Jumatano tarehe 7 Machi 2018
Leo ni Jumatano 18 Jamadithani 1439 Hijria sawa na Machi 7, 2018.
Siku kama ya leo miaka 744 iliyopita, alifariki dunia mwanafalsafa wa Kitaliano Thomas Aquinas. Alizaliwa mwaka 1225 katika mji wa Napoli na kupata elimu ya dini katika mji huo hadi chuo kikuu. Mwanafikra huyo alibuni falsafa makhususi na kutambua kwamba saada na ufanisi mkubwa zaidi wa mwanadamu ni kupiga hatua za kuelekea kwenye ukamilifu wa kiroho na kwa Mwenyezi Mungu. Aquinas kama alivyokuwa Aristotle, aliamini kuwa ndani ya nafsi ya kila mwanadamu kuna nguvu inayoweza kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiroho. Vilevile aliamini kwamba teolojia haipingani na sayansi kwani kila moja kati ya viwili hivyo inataka kujua hakika na kweli. Itikadi za Aquinas na misimamo yake ya kutumia akili na mantiki ambayo ilikuwa ikipingwa vikali na kanisa katika karne za kati, ilisaidia sana kueneza elimu.
Tarehe 18 Jumadi Thani miaka 158 iliyopita aliaga dunia faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Murtadha Ansari katika mji mtakatifu wa Najaf huko Iraq. Alizaliwa mwaka 1214 Hijria Shamsia katika mji wa Dezful nchini Iran na baada ya kupata elimu ya msingi kwa baba yake alielekea katika miji mitakatifu ya Karbala na Najaf huko Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Miaka kadhaa baadaye Sheikh Ansari alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni na walimu mashuhuri wa zama hizo. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Rasail na Makasib ambavyo vingali vinatumiwa hadi sasa kufundishia katika vyuo vikuu vya kidini.
Katika siku kama ya leo miaka 253 iliyopita alizaliwa Nicephore Niepce mwanakemia wa Kifaransa na mmoja wa waasisi wa fani ya upigaji picha. Niepce alikuwa mtu wa kwanza aliyefanikiwa kupiga picha ya kwanza duniani. Baada ya hapo, Nicephore alitengeneza kamera ya kupiga picha kwa kushirikiana na marafiki zake. Mwanakemia huyo wa Ufaransa aliaga dunia mwaka 1833.
Siku kama hii ya leo miaka 82 iliyopita vikosi vya jeshi la Ujerumani ya Kinazi vilifanya mashamulizi ya kwanza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Wanajeshi wa Ujerumani walipuuza makubaliano ya Warsaw na Locarno kwa amri ya Adolph Hitler na hivyo kuingia eneo la Ranani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya Locarno na Warsaw eneo la Ranani lililokuwa likigombaniwa kati ya Ufaransa na Ujerumani lilitangazwa kuwa eneo lisiloegamea upande wowote. Hata hivyo jeshi la Ujerumani liliamua kuliteka na kulikalia kwa mabavu eneo hilo katika siku kama hii ya leo.
Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, aliuawa Ali Razmara, Waziri Mkuu wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Uingereza. Razmara aliyekuwa jenerali wa jeshi katika utawala wa kifalme aliuawa na mwanamapinduzi wa Kiislamu aliyejulikana kwa jina la Khalil Tahmasbi. Usaliti na uovu wa wazi wa Ali Razmara katika siasa za kuiongoza nchi, ulizusha upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya Waziri Mkuu huyo na kutayarisha mazingira ya kuangamizwa kwake.