Jun 14, 2017 03:09 UTC
  • Jumatano 14 Juni, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 19 Ramadhani 1438 Hijiria sawa na tarehe 14 Juni 2017.

Miaka 1398 iliyopita, inayosadifiana na siku kama ya leo Imam Ali bin Abi Talib AS ambaye ni mkwe, binamu na shakhsia wa karibu kwa Mtume Mtukufu SAW alipigwa upanga wa sumu na kujeruhiwa vibaya akiswali Sala ya alfajiri katika Msikiti wa Kufa nchini Iraq. Imam Ali A.S alikufa shahidi baada ya siku 3 kutokana na jeraha hilo. Ali bin Abi Talib ni shakhsia wa pili mkubwa baada ya Mtume Muhammad SAW ambaye anaelezwa na historia ya Uislamu kuwa alikuwa shujaa, mwenye imani, akhlaki njema, elimu na mwadilifu. Alipata elimu na mafunzo kwa Mtume Mtukufu SAW na alikuwa mwanamume wa kwanza kuukubali Uislamu. Katika vipindi tofauti daima Imam Ali AS alikuwa msaidizi wa karibu wa Mtume SAW katika hali zote za shida na matatizo na alihatarisha hata maisha yake kwa ajili ya kumlinda Mtume Mtukufu na dini ya Uislamu. Licha ya kuwa shujaa na mpiganaji shupavu, Imam Ali AS alikuwa mpole na mwenye upendo. Alipenda haki na uadilifu na kupambana ipasavyo na dhulma katika kila njanya.

Siku kama ya leo miaka 281 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika nyanja za umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea pia kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina Lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

Charles Augustin de Coulomb

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi Sudani mwaka 1881 walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na hivyo kulikomboa eneo hilo.

Ramani ya Sudan

Siku kama ya leo miaka 187 iliyopita, wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili, kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za walio wengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, alifariki dunia Jorge Luis Borges, mwandishi mkubwa wa Amerika ya Latini. Luis alizaliwa mwaka 1899 Miladia nchini Argentina na kutokana na kutalii sana athari za wasomi wakubwa kama vile Edgar Allan Poe, Charles Dickens na Cervantes akafanikiwa kuinukia na kuwa hodari katika uwanja huo. Mwishoni mwa masomo yake, Jorge Luis Borges akaanza shughuli ya uandishi na taratibu akaanza kuandika kisa mashuhuri cha Amerika ya Latini. Hata hivyo kutokana na upofu wake, hakuweza kumaliza kuandika kisa hicho. Luis ameacha athari mbalimbali za vitabu ambavyo vinapatikana katika maktaba mbalimbali za dunia.

Jorge Luis Borges

Na tarehe 24 Khordad miaka 36 iliyopita wawakilishi 120 wa Majlisi ya Ushaudi ya Kiislamu ya Iran (Bunge) waliwasilisha muswada wa kutokuwa na imani na Bani Sadr aliyekwua rais wa wakati huo wa Iran. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kusambaratika mapambano ya wananchi dhidi ya wavamizi wa chama cha Baath kutoka Iraq katika hujuma iliyofanywa katika ardhi ya Iran kutokana na kukosa misaada ya dharura kutoka kwa Bani Sadr aliyekuwa Kamanda na Amri jeshi Mkuu, na vilevile hitilafu zilizojitokeza baina ya Rais wa nchi na mihimili mingine miwili ya dola.

Bani Sadr