Ijumaa, Mei 12, 2017
Leo ni Ijumaa, tarehe 15 Shaaban mwaka 1438 Hijria, sawa na Mei 12 mwaka 2017 Miladia.
Siku ya leo yaani tarehe 15 Shaaban mwaka 255 Hijria, Imam Mahdi AS alizaliwa mjini Samarra kaskazini mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq. Baba yake ni Imam Hassan Askari AS. Imam Mahdi ni mjukumuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW kupitia kizazi cha masharifu na masayyid cha binti mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad yaani Bibi Fatimatu Zahra SA. Mama yake alikuwa bibi mwenye heshima kubwa aliyejulikana kwa jina la Nargis. Imam Mahdi AS ni nyota ya 12 ya Maimamu wa Ahlul Bayt AS waliousiwa na Bwana Mtume Muhammad SAW. Mahdi, Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake, ni wa mwisho kati ya Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume Muhammad (SAW) na kwa mujibu wa hadithi zilizopokewa kutoka kwa babu yake, yaani Bwana Mtume, atakuja kuijaza dunia haki na uadilifu baada ya kujazwa dhulma na uonevu. Radio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuadhimishwa siku hii tukufu ya kuzaliwa Imam Mahdi AS.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 278 na hivyo likawa limekubaliana na ombi la wananchi wa Bahrain la kutaka kutumwa nchini humo, mjumbe wa Umoja wa Mataifa.
Mjumbe huyo alisalia nchini Bahrain kwa muda wa wiki mbili na kukutana na viongozi wa kisiasa na kikabila waliokuwa na ushawishi nchini humo. Natija ya mazungumzo hayo ikawa ni Bahrain kutangaza uhuru wake.
Miaka 9 iliyopita, katika siku kama ya leo, tetemeko kubwa la ardhi lenye uzito wa 7.9 katika kipimo cha rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha, watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Aidha tukio hilo la kutisha liliwaacha mamilioni ya watu bila makazi. Zilzala hiyo inahesabiwa kuwa moja ya mitetemeko mikubwa ya ardhi iliyowahi kuikumba China.
Na miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, yaani tarehe 22, Ordibehesht, mwaka 1364 Hijria Qamaria, makumi ya watu walikufa shahidi na kujeruhiwa kutokana na shambulizi a bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la Munafiqiin (MKO) mjini Tehran. Mripuko huo mbali na kusababisha uharibifu mkubwa, uliteketeza kikamilifu jengo moja la orofa mbili na karakana ya ufumaji nguo katika barabara ya Naser Khosro na kuua watu 9 na kujeruhi wengine 45. Katika hujuma hiyo ya kigaidi, magaidi wa MKO walitumia bomu lililokuwa na mada za milipuko za TNT zilizokuwa na uzito wa pauni 50. Kundi hilo la kigaidi limekuwa likifanya mashambulizi ya aina hii hapa nchini kwa shabaha ya kupiga vita Mfumo wa Kiislamu na kudhoofisha usalama wa taifa. Mauaji hayo ya kinyama kwa mara nyingine tena yaliidhihirishia dunia jinai za kutisha za kundi la kigaidi la MKO, lenye kuungwa mkono na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni.