Aug 31, 2017 02:50 UTC
  • Alkhamisi, 31 Agosti 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Mfunguo Tatu Dhulhija 1438 Hijria sawa na tarehe 31 Agosti 2017.

Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhil-Hija. Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingine za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho. Hadithi zinasema kuwa, Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma.

Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija.

Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib (as) aliuawa shahidi mjini Kufa, Iraq. Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wachamungu katika zama zake. Alielekea mjini al-Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussein, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimtaka aende mjini humo na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya. Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad na woga uliotokana na ukatili mkubwa wa mtawala huyo na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake. Muslim alikamatwa na kuuawa shahidi kwa kutupwa chini kutoka juu ya jengo la kasri ya mtawala akiwa amefungwa kamba.

Ziara la Muslim bin Aqil, Kufa

Miaka 890 iliyopita, aliaga dunia Fadhl bin Hassan Tabarsi anayejulikana kwa lakabu la Aminul Islam, alimu, mpokeaji wa hadithi na mfasiri mkubwa wa Qur'ani. Fadhl bin Hassan Tabarsi alikuwa mwanazuoni mkubwa na alikuwa akiheshimiwa na makundi mengi ya Kiislamu. Sheikh Tabarsi pia alikuwa miongoni mwa makadhi waadilifu katika zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha msomi huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani ya Majmaul Bayan yenye juzuu kumi. Vilevile ameandika tafsiri nyingine ya Qur'ani aliyoipa jina la Jawamiul Jamii.

Tafsiri ya Qur'ani ya Majmaul Bayan

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, nchi ya Malaysia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Wananchi wa Malaysia walianza kuingia taratibu katika dini ya Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa nchi za Ulaya ulianza kuenea nchini humo mwanzoni mwa karne ya 16 sambamba na kuwasili nchini humo baharia wa Kireno, Albuquerque. Uholanzi iliidhibiti nchi hiyo katika karne ya 17 na kuanza kuikoloni. Mwaka 1824 nchi za Uholanzi na Uingereza zilifikia makubaliano ambapo Waingereza waliichukua Malaysia na Waholanzi wakachukua Indonesia. Waingereza waliendelea kuikolonia Malaysia hadi nchi hiyo ilipopata uhuru katika siku kama ya leo.

Bendera ya Malaysia

Tarehe 31 Agosti miaka 39 iliyopita, Imamu Mussa Sadr, mwanazuoni na msomi mashuhuri wa Lebanon alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa safarini nchini Libya. Alizaliwa mnamo mwaka 1928 katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Lebanon. Baada ya kuwasili nchini humo, Imamu Mussa Sadr alichukua hatua kubwa za kuboresha maisha ya Walebanoni waliokuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mwanazuoni huyo pia alikuwa muungaji mkono wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina na aliasisi Harakati ya Wanyonge kwa ajili ya kutetea haki za Waislamu wa Lebanon. Hadi sasa juhudi mbalimbali za kutaka kujua hatima ya Imamu Mussa Sadr bado hazijazaa matunda.

Imam Mussa Sadr

Na siku kama ya leo miaka 12 iliyopita karibu Waislamu 1,000 wa Iraq waliokuwa katika shughuli ya maombolezo kwenye mji mtakatifu wa Kadhimain waliuawa. Siku hiyo karibu Waislamu milioni moja wa madhehebu ya Shia walikuwa katika maombolezo ya kukumbuka siku ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Mussa al-Kadhim (as). Milipuko kadhaa ya mabomu iliyotokea katika eneo la maombolezo hayo iliwatia hofu waombolezaji hao ambao walianza kukimbia huko na kule na baadhi yao kuanguka chini na kukanyagwa hadi kufa. Baadhi ya wahanga wa tukio hilo pia walianguka kutoka kwenye daraja maarufu la Aimma lililoko katika mji huo wa Kadhimain.

Kadhimain