Mar 15, 2016 10:28 UTC
  • Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (21)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea sehemu ya 21 ya kipindi cha Ufeministi, Itikadi na Misingi Yake. Kizazi cha sasa ambacho kimeathiriwa na fikra za kifeministi kinakimbia na kukwepa majukumu ya kifamilia na hakina hamu ya kuoa au kuolewa na kuanzisha familia.

Katika upande mwingine tunashuhudia kupanda juu kwa kiwango cha talaka na kusambaratika familia hususan katika jamii za Magharibi. Kipindi chetu leo kitazungumzia taathira za mitazamo ya kifeministi katika kuzidisha talaka katika jamii za Magharibi na mtazamo wa Uislamu kuhusu talaka.

Talaka (Divorce) katika lugha ina maana ya mwanamke kuachana na mwanaume na kufungua pingu za ndoa na nikahi. Katika istilahi talaka katika mfumo wa sheria katika nchi za Magharibi humaanisha kusambaratika uhusiano wa ndoa rasmi na ya kisheria katika kipindi cha uhai wa mwanamke na mwanaume, na baada ya kutokea kwake kila mmoja wao anaweza kuoa au kuolewa tena.

Hapana shaka kuwa familia ni moja kati ya nguzo muhimu za kulinda na kulea mwanadamu. Sababu kubwa zaidi ya kusambaratika taasisi hiyo muhimu ni talaka na kuachana mume na mke. Japokuwa talaka ilikuwepo tangu mwanzoni mwa maisha ya kijamii ya mwanadamu na kwa mujibu wa nyaraka za kisheria za kale, ilikuwa na sura ya kisheria tangu hapo awali, lakini kiwango cha talaka katika kila zama kimekuwa katika hali inayokubalika na wala hakikuwa na madhara yasiyoweza kufidika kama ilivyo hivi sasa. Hii leo tunashuhudia ongezeko kubwa la talaka katika jamii kwa kadiri kwamba, kuna wasiwasi wa kusambaratika taasisi ya familia. Vilevile taathira za jambo hilo limezidisha ufuska wa kijamii, matatizo ya kiakili na aina mbalimbali ya maradhi ya kinafsi.

Wataalamu wa masuala ya familia wanasema kuwa, moja kati ya sababu za kuongezeka talaka ni wimbi la utamaduni wa ufeministi katika nchi za Magharibi. Juhudi za kupasisha haki na majukumu sawa na ya wanaume ya kiuchumi kwa ajili ya wanawake, kudunisha na kutothamini kazi za mwanamke ndani ya nyumba na familia, kubadilika kikamilifu nafasi za mwanaume na mwanamke ndani ya familia na jamii kwa kisingizio cha kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake, kudhoofishwa au hata kutokomezwa familia baada ya kuitambua kuwa ndiyo kituo na chanzo kikuu cha dhulma na ukandamizaji dhidi ya mwanamke, kuanzisha na kutunga sheria na miundo ya kijamii ya kurahisisha suala la mwanamke kuingia katika jamii katika hali sawa na ile ya wanaume, utumiaji wa wenzo wa mashinikizo, sheria na uchumi kwa ajili ya kumlazimisha mwanamke kuingia katika jamii kutafuta kipato na ajira na kadhalika, vimetoa changamoto kubwa kwa suala la kuanzisha au kudumisha maisha ya familia. Kwa mfano tu, mitazamo ya kifeministi hususan katika maudhui ya uchumi wa wanawake, imewafanya wanawake wengi ama wasiolewe kabisa au wanapoolewa mahitaji yao kama mwanamke yasikidhiwe kutokana na masuala ya kiajira na kikazi. Kwa msingi huo, suala hilo limekuwa sababu ya wanawake wengi kutalikiwa muda mfupi tu baada ya kuolewa na kujiunga na mamilioni ya wanawake wanaosimamia familia zao wenyewe katika jamii za Magharibi baada ya kupoteza haki za kifedha na kiroho wanazopaswa kuwa nazo katika muundo wa familia.

Katika dunia ya sasa wanaume wengi wanaoa kwa kuchelewa na wanaamini kuwa wana majukumu machache sana mkabala wa familia na wake zao. Kwa maneno mengine ni kuwa, wanaume wengi wa zama hizi wanataka mke mwenye uwezo wa kujikimu kimaisha, wanafadhilisha familia ndogo na pale ambapo hawaridhishwi na aina ya maisha ya ndoa hukimbilia talaka kwa urahisi na wepesi. Wakati huo huo mabadiliko yaliyofanywa katika sheria za talaka yamerahisisha sana mchakato wa kisheria wa mwanaume na mwanamke kuachana na kutalikiana kirahisi na kudhoofisha misingi ya kimantiki ya udharura wa mwanaume kudhamini mahitaji ya kimaisha ya mke na familia yake. Vilevile mafeministi wamehamasisha sana suala hilo.

Hata hivyo inatupasa kuweka wazi kuwa, wakati mafeministi wanaendelea kuwahamasisha wanawake kutalikiana na waume zao na kuchukua jukumu la kulea watoto wao wenyewe na wanazishinikiza serikali kubuni sheria katika uwanja huo, ushahidi unaonesha kuwa, katika upande wa uchumi, wanawake waliotalikiwa na watoto wao, wanaishi katika hali ngumu sana na wengi miongoni mwao wanasumbuliwa na taathira za kiuchumi zinazosababishwa na kusambaratika ndoa zao. Wanawake hao si tu kwamba wanastahamili tabu na mashaka ya moja kwa moja ya talaka, bali pia hubeba majukumu mazito na gharama kubwa za kulea watoto wa talaka. >

Katika dini ya Uislamu mfungamano wa ndoa ni mfungamano mtakatifu na dharura sana kwa ajili ya utulivu wa kimwili na kiroho. Aya nyingi za Qur’ani Tukufu zimewaamuru Waislamu kuoa na kuolewa na Mtume Muhammad (saw) amelisisitiza sana suala hilo. Mtukufu huyo anawatahadharisha sana Waislamu wasiache kuoa kwa kuogopa umaskini na ukata.

Kama ambavyo dini ya Uislamu imesisitiza sana ndoa na kuitambua kuwa ni mfungamano mtakatifu, vivyo hivyo imeitambua talaka kuwa ni jambo baya na lisilopendeza. Dini ya Uislamu imeenda mbali zaidi na kuitambua talaka kuwa ni jambo linalomchukiza sana Mola Muumba. Imenukuliwa kwamba, Mtume (saw) amesema: Talaka ndiyo halali inayochukiwa zaidi na Mwenyezi Mungu. Mjukuu wake, yaani Imam Ja’far Swadiq (as) amesema; “Katika dini ya Uislamu hakuna kitu kinachomchukiza na kumuudhi zaidi Mwenyezi Mungu kuliko nyumba inayoharibiwa kwa sababu ya talaka. Mwenyezi Mungu huwachukia watu wanaotalikiana na talaka hutetemesha arshi na kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu”.

Inapasa kueleweka kuwa, tofauti na mikataba mingine ya kijamii, hamu ya mwanadamu ya kutaka kuoa au kuolewa ni jambo la kimaumbile na la dhati linalopatikana kutokana na haja ya mahaba, mfungamano, ushirikiano na kujitolea kwa mwanamke na mwanaume wanaotaka kuishi pamoja.

Muundo wa kimaumbile wa ndoa ambao ulitegemewa na Uislamu katika kutunga sheria zake ni kwamba mwanamke katika muundo wa familia ni kipenzi, mahabubu na kito cha kuheshimiwa. Kwa msingi huo iwapo -kwa sababu moja au nyingine- mke atapoteza nafasi hiyo kwa mumewe na taa ya mahaba na mapenzi ikafifia na kuzima katika nafsi ya mume, msingi na nguzo muhimu ya familia itakuwa imeharibika. Uislamu unasikitishwa sana na mazingira kama haya lakini baada ya kuona kuwa msingi wa familia husika yaani mahaba, upendo na heshima baina ya wanandoa wawili vimesambaratika na kutoweka, hauwezi tena kuwalazimisha kuendelea kuishi katika hali kama hiyo. Hapa ndipo ikaruhusiwa talaka lakini kama jambo lisilopendwa bali linalomchukiza Mwenyezi Mungu. Hata hivyo Uislamu umefanya jitihada kubwa na kuweka taratibu maalumu za kunusuru familia na kulinda mfungamano huo. Mafundisho na maagizo ya dini ya Uislamu yanayomsisitiza mwanamke kujipamba na kujikwatua kadiri inavyowezekana kwa ajili ya mume wake na kufanya jitihada za kushibisha matamanio yake, na vilevile kumtaka mwanaume kumuashiki, kumpenda na kuamiliana vyema na mkewe, yote hayo ni kwa ajili ya kulinda na kutaka kubakisha daima ndoa na mfungamano huo mtakatifu.

Maisha ya ndoa katika Uislamu yanapaswa kutawaliwa na suluhu, amani na maelewano lakini suluhu na maelewano hayo yanatofautiana na yale yanayopaswa kuwepo baina ya mtu na jirani yake, rafiki yake, mfanyakazi mwenzake na kadhalika. Suluhu na maelewano katika maisha ya ndoa vina maana ya kujitolea kila mmoja kwa ajili ya mwenzake, kumtakia mustakbali mwema, kukurubiana zaidi na kuwa kama mtu mmoja, kutambua kuwa saada na ufanisi wa kila mmoja wao na vilevile masaibu na mashaka yake ni masaibu na saada ya mwenzake na kadhalika. Mfungamano kama huu si tu kwamba hautavunjika bali utakuwa ukiimarika siku baada ya siku.

Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.       

Tags