Jumatano, 8 Februari, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 10 Jamadil Awwal 1438 Hijria sawa na Februari 8, 2017.
Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, vibaraka wa gadi ya mfalme Shah wa Iran, walivamia moja ya kambi za kikosi cha Jeshi la Anga mjini Tehran majira ya usiku, baada ya kundi la makamanda wa jeshi hilo kutangaza uungaji mkono wao kwa Mapinduzi ya Kiislamu na utiifu wao kwa Imam Ruhullah Khomeini. Baada ya kutangazwa habari hiyo, wananchi Waislamu wa Iran kutoka pembe zote za mji wa Tehran walielekea katika kambi ya kikosi cha Jeshi la Anga ili kuwasadia wanajeshi hao ambao walikuwa wakipambana na vibaraka hao wa mfalme Shah. Licha ya kutokuwa na silaha za maana wananchi hao walifanikiwa kuzima shambulio la mamluki hao na kwa utaratibu huo, hatua ya mwisho ya kuuangusha utawala wa Shah nchini Iran ikawa imeanza.
Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni iliyopewa jina la Walfajr 8 kwa kushambulia ngome za jeshi la utawala wa zamani wa Iraq katika eneo la kusini zaidi la mpaka wa nchi mbili hizi. Maelfu ya wapiganaji wa Iran walivuka Mto Arvand na kufanikiwa kuuteka mji wa Faw unaopatikana kusini mashariki mwa Iraq, katika siku ya kwanza ya operesheni hiyo. Operesheni hiyo ilikuwa ya ghafla na tata kwa upande wa kijeshi na iliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi na kisiasa ulimwenguni na utawala wa zamani wa Iraq. Operesheni ya Walfajr-8 ilitekelezwa kwa lengo la kuushinikiza utawala wa Saddam uache kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran na kuilipa fidia Tehran kutokana na hasara na maafa yaliyosababishwa na uvamizi wa Iraq.

Tarehe 8 Februari miaka 54 iliyopita Kanali Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa kijeshi wa Chama cha Baath. Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.