Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (17)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 17.
Kwa wale wasikilizaji wa kawaida wa kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu bila ya shaka mnakumbuka kuwa kipindi chetu hiki kilisita kwa muda wa majuma kadhaa kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hivyo kabla ya kuendelea mbele na maudhui nyengine mpya nichukue fursa hii kwanza kuashiria kwa muhtasari yale tuliyozungumza katika mifululizo 16 ya kipindi hiki.
Nukta moja ya msingi tuliyoizungumzia katika utangulizi wa kipindi hiki ni kujibu suali kwamba tunapozungumzia umoja baina ya Waislamu tunakusudia umoja wa jambo gani na wa aina ipi? Tukasema kuwa kuna rai mbili zilizotolewa katika kujibu suali hili. Rai ya kwanza ni ya mtazamo wenye muelekeo ambao, tunaweza kuuita wa 'kiumakanika' juu ya umoja wa jamii ya Kiislamu, unaoitakidi kwamba ili kuwa na umoja, Waislamu wote, Mashia, Masuni na wengineo waache imani na itikadi zao za kimadhehebu na badala yake waamini na kuyatekeleza yale tu yanayoziunganisha pamoja madhehebu zote za Uislamu. Kwa mujibu wa mtazamo huu, Waislamu wote inapasa wafuate madhehebu moja ya pamoja, kwa namna ambayo hakutokuwapo na hitilafu wala tofauti yoyote katika itikadi na hukumu za kifiqhi katika jamii ya Kiislamu. Rai ya pili ina mtazamo mwingine kuhusu umoja na kuwaunganisha Waislamu. Rai hii ina muelekeo tuwezao kuuita wa kioganiki na wenye kuzingatia maumbile na hali halisi. Kwa mujibu wa mtazamo wa rai hii, madhumuni na makusudio ya umoja baina ya Waislamu ni kwamba sambamba na wafuasi wa kila madhehebu kushikamana na itikadi na hukumu maalumu za madhehebu yao, katika uhusiano wa kijamii, kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kiutamaduni wawe kitu kimoja na Waislamu wenzao na wazingatie maslahi makuu ya Uislamu na umma wa Kiislamu na wote kwa pamoja daima wawe mithili ya "mkono mmoja" na nguvu moja katika kukabiliana na maadui wa Uislamu. Ukweli ni kwamba umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu katika muelekeo wa kwanza, si jambo la dharura wala linaloyumkinika katika mazingira tuliyonayo. Umoja wa aina hiyo hauwezekani kufikiwa hata baina ya madhehebu nne maarufu za Ahlu Sunna, yaani Shafi, Hanafi, Maliki na Hanbali. Na sababu ni kwamba hitilafu katika baadhi ya masuala ya kiitikadi na hukumu za utekelezaji ni matokeo ya kimaumbile ya ijtihadi, fikra na tafakuri huru; na wala haziwi sababu ya kutengana nyoyo za Waislamu na kuwa mbalimbali.
Baada ya kubainisha na kutupia jicho kwa muhtasari suala la umoja lilivyokuwa katika zama za mwanzoni mwa Uislamu wakati wa Bwana Mtume Muhammad SAW na yale yaliyojiri baada ya mtukufu huyo kurejea kwa Mola wake, tukaanza kuwazungumzia shakhsia kadhaa wa Ulimwengu wa Kiislamu waliotoa mchango mkubwa katika kupigania suala la umoja katika umma wa Kiislamu. Shakhsia hao ni pamoja na Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi, Muhammad Iqbal-e Lahori, Sheikh Muhammad 'Abdou na Rashid Ridha. Mazungumzo yetu katika sehemu ya 16 ya kipindi hiki yaliishia katika kumzungumzia Rashid Ridha. Tulisema kuwa Rashid Ridha, ambaye kwa upande wa sha’ar na misingi ya urekebishaji wa dini alikuwa akiwafuata Sayyid Jamaluddin Asad Aabadi na Sheikh Muhammad 'Abduh, kinyume na mwalimu wake 'Abduh, alikuwa akitilia mkazo sana umoja wa Kiislamu sambamba na kuendelezwa Ukhalifa. Alikuwa akitaka kurejeshwa Ukhalifa katika muundo uleule wa zama za mwanzoni mwa Uislamu sambamba na kufanyiwa marekebisho na kuondolewa kasoro ulizokuwa nazo. Tukabainisha kuwa kiini cha fikra kuu za Rashid Ridha kuhusu Ukhalifa, badala ya kukita zaidi katika kumzingatia Khalifa mwenyewe, kinatilia mkazo kwenye "Ahlul-Halli wal-Aqd", yaani jopo la wawakilishi wa umma ambalo ndiyo msingi mkuu unaojenga utawala wa Kiislamu unaozungumziwa na mwanafikra huyo.
