Maadhimisho ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu (6)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio makala maalumu yanayokujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, hii ikiwa ni sehemu ya sita ya mkala hizo.
Ndugu wasikilizaji ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, uliandaa mazingira ya ushiriki wa kila upande wa wananchi katika maamuzi mbalimbali yanayoihusu nchi yao. Pamoja na kwamba katika mwaka wa mwisho wa utawala wa Shah, wananchi walilazimishwa mfumo wa utawala wa chama kimoja, pamoja na hayo katika uchaguzi uliokuwa ukifanyika nchini hapa walikuwa wakitengwa mbali na demokrasia ya uchaguzi wa kweli.
Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu ilikuwa nukta ya mwanzo wa mabadiliko ya kidemokrasia nchini Iran ambapo yaliweza kuhusisha sekta mnalimbali kama vile za kijamii, kiuchumi na kwa misingi ya katiba. Misingi hiyo ilihusu masuala ya haki za taifa la Iran, haki ya kujitawala na kujiainishia mustakbali, kuchagua mihimili tofauti ya utawala, uhuru wa vyombo vya habari, usawa wa haki za kitaifa, usawa mbele ya sheria, uhuru wa vyama vya siasa na mambo mengine kama hayo ambayo yanawajumuisha raia wote wa taifa hili katika kustawisha demokrasia ya kidini nchini. Ni kwa kutegemea misingi hiyo, ndio maana tangu mwanzo kulipojiri mapinduzi ya Kiislamu, raia wa nchi hii wakawa wanashiriki kwa wingi katika chaguzi mbalimbali hapa nchini. Hata hivyo isisahaulike kuwa, baada ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara ya kwanza wananchi walishirikishwa katika kura ya maoni juu ya uainishwaji wa katiba, hapo tarehe 12 Farvardin mwaka 1358, sawa na tarehe Mosi April 1979 Miladia, ambapo asilimia 98.2 ya wananchi waliupigia kura ya ndio mfumo wa Kiislamu. Wito uliotolewa wa 'kesho tokeni nje ya nyumba zenu na mpige kura, lakini kwa uhuru na kuchagua mfumo mnaoutaka,' ilikuwa ni harakati ya kidemokrasia ya wananchi kupitia pendekezo la Imam Ruhullah Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, harakati ambayo iliidhihirishia dunia kwamba wananchi ndio waamuzi wa thamani za Mapinduzi ya Kiislamu nchini kupitia upigajikura wao. Kwa utaratibu huo tangu awali muundo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukawa umejengeka juu ya msingi wa katiba ambapo wananchi walishirikishwa moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika uchaguzi wa mihimili yote ya utawala. Mfumo huo unajumuisha pia uchaguzi wa Kiongozi Muadhamu katika nafasi ya Walii Mtawala, ambapo naye huchaguliwa na wawakilishi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao nao huchaguliwa na wananchi.
Ndugu wasikilizaji ni vyema mfahamu kwamba, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umejengeka juu ya misingi mikuu miwili ya Jamhuri na Uislamu. Kwa mtazamo wa mfumo wa kidemokrasia, jamhuri ina maana ya utawala unaotokana na wananchi. Kuhusiana na suala hilo, Omar Alaysapahych, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa nchini Bosnia anasema: "Tunapotazama kwa ufupi historia za kipindi cha mwisho wa karne za kati yaani karne ya 13 Miladia na kuendelea, na mwanzo wa kudhihiri ulimwengu wa leo, tunaona kuwa zilizama katika lindi la migogoro na hali mbaya inayofanana na ile tunayoishuhudia katika ulimwengu wa leo. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakiwa ni tukio ambalo linafungamana na nara, malengo, nguvu na kiongozi aliye na utambuzi sahihi wa mambo, ni mapinduzi ya kidini. Kwa hakika Iran ni mfano bora wa mapinduzi ya kidini yanayotegemea uamuzi wa wananchi." Mwisho wa kunukuu. Aidha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeandikwa kwa kutegemea mfumo wa kiuchaguzi na kibunge, mfumo wa mabaraza na uhuru wa kiraia na kisiasa. Kifungu cha kwanza cha katiba kinasema: "Aina ya serikali nchini Iran ni Jamhuri ya Kiislamu," na hii ina maana ya mfumo wa serikali ya Jamhuri na Uislamu yaani misingi miwili ambayo kwanza ni thamani za dini na pili ni uchaguzi wa wananchi. Mfumo huu wa demokrasia unatekelezwa hapa nchini kama sehemu ya haki za kiraia na kisiasa za wananchi. Hii ni kusema kuwa katika kipindi chote cha miaka 38 ya Mapinduzi ya Kiislamu, karibu kila mwaka wananchi hushiriki kwa uchache katika uchaguzi mmoja, suala ambalo linaonyesha kwamba raia wa taifa hili ndio marejeo ya serikali, kupitia ustawi wa kisiasa na utawala bora wa demokrasia ya wananchi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Kuhusiana na suala hilo, Ahmed Hatit, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa nchini Lebanon anasema: "Tawala za kidemokrasia za wananchi katika kipindi cha karne za hivi karibuni, ni tawala ambazo kimsingi utendajikazi wake unatokana na matakwa ya wananchi, Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu imeunda mfumo mpya wa demokrasia ya wananchi ambao asili na dhati yake inatokana tu na matakwa na irada ya wananchi….Baada ya Mapinduzi, Imamu Khomein aliandaa kura ya maoni mfumo ambao hukaririwa kila mara nchini Iran ambapo wananchi hupewa nafasi ya kuweza kuwachagua viongozi wao. Hali hiyo inajiri katika hali ambayo katika aghlabu ya nchi nyingi za eneo la Mashariki ya Kati chaguzi huwa hazifanyiki na wala wanawake hawapewi nafasi yoyote ya kujieleza au kushiriki kwenye chaguzi. Mwishoni wa kunukuu. Takwimu zinaonyesha kwamba hali ya kisiasa nchini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni bora zaidi kuliko nchi nyingi hasa kuhusiana na idadi ya chaguzi zinazofanyika na vilevile ushiriki mkubwa wa wananchi katika chaguzi hizo, ikilinganishwa na nchi nyingi za dunia. Aidha hali hiyo ya demokrasia nchini Iran ni bora zaidi ikilinganishwa na nchi zote za Mashariki ya Kati huku ikiwa sawa na mataifa mengi ya Kimagharibi katika uwanja huo. Hii ni katika hali ambayo licha ya nchi nyingi kupiga hatua katika harakati za demokrasia, lakini hii leo karibu theluthi moja ya nchi nchi hizo zimeshindwa kabisa kuwapatia raia wao haki ya kuainisha mustakbali wao. Aidha ushiriki wa wananchi katika chaguzi, nao bado unakabiliwa na mdororo mkubwa. Kuhusiana na suala hilo, Erica Bobrow mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Moja ya vipimo vya demokrasia katika jamii nyingi ni chaguzi. Kwa kipindi cha miongo kadhaa iliyopita, kiwango cha ushiriki wa wananchi katika chaguzi duniani kimepungua sana suala ambalo kwa hakika limezua wasi wasi kwa tawala na asasi za kusimamia chaguzi. Hivi sasa nchi nyingi zinafanya juhudi kubwa za kuwafanya wananchi waweze kushiriki katika chaguzi hizo. Suala hilo linashuhudiwa zaidi katika nchi zinadai kuwa zimeendelea ambapo sasa zimeamua kuwapiga faini watu anaokwepa kushiriki katika uchaguzi. Katika hilo Bi, Erica anazitaja nchi kama vile Ubelgiji, Australia, Bolivia na Misri, ambazo sasa zinawatoza faini raia ambao wanakataa kushiriki katika zoezi hilo au kuwanyima baadhi ya haki za kijamii." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo faini hizo na matangazo mengi yanayofanywa na vyombo mbambali vya habari katika nchi za Magharibi zinazodai kupiga hatua kubwa katika demokrasia, bado hazijaweza kufanikiwa katika kuwafanya wananchi waweze kushiriki kwa wingi katika chaguzi ambapo karibu kila siku tunashuhudia ongezeko kubwa la mdodoro katika uwanja huo. Kwa mfano tu, katika chaguzi za rais nchini Marekani zilizofanyika katika karne za hivi karibuni, ushiriki wa wananchi umekuwa chini ya asilimia 50 katika hali ambayo Marekani hiyohiyo imekuwa ikijinadi kuwa imepiga hatua na mbeba bendera halisi wa demokrasia duniani.
Huku hali ikiwa hivyo katika nchi za Magharibi, nayo mataifa ya eneo la Ghuba ya Uajemi na ambayo tawala zake ni marafiki wakubwa wa Magharibi, nazo zimefeli kwa kiasi kikubwa katika suala zima la demokrasia ambapo tawala hizo zinaongozwa kwa mfumo wa kurithishana madaraka sambamba na kuwanyima raia haki ya kuchagua viongozi wanaowataka. Nchini Saudia tangu miaka 100 iliyopita utawala unaoongoza nchi hiyo ni wa kifalme tu. Hata hivyo miaka michache iliyopita watawala wa nchi hiyo waliasisi baraza la ushauri ambalo kimsingi nalo halina uwezo wowote wa kuchukua maamuzi na kinyume chake linaweza tu kumshauri mfalme katika maamuzi yake. Aidha nusu ya wajumbe wa baraza hilo hawachaguliwi na wananchi bali wanateuliwa na mfalme mwenyewe wa Saudia. Kuhusiana na suala hilo gazeti la al-Akhbar linaandika: "Kutokana na raia wa Saudia kuishi chini ya makucha ya utawala wa karne za kati wa Aal-Saud, wamekosa hata haki ndogo kabisa ya kushiriki chaguzi kwa ajili ya kuwapigia kura viongozi na wakuu wao wanaowataka. Nchini Saudia si serikali kuu, bunge wala katiba iliyobuniwa kwa uungwa mkono wa wananchi kama ambavyo wananchi pia wananyimwa haki ya kuwachagua viongozi wao. Na kwa ajili hiyo tunaweza kuuta utawala wa Saudia kuwa ni utawala usio na ridhaa ya wananchi, wala wa kidemokrasia bali ni utawala wa kidikteta. Ni utawala ambao hata wanawake wamenyimwa haki ya kuendesha magari ambapo inapotokea mwanamke akakamatwa akiwa anaendesha chombo cha usafiri basi huadhibiwa bila huruma." Mwisho wa kunukuu. Hata katika nchi jirani na Saudia ambayo nayo inaongozwa na utawala wa kiukoo, yaani Bahrain, kiwango cha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi wa bunge wa hivi karibuni, hakikuvuka asilimia 18. Hii ni katika hali ambayo utawala wa nchi hiyo ulikuwa umetangaza kutekeleza adhabu mbalimbali ikiwemo ya kuwanyima huduma za kijamii watu ambao wangesusia uchaguzi huo. Hali ikiwa hivyo nchini Bahrain, nchi nyingine za eneo la Ghuba ya Uajemi nazo zinakabiliwa na hali hiyo hiyo ya mdodoro wa ushiriki wa wananci kwenye chaguzi, suala ambalo linawanyima usingizi watawama wa nchi hizo.
Uchaguzi nchini Iran unazingatia sheria zote zilizoainishwa kutokana na misingi ya kisiasa huku ukiwa na baraka zote za wananchi. Ni kwa kuzingatia umuhimu wa kuhudhuria wananchi katika chaguzi za kuwachagua viongozi wao nchini, ndipo katiba ikaandaa mzingira mazuri ya kushirikishwa kikamilifu wananchi katika uwanja huo. Kwa hakika ushiriki wa wananchi kwa ajili ya kuainisha mustakbali wa taifa lao kupitia njia ya chaguzi zinazozingatia misingi ya demokrasia, ni jambo ambalo limepewa umuhimu mkubwa na siasa za Mapinduzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Aidha katiba ya taifa hili imefunga njia zote zinazoweza kutoa mwanya wa kutokea udikteta nchini. Kwa mfano tu, lengo la kutotoa madaraka zaidi kwa upande mmoja, ni kugawa kwa usawa mihimili mitatu ya dola, ambapo matokeo yake ni kuwapa raia haki ya kushiriki katika kuwachagua viongozi wa mihimili hiyo. Kwa ajili hiyo wananchi sambamba na kushiriki kwa njia ya uhuru katika chaguzi, huweza kuwachagua watu wenye sifa stahiki na kushikilia nafasi maalumu serikalini. Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ‘uchaguzi ni dhihirisho kubwa la uwezo wa kitaifa.’ Mwisho wa kunukuu.
Ndugu wasikilizaji sehemu ya 6 ya makala haya inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu.