Dec 02, 2017 04:11 UTC
  • Jumamosi, Disemba 2, 2017

Leo ni Jumamosi tarehe 13 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria mwafaka na tarehe Pili Disemba 2017 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, Mirza Kuchik Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza. Mirza Kuchik Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka. ***

Mirza Kuchik Khan Jangali,

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, Laos ilipata uhuru kamili. Uhuru wa nchi hiyo ulipasishwa katika mkutano uliofanyika Geneva mwaka 1945 kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo na serikali kubwa duniani. Laos ilikuwa chini ya uongozi rasmi wa Ufaransa tangu mwaka 1893. Na ilipofika mwaka 1949, Ufaransa ililazimika kuipatia Laos uhuru wa kiasi fulani katika fremu ya Umoja wa Kifaransa, kufuatia mapambano ya ukombozi yaliyoanzishwa katika eneo la India na China. ***

Bendera ya Laos

Katika siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Fidel Castro alianzisha harakati ya kuikomboa nchi yake ya Cuba. Castro akiwa na lengo la kupambana na dikteta Fulgencio Batista, alianzisha mapambano ya silaha akiwa pamoja na wenzake kwa kuishambulia kambi ya kijeshi ya Moncada. Hata hivyo vikosi vya dikteta Batista viliikandamiza vibaya harakati hiyo na kumtia mbaroni Fidel Castro na kumfunga jela. Baada ya muda Castro alipelekwa uhamishoni.

Hata hivyo baadaye aliunda kundi jingine la wapiganaji na kurejea Cuba alikoanzisha mapambano mapya. Hatimaye wanamapinduzi hao wa Cuba walifanikiwa kuyadhibiti maeneo muhimu ya nchi hiyo hali iliyomfanya dikteta Fulgencio Batista akimbilie katika kituo cha kijeshi cha Marekani na baadaye kuitoroka nchi hiyo. ***

Fidel Castro

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Umoja wa Falme za Kiarabu ulipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na kila inapowadia siku kama hii ya leo nchi hiyo huiadhimisha kama siku ya taifa. Ni vyema kutaja hapa kuwa, tawala za kifalme za kusini mwa Ghuba ya Uajemi zilikuwa chini ya utawala wa Uingereza tangu mwaka 1920 Miladia. Uingereza iliasisi vituo vingi vya kijeshi katika eneo hilo, hata hivyo baada ya Vita vya Pili vya Dunia, nchi hiyo ilidhoofika na ikaliweka katika ajenda yake suala la kuondoka katika Ghuba ya Uajemi. ***

Bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati)

Na tarehe Pili Disemba kila mwaka huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa kote duniani. Japokuwa utumwa umefutwa katika maeneo mengi ya dunia lakini suala hilo lingali linashuhudiwa duniani katika kalibu ya utumwa mambo leo.

Siku ya Kimataifa ya Kufutwa Utumwa

 

Tags