Alkhamisi 23 Novemba, 2017
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 23 Novemba 2017.
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo, huku katika Vita vya Pili vya Dunia akitiwa mbaroni mara mbili na askari wa Kinazi na kutoroka. André aliyekuwa akipinga vita na umwagaji damu, hali kadhalika alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.
Tarehe 23 Novemba miaka 144 iliyopita, Hanoi mji mkuu wa Vietnam, ulivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Ufaransa. Tukio hilo lilijiri wakati wa vita vya Ufaransa vya kutaka kuzikoloni nchi za India na China. Tangu katikati mwa karne ya 19, Ufaransa ilikuwa ikifanya njama na jitihada za kuongeza makoloni yake suala lililoifanya nchi hiyo pia kuamua kuuvamia mji huo. Hadi mwaka 1885 askari wa Ufaransa waliikalia na kuidhibiti ghuba ya Tonkin na Vietnam. Hatimaye vikosi vya Ufaransa vililazimika kuondoka huko Vietnam mwaka 1954 baada ya kushindwa vibaya katika vita hivyo.
Na siku kama ya leo miaka 253 iliyopita alifariki dunia huko Karbala, Iraq faqihi, mpokezi wa hadithi, mhakiki na mwandishi maarufu wa Kiislamu katika karne ya 12 Hijria Sheikh Yusuf Bahrani. Alijifunza elimu ya msingi kwa baba yake na baadaye alielekea Bahrain na Makka kwa ajili ya kupata elimu ya juu. Baadaye alielekea katika mji wa Fasa kusini mwa Iran ambako alianza kufundisha na kuandika vitabu. Wakati huo alianza kuandika kitabu chake kikubwa zaidi cha fiqhi kinachoitwa "al Hadaiqun Nadhirah". Mwanzuoni huyo ameandika vitabu 32 katika taaluma mbalimbali vikiwa ni pamoja na "Anisul Musafir" na "Jalisul Khawatwir.''
