Jun 30, 2017 02:26 UTC
  • Ijumaa 5 Shawwal 1438 Hijria, sawa na Juni 30, 2017

Ijumaa tarehe 5 Shawwal 1438 Hijria, sawa na 30 Juni 2017.

Tarehe 5 Shawwal miaka 1378 iliyopita Muslim bin Aqiil, binamu yake Imam Hussein bin Ali (as) aliwasili katika mji wa Kufa nchini Iraq kwa ajili ya kuwalingania watu wa mji huo wampe mkono wa utiifu na kumsaidia mjukuu huyo wa Mtume katika mapambano yake dhidi ya utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiyya. Kabla ya safari ya Muslim bin Aqiil watu wa mji wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua nyingi Imam Hussein (as) wakimuomba aende kwenye mji huo na kuwaongoza katika mapambano dhidi ya serikali ya kidhalimu ya Banii Umayyah. 

Miaka 57 iliyopita mwafaka na tarehe 30 mwezi Juni 1960, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaani Zaire ya zamani ilitangaza uhuru wake. Kasavubu alichaguliwa kuwa Rais na Patrice Lumumba Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Kabla ya uhuru, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa ikikoloniwa na Wabelgiji. Mapambano ya wapigania ukombozi wa Kongo chini ya uongozi wa mpigania uhuru mashuhuri wa Kiafrika Patrice Lumumba yalifikia kilele miaka kadhaa baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kupelekea kukombolewa Zaire ya zamani. Hata hivyo baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake, serikali ya Ubelgiji ilihusika pakubwa katika kuzusha uasi mkubwa nchini humo. Aidha ulijiri mzozo kati ya Lumumba na Moise Tshombe kibaraka aliyekuwa na uhusiano wa wakoloni wa Kibelgiji na hivyo kuzidisha hali ya machafuko huko Zaire ya zamani. Nchi hiyo ilizidi kuwategemea wageni baada ya kuuawa Lumumba na vibaraka wa ndani. Hatimaye Jenerali Mobutu Seseseko alichukua madaraka katika mapinduzi ya mwaka 1965 Miladia kwa uungaji mkono wa Marekani na kuanza kuwakandamiza wananchi wa nchi hiyo.

Bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita ilianza operesheni ya kijeshi ya Karbala -1 kwa ajili ya kukomboa mji wa Mehran huko magharibi mwa Iran uliokuwa umetwaliwa na jeshi vamizi la Saddam Hussein wa Iraq. Mji huo ulikaliwa kwa mabavu muda mfupi baada ya jeshi la Baath la Iraq kuvamia ardhi ya Iran Septemba 1981 na ulikombolewa na wapiganaji shupavu wa Iran katika operesheni makini ya Karbala-1.

Operesheni Karbala-1

Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo Jenerali Omar Hassan Ahmad al Bashir aliipindua serikali ya Sadiq al Mahdi iliyokuwa ikikabiliwa na migogoro ya ndani, katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu. Omar al Bashir na Dakta Hassan Turabi waliunda chama cha Congres ya Kitaifa ya Sudan kabla ya mapinduzi hayo na wao ndio waliokuwa wakiongoza chama hicho na kushikilia madaraka ya nchi.

Omar Hassan al Bashir

Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita mfumo wa ubaguzi wa rangi ulihitimishwa rasmi huko Afrika Kusini. Wazungu walio wachache wa Afrika Kusini waliwatwisha raia weusi wa nchi hiyo utawala wa ubaguzi wa rangi yaani Apartheid tangu mwaka 1948 Miladia na kwa mujibu wa mfumo huo wa kibaguzi, asilimia 20 ya wazungu wachache wa Afrika Kusini walitambulika kama watu wa tabaka la juu na wenye madaraka ya kuainisha mustakbali na kuongoza nchi. Vilevile ndoa kati ya raia weusi na wazungu zilipigwa marufuku huko Afrika Kusini na wazalendo walizuiwa kuendesha shughuli za kisiasa. 

Mzee Nelson Mandela, shujaa wa kupigania uhuru Afrika Kusini