Jumamosi, 3 Machi, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 1439 Hijria mwafaka na tarehe 3 Machi 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 934 iliyopita, alifariki dunia msomi na mtaalamu wa fiq'hi wa Kiirani Abu Muhammad Ghazali Tusi maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali. Baada ya kufa baba yake, yeye na kaka yake Ahmad walilelewa na Ahmad bin Radkani. Ghazali alisoma elimu ya fiq'hi kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo. Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khwaja Nidham al-Mulk kumualika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu. Kabla ya kurejea kwake Iran Imam Muhammad Ghazali aliandika kitabu chake maarufu cha "Ihyau Ulumud Din." ***
Miaka 315 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uingereza. Hooke alizaliwa mwaka 1635 huko kusini mwa nchi hiyo. Alifanya tafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia. Robert Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini yake na kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli. Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, tawala za Othmaniya na Urusi zilisaini mkataba katika eneo lililopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano (Treaty of San Stefano). Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan. ***

Tarehe 14 Mfunguo Tisa Jamadi Thani miaka 127 iliyopita, aliaga dunia, Ayatullah Mirza Habibullah Rashti mmoja wa maulama na marjaa mkubwa wa Kiislamu. Akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu, Mirza Habibullah alifanyay safari na kuelekea Najaf Iraq ambapo akiwa huko alihudhuria darsa za Sheikh Murtadha Ansari. Bidii ya masomo na kukwea kwake daraja za kielimu vilimfanya awekwe katika orodha ya marajii wakubwa wa Chuo cha Kidini cha Najaf katika zama hizo. Alimu huyo ameandika pia vitabu na kuvirithisha elimu vizazi vilivyokuja baadaye. Bada'iul Afkaar, ni moja ya vitabu vyake. ***
Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa na kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ilikuwa ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan. ***
Na katikka siku kama ya leo 16 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Gujarat nchini India. Serikali ya India ilitangaza kuwa, Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji hayo, lakini vyombo vingine huru vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ilikuwa ni zaidi ya 2000. Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi lililokuwa limebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Katika mauaji hayo polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji dhidi ya Waislamu. ***