Oct 16, 2017 02:36 UTC
  • Jumatatu tarehe 16 Oktoba, 2016

Leo ni Jumatatu tarehe 25 Muharram 1439 Hijria sawa na Oktoba 16, 2017.

Siku kama ya leo miaka 1344 inayosadifiana na tarehe 25 Muharram mwaka 95 Hijria, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, aliuawa shahidi Ali bin Hussein mwenye lakabu ya Sajjad na Zainul Abidiin AS, mtoto wa Imam Hussein bin Ali AS, na mjukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Imam Zainul Abidiin AS alizaliwa mjini Madina mwaka 38 Hijria. Mtukufu huyo alichukua jukumu la kuwafikishia Waislamu ujumbe mzito wa mapambano ya baba yake baada ya kuuawa shahidi huko Karbala. Imam Sajjad AS ameuachia Umma wa Kiislamu kitabu cha Al Swahifatu Sajjadiyya' chenye thamani kubwa ambacho kimejaa dua zenye mafunzo na maarifa ya Kiislamu.

Tarehe 25 Muharram miaka 186 iliyopita, lilichapishwa gazeti la kwanza la Iran lililojulikana kwa jina la Kaghaze Akhbar. Gazeti hilo lilichapishwa na Mirza Swaleh Shirazi mjini Tehran, likiwa na kurasa mbili kubwa. Gazeti hilo lilikuwa likichapishwa mara moja kwa mwezi na lilizungumzia habari za Tehran na miji mingine ya Iran, nchi za Kiarabu na Uturuki.

Nakala pekee iliyobakia ya gazeti hilo imehifadhiwa kwenye jumba la makumbusho la Uingereza.

Kaghaze Akhbar

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 16 Oktoba 1946, kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Nuremberg walinyongwa viongozi 10 wa Ujerumani ya utawala wa Kinazi baada ya kupatikana na hatia za kutenda jinai za kivita. Herman Goering aliyekuwa Kamanda Mkuu wa kikosi cha Jeshi la Anga la Ujerumani na msaidizi wa dikteta Adolphe Hitler ambaye alikuwa amehukumiwa adhabu ya kifo, pia aliamua kujinyonga yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo ya kifo. Hali kadhalika mahakama hiyo iliwahukumu adhabu ya kifungo cha muda mrefu viongozi wengine 9 wa Ujerumani ya Wanazi na wengine watatu hawakupatikana na hatia. Mahakama ya Nuremberg iliyoundwa na wawakilishi wa Marekani, Urusi ya zamani, Uingereza na Ufaransa kwa shabaha ya kuwahukumu maafisa 22 wa Manazi wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita ilikamilisha shughuli zake tarehe 30 Septemba mwaka 1946.

Na siku kama ya leo tarehe 24 Mehr miaka 39 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya vikosi vya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuadhimisha 40 ya mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Shambulio hilo la vikosi vya usalama vya Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.

Mapambano ya wananchi dhidi ya askari wa utawala wa Shah, Kerman