Nov 15, 2017 03:49 UTC
  • Jumatano Novemba 15, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 26 Safar 1439 Hijria inayosadifiana na Novemba 15, 2017.

Siku kama ya leo miaka 387 iliyopita, alifariki dunia Johannes Kepler, mwanahisabati, mnajimu na mtaalamu wa nyota wa Kijerumani. Kepler alizaliwa mwaka 1517 na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Austria na kuanza kufundisha. Baadaye Kepler alifahamiana na Tycho Brahe, mnajimu mtajika wa Denmark na kuanzia hapo taratibu akavutiwa na elimu ya nyota kutoka kwa msomi huyo. Kepler alichunguza na kufanya utafiti katika uwanja huo kwa miaka mingi.

Johannes Kepler

Siku kama ya leo, miaka 148 iliyopita, alizaliwa Vasily Bartold, mustashiriki maarufu wa Russia huko mjini Saint Petersburg. Bartold alisoma na kuhitimu elimu katika chuo kidogo cha lugha za mashariki huko huko Saint Petersburg huku akiwa hodari katika lugha za Kifarsi, Kiarabu na Kituruki. Akiwa na umri wa miaka 27 alifikia daraja la mhadhiri msaidizi katika chuo hicho ambapo alifundisha historia ya mataifa ya mashariki, huku akifanya pia utafiti na utalii mkubwa katika uwanja huo. Aidha kwa kipindi fulani alifanya safari huko Turkestani kwa minajili ya kuendeleza utafiti wake na kubahatika kuandika utafiti huo katika kitabu chake alichokipa jina la 'Turkestani katika kipindi cha mashambulizi ya Mongoli.'

Vasily Bartold

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, utungaji na upasishaji wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulikamilishwa na Baraza la Wataalamu. Katiba hiyo ilianisha na kuupasisha mfumo wa Kiislamu uliojengeka juu ya misingi ya mafunzo na matukufu ya Kiislamu hasa uadilifu katika jamii na kuheshimiwa haki za binadamu. Baada ya katiba hiyo kupasishwa kulifanyika kura ya maoni ya wananchi wote na katiba hiyo ikapasishwa kwa wingi wa kura.

Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, siku chache baada ya kuvamiwa na kutekwa Pango la Ujasusi la uliokuwa ubalozi wa Marekani hapa mjini Tehran, serikali ya Marekani katika radiamali yake kali dhidi ya hatua hiyo ya kimapinduzi, ilizuia fedha za kigeni za Iran katika mabenki yake yote duniani. Kufungwa kwa akaunti za Iran, kulipelekea mashinikizo ya kiuchumi ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua mkondo mpana zaidi. Siku chache kabla ya hatua hiyo, Iran ilikuwa imesimamisha uuzaji wa mafuta yake kwa Marekani kutokana na hatua na misimamo ya chuki ya Washington dhidi ya Jamhuri ya kiislamu ya Iran.

Ubalozi wa Marekani mjini Tehran ukidhibitiwa na wanapambano

Na siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa, mfasiri mkubwa wa Qur'ani na msomi mashuhuri wa Kiislamu Allamah Muhammad Hussein Tabatabai akiwa na umri wa miaka 80. Mwanazuoni huyo mkubwa alizaliwa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa hodari sana katika elimu za falsafa, irfani, tafsiri ya Qur’ani na vilevile katika masuala ya fasihi, hisabati na fiqihi. Allamah Tabatabai ameandika vitabu vingi na miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni tafsiri ya Qur'ani ya al-Mizan.

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

 

Tags