenyezi Mungu? Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba amani ni moja ya neema za Allah; na njia sahihi ya kuishukuru ni kujiweka mbali na kila aina ya shirki na kufru. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kukumbusha neema za Mwenyezi Mungu kunaandaa mazingira mazuri ya kuwalingania na kuwaita watu katika ibada ya Mola mmoja tu wa haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 68 ambayo inasema:

وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَى عَلَى اللَّهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِالْحَقِّ لَمَّا جَاءَهُ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْكَافِرِينَ

Na ni nani dhaalimu zaidi kuliko yule amzuliaye uwongo Mwenyezi Mungu au akadhibishaye Haki inapo mjia? Je! Si katika Jahannamu ndio yatakuwa makaazi ya makafiri?

Katika utamaduni wa wanadamu, maana ya dhulma inaelezwa kupitia mahusiano ya kijamii; na kwa msingi huo, dhalimu huwa ni mtu anayewakosesha watu wengine haki zao. Lakini katika utamaduni wa dini, japokuwa aina hii ya dhulma imekemewa vikali pia lakini kuna aina nyingine ya dhulma iliyo muhimu zaidi ambayo ni chanzo cha aina nyingine nyingi za dhulma. Ikiwa mtu atalifanya sanamu au kitu kingine kuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu atakuwa amemfanyia dhulma Allah kwa sababu atakuwa amekiweka kitu katika nafasi sawa na ya Yeye Mola ilhali hakuna wa kulingana naye. Aidha mtu ambaye anawatuhumu Mitume wa Mwenyezi Mungu kuwa ni waongo na akawakadhibisha huwa amewafanyia dhulma watukufu hao, kwa sababu atakuwa amezipuuza jitihada zisizo na kifani walizofanya bila ya kuchoka kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye njia ya uongofu na atakuwa ameikufuru pia neema hiyo kubwa. Ni wazi kwamba ikiwa mtu atawafanyia dhulma watu wa kawaida atapata adhabu kali Siku ya Kiyama; kwa hivyo kama dhulma atakayotenda atakuwa amemfanyia Mwenyezi Mungu na Mitume wake adhabu yake itakuwa kali kabisa isiyo na mfano. Tab'an kuhusu shirki, inaweza ikadhihirika katika sura tofauti; kama kuabudu sanamu au katika sura nyingine mathalani kuabudu cheo, matamanio ya nafsi, pesa n.k. Kwa sababu hiyo waumini pia wako katika hatari ya kutumbukia kwenye lindi la aina hii ya shirki na kwa hivyo wanatakiwa wazivue nyoyo zao na wazisafishe nafsi zao na mapenzi ya vitu vinavyomfanya mtu awe mbali na Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba dhulma mbaya zaidi ni dhulma ya kiutamaduni, ambapo neno la haki hukanushwa na kukandamizwa; na neno la batili likaenezwa na kuzoeleka. Mtu dhalimu anayeikadhibisha haki bila ya shaka huwa hayuko tayari kuifuata. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kuongeza kitu kwenye dini na kuinasibisha na vifadhilishi na matashi ya nafsi zetu ni aina mojawapo ya kuingiza bid'a katika dini na kumzulia uongo Mwenyezi Mungu. Sisi tunapaswa kufuata mafundisho ya dini; na si kutaka dini ifuate fikra, matamanio na vifadhilishi vya nafsi zetu.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya 69 ambayo inasema:

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا وَإِنَّ اللَّهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ

Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, hakika tutawaongoza kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema. 

Aya hii ambayo ndiyo aya ya mwisho ya Suratul A'nkabut inaashiria maudhui ya Jihadi na kufanya jitihada na idili katika njia ya Mwenyezi Mungu, ambayo inajumuisha kupigana Jihadi na maadui na vilevile kufanya jitihada kubwa katika njia ya kueneza dini ya Allah. Katika utamaduni wa Kiislamu, Jihadi inajumuisha kupigana Jihadi na adui wa nje na kupigana Jihadi na adui wa ndani. Mtu muumini anatakiwa apambane na maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu na awe tayari kujitolea mhanga roho yake katika njia hiyo; kama ambavyo anapaswa pia kupambana na nafsi yake na matamanio haramu ya nafsi  ili asije akatekwa na hawaa na matamanio ya nafsi. Kinachotiliwa mkazo na aya hii ni kupigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili yake Yeye Mola. Kwani si hasha watu wakawa wanapigana na maadui wa dini lakini lengo lao likawa ni kujitafutia umaarufu au kunufaika na baadhi ya fursa za kidunia na ngawira za vita. Kwa sababu hiyo lililo muhimu zaidi ya Jihadi na juhudi katika njia ya dini ni kuwa na ikhlasi katika ufanyaji mambo; kwani kama mtu hatokuwa na ikhlasi, kujitoa mhanga roho yake vitani hakutokuwa na thamani yoyote bali kutakuwa sababu ya kuhasirika na kupata hasara Siku ya Kiyama. Ikiwa mtu atapigana Jihadi na kufanya jitihada katika njia ya Allah, kwa mujibu wa aya hii Yeye Mola ameahidi kumwongoza mja huyo kwenye njia ya uongofu na pia kumpa auni na msaada wake. Ni wazi kuwa katika safari ya kuelekea kule mtu alikokusudia, njiani kunaweza kujitokeza vizuizi na matatizo chungu nzima kiasi kwamba baadhi ya wakati humwiya vigumu mtu kujua njia za kuvikabili na kuvivuka vizuizi na matatizo hayo. Kwa sababu hiyo Allah SW anamuahidi mja wake kuwa katika hali na mazingira hayo magumu, mimi nitakusaidia kukuwezesha kujua njia sahihi ya kupita na kuyashinda matatizo utakayokabiliana nayo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba mbali na mwongozo anaotoa Allah kwa watu wote kwa ajili ya kuufikia uongofu, kuna mwongozo makhsusi wa uongofu anaowapa waja wanaofanya jitihada katika njia yake kwa ikhlasi. Tab'an yeye mja mwenyewe ndiye anayepaswa kupiga hatua ya kwanza ili kuipata taufiki hiyo. Funzo jingine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa kama tutaanza kufanya mambo kwa ikhlasi, Mwenyezi Mungu atatuongoza kuweza kufikia mafanikio na wala hatutoacha mkono. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba ikiwa mtu ataanza kupiga hatua katika njia ya Allah na kuelekeza bidii na jitihada zake zote katika njia hiyo Yeye Mola atampa auni na msaada wake hadi kufikia lengo lake. Wapenzi wasikilizaji darsa ya 716 ya Qur'ani imefikia tamati; na ndiyo inayotuhatimishia tarjumi na maelezo ya sura ya 29 ya Al A'nkabut. Tunamwomba Allah atujaalie kuwa wenye kuyatekeleza yale tuliyojifunza katika sura hii. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags