Jumatano tarehe 12 Julai, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 17 Shawwal 1438 Hijria, inayosadifiana na tarehe 12 Julai 2017.
Tarehe 17 Shawwal miaka 1433 iliyopita vilitokea vita vya Khandaq au Ahzab pambizoni mwa mji wa Madina. Siku hiyo washirikina wa Makka, kwa kuchochewa na Mayahudi wa Madina waliokuwa na hofu kutokana na maendeleo ya Uislamu, walielekea katika mji wa Madina wakiongozwa na Abu Sufiyan na wafuasi wa makabila mengine. Baada ya Mtume Mtukufu kupata habari za harakati za jeshi la maadui, alishauriana na masahaba wake na akaamrisha kuchimbwa handaki pambizoni mwa mji wa Madina kwa mujibu kwa pendekezo lililokuwa limetolewa na Salman Farsi, na Mtume mwenyewe akishiriki katika shughuli hiyo. Wakati jeshi la washirikina lilipowasili lilipigwa na butwaa kuona handaki hilo na halikuwa na njia nyingine isipokuwa kusimama upande wa handaki hilo na kushindwa kuuzingira mji wa Madina. Siku kadhaa baadaye wapiganaji kadhaa na majemedari wa Kiquraish akiwemo Amr bin Abdu Wudd walivuka handaki hilo. Imam Ali bin Abi Twalib (as) alipambana na shujaa huyo kafiri wa Kiquraish na kumuuwa na makafiri wengine wakatimua mbio.

Siku kama ya leo miaka 1306 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo umeendelea hadi leo kufikia Ufaransa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya sehemu za Uhispania ya leo.
Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, alizaliwa Henry David Thoreau, msomi na mwanaharakati wa Kimarekani. David alikuwa akiheshimu mazingira asilia kama viumbe vya Mwenyezi Mungu huku akiwa mwenye akhlaqi njema. Henry David alikuwa akisisitiza kuwa, haifai kuangamiza maisha ya wanadamu kwa tamaa ya kufikia mali na fedha nyingi. Aidha mwanaharakati huyo, aliamini kuwa kama vile ambavyo serikali inavyomuadhibu mtu mkosefu, kadhalika inapotokea serikali hiyo ikashindwa kutekeleza wadhifa wake wa kiuongozi, basi wananchi nao wanatakiwa kuipa adabu serikali hiyo sanjari na kuiondoa madarakani. Miongoni mwa athari muhimu za Henry David Thoreau ni pamoja na kitabu cha 'Uasi wa Kiraia' na alifariki dunia mwaka 1862.
Tarehe 12 Julai miaka 71 iliyopita, hoteli ya Mfalme Daud huko Baitul Muqaddas iliripuliwa kwa bomu na kundi la Kizayuni la Irgun. Hoteli hiyo ilikuwa ikitumiwa sana na raia wa Palestina. Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya hoteli hiyo liliripuka na kuuawa watu zaidi ya 200. Kuweko Wayahudi watano miongoni mwa waliouawa katika mlipuko huo kunabainisha wazi namna Wazayuni wasivyothamini hata maisha ya Wayahudi ili kufikia malengo yao ya kujitanua na kuzusha hofu miongoni mwa Wapalestina.
Siku kama ya leo miaka 11 iliyopita Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilifanya mashambulizi ya anga na bahari huko Lebanon. Utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kukamatwa mateka wanajeshi wake wawili na wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kupitia oparesheni yake ya kujilinda. Tel Aviv ilifanya mashambulizi hayo ya kijeshi huko Lebanon ikiungwa mkono na Washington lengo lake kuu likiwa ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na kuipokonya silaha harakati hiyo inayohesabiwa kuwa nguvu kuu ya mapambano huko Lebanon mbele ya jeshi ghasibu la utawala wa Kizayuni.
