Apr 27, 2017 02:38 UTC
  • Alkhamisi 27 Aprili, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Rajab 1438 Hijria sawa na 27 Aprili, 2017.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita alifariki dunia Kwame Nkrumah, mwanasiasa mashuhuri wa Kiafrika na mwasisi wa uhuru wa Ghana. Mkrumah alizaliwa mwaka 1909 na baada ya kupata shahada ya uzamivu nchini Marekani alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa. Baadaye Kwame Nkrumah aliasisi chama cha Kitaifa cha Watu wa Ghana na kuanza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Mwaka 1951 alishiriki katika uchaguzi wa Bunge na kuwa Waziri Mkuu. Baada ya Ghana kupata uhuru mwaka 1960 Kwame Nkrumah alikuwa Rais wa nchi hiyo lakini Februari 24 mwaka 1966 aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na wafuasi wa nchi za Magharibi akiwa safari nchini Uchina. Baadaye alielekea Guinea ambako aliishi hadi kufariki dunia. Kwame Nkrumah anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamapambano mashuhuri wa Afrika waliofanya jitihada kubwa katika kupata uhuru na kujitawala nchi za bara hilo.

Miaka 56 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Sierra Leone moja ya makoloni makongwe ya Uingereza magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Sierra Leone ilianza kukoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 na nchi hiyo ilikuwa mojawapo ya vituo muhimu vya kuuzia watumwa waliokuwa wakipelekwa Ulaya. Uingereza ilianza kuikoloni Sierra Leone mwishoni mwa karne ya 18 hadi mwaka 1961 wakati nchi hiyo ilipopata uhuru. Baada ya uhuru, nchi hiyo ilikumbwa na mapinduzi na uasi mwingi. Kijiografia  Sierra Leone iko magharibi mwa Afrika ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 71,000 na inapakana na Guinea na Liberia. 

Bendera ya Sierra Leone

Miaka 57 iliyopita katika siku inayofanana na hii ya leo, nchi nyingine inayopatikana huko katika pwani ya magharibi mwa Afrika kwa jina la Togo ilipata uhuru. Wareno walikuwa watu wa kwanza kuikoloni Togo na nchi hiyo ilijulikana sana kwa jina la "Pwani ya Watumwa"  kwa kuwa nchi za Ulaya  zilikuwa zikiitumia nchi  hiyo kama kituo cha kusafirishia watumwa kuelekea Ulaya. Togo inapakana na nchi za Ghana na Benin na mji mkuu wake ni Lome.

Ramani ya nchi ya Togo

Tarehe kama ya leo miaka 496 iliyopita, Ferdinand Magellan, baharia wa Kireno aliuawa na wenyeji wa Ufilipino kutokana na kuingilia mambo yao. Alizaliwa mwaka 1470 na kuanzia mwaka 1519 Miladia baharia huyo alianza safari yake kubwa ya baharini akiwa na meli tano. Ferdinand Magellan aligundua lango bahari huko kusini mwa bara la Amerika baada ya kuwasili katika pwani ya Amerika ya Latini. Lango bahari hilo limepewa jina la baharia huyo wa Kireno yaani Lango Bahari la Magellan.

Ferdinand Magellan

Na Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Jenerali Abdul Qadir alifanya mapinduzi nchini Afghanistan na baada ya kumuua Daud Khan Rais wa wakati huo wa nchi hiyo, alimuweka madarakani Noor Muhammad Taraki kiongozi wa Chama cha Kidemokrasia cha Khalq. Baada ya muda Hafizullah Amin alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Muhammad Taraki na yeye kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Hata hivyo mlolongo huo wa mapinduzi uliendelea kwani Hafidhullah Amin alipinduliwa na kisha kuuawa na Babrak Karmal. Katika kipindi cha uongozi wa Babrak, ndipo Afghanistan ilipovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Shirikisho la Umoja wa Sovieti.

enerali Abdul Qadir

Siku kama ya leo, miaka 1162 iliyopita, alifariki dunia Abdullah bin Muslim Dinuri, maarufu kwa jina la Ibn Qutaybah akiwa na umri wa miaka 63. Ibn Qutayba alizaliwa mjini Kufah, Iraq na kushika hatamu za ukadhi huko mjini Dinuri, magharibi mwa Iran. Alitabahari katika Qur’ani, Hadithi, mashairi na fasihi. Alimu huyo aliandiandika vitabu mbalimbali katika elimu za Kiislamu maarufu zaidi vikiwa ni pamoja na “Ta’awiilu Mushkili-Qur’ani”, “Tafsiru Ghariibul-Qur’an”, “Uyunul-Akhbaar”, “Maani ash-Shi’ir” na “Gharibul- Hadith.”

Ibn Qutayba

 

Tags