Kwa muhtasari tunaweza kusema kwamba umoja, ushirikiano na kuwaamsha Waislamu na nchi za Kiislamu ni miongoni mwa daghadagha na mambo yaliyoishughulisha zaidi akili ya Rashid Ridha na kuchukua muda mwingi wa harakati zake. Harakati zake kuhusiana na masuala hayo zilijiakisi kupitia njia tatu. Ya kwanza ni makala alizokuwa akiandika katika jarida la Al-Manar na kuakisi habari na harakati za Waislamu ulimwengu mzima katika muelekeo wa kuleta ushirikiano na kuzikurubisha madhehebu za Kiislamu na umoja baina yao. Njia ya pili ni kupitia utoaji hotuba na indhari mbalimbali katika hafla za Kiislamu na maeneo ya elimu na mafunzo. Na njia ya tatu ni kuandika na kualifu vitabu kikiwemo cha Al-Wahdatul-Islamiyyah. Katika jarida la Al-Manar ambalo lilikuwa na wigo mpana wa kuakisi masuala ya maeneo mengi ya Ulimwengu wa Kiislamu, Rashid Ridha alikuwa akiandika makala mbalimbali kwa nia na madhumuni ya kuwakurubisha pamoja Waislamu

Rashid Ridha alikuwa akitoa wito kwa maulamaa wa Ulimwengu wa Kiislamu kuchukua hatua za kujenga maelewano zaidi baina ya Waislamu kwa kubainisha mitazamo yao kwa ajili ya kuleta umoja baina yao. Aidha kupitia wito huo kuwawezesha Waislamu kueleza mishkili na matatizo yao pamoja na mas-ala ya kifiqhi yanayohitaji fatua za maulamaa hao. Kwa kulitumia jarida la Al-Manar, Rashid Ridha aliweza kujenga mtandao huo wa mawasiliano na maelewano baina ya Waislamu kuanzia Morocco na Tunisia za bara la Afrika mpaka India na Indonesia katika bara la Asia.
Mwanamageuzi na mwanafikra huyo wa kupigania umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu alikuwa akitoa indhari na kuwatahadharisha pia Waislamu na Waarabu juu ya hatari ya Uzayuni na njama za wakoloni dhidi yao na akawa anasisitiza kwa kutaka kuwepo umoja wa Kiislamu wa kukabiliana na Uzayuni na Ukoloni. Katika sehemu nyengine ya makala na maandiko yake katika jarida la Al-Manar, Rashid Ridha alikuwa akizihakiki na kuzikosoa hadithi za kutunga za Israiliyyat na kutokana na jitihada na idili kubwa aliyofanya ya kuzizuia zisienee katika mfumo wa kifikra wa Ulimwengu wa Kiislamu, aliweza kupunguza mifarakano na ukereketwa hasi wa kimadhehebu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika zama ambapo wanamageuzi na wanafikra wapya wa Ulimwengu wa Kiarabu walikuwa wakipigia upatu fikra kama ya Umajimui wa Kiarabu, yaani Pan-Arabism, Uzalendo wa Kiarabu, yaani Arab-Patriotism na Vuguvugu la Kiarabu, Rashid Ridha alikuwa akisisitiza kwamba, njia pekee ya kujiondoa kwenye hali ya kulemaa na kubaki nyuma kimaendeleo na kufikia ustawi ni kupatikana umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu na kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 17 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Natumai kuwa mumenufaika na kuelimika kutokana na yale mliyoyasikia katika kipindi hiki. Inshallah katika mfululizo ujao wa 18 tutakuja kumzungumzia Abdulrahman Al-Kawakibi, mrekebishaji mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.