Jumamosi, Machi 17, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 28 Mfunguo Tisa Jamadi Thani 1439 Hijria sawa na tarehe 17 Machi 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita, ardhi ya Baitul-Muqaddas huko Palestina ilikombolewa na Waislamu baada ya Warumi kushindwa. Vita vya kwanza kati ya Waislamu na Warumi vilijiri huko kaskazini mwa Bahari Nyekundu baada ya kudhihiri Uislamu. Jeshi la Waislamu lilitoa pigo kwa Warumi na eneo la kusini mwa Palestina likakombolewa katika zama za utawala wa Umar bin Khattab. Baada ya kushindwa huko, mfalme wa Roma alituma jeshi kubwa katika ardhi za Palestina. Warumi walishindwa vibaya na jeshi la Kiislamu katika vita vilivyojiri huko Palestina na mwishoni mwa mapigano hayo, kamanda wa jeshi la Roma aliuawa na Damascus ikadhibitiwa na Waislamu. ***

Katika siku kama ya leo miaka 849 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia katika mji mkuu wa Misri Cairo Abul Qassim Shatibi, alimu na qarii mashuhuri wa Qur'ani ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Imam al-Qurra. Alizaliwa mwaka 538 Hijria ambapo mbali na elimu ya usomaji Qur'ani, alikuwa amebobea pia katika elimu ya tajwidi, Tafsiri ya Qur'ani, hadithi, nahau, lugha na elimu nyingine. Abul Qassim Shatibi ameacha athari nyingine katika nyuga mbalimbali ambapo Qasidat al-Shatibiyah ni moja tu ya vitabu vyake mashuhuri, kitabu ambacho kinazungumzia masuala jumla yanayohusiana na elimu ya tajwidi na kitabu hiki kimechapishwa mara chungu nzima katika nchi za Misri na India. ***

Miaka 70 iliyopita katika siku kama ya leo, wawakilishi wa nchi za Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg, walitia saini mkataba wa ushirikiano wa pamoja mjini Brussels, Ubelgiji. Katika mkataba huo uliofahamika kwa jina la "Mkataba wa Brussels", nchi hizo zilikubaliana kuanzisha mfumo wa ulinzi wa pamoja na kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kiutamaduni. Aidha mkataba huo ndio uliokuwa chachu ya kuanzishwa kwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Kwani ni baada ya hapo ndipo yalifanyika mazungumzo kati ya Marekani, Canada na baadhi ya nchi wanachama wa Mkataba wa Brussels huko mjini Washington, Marekani ambapo baadaye kuliundwa Shirika hilo la NATO mwezi Aprili 1949.***

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita inayosadifiana na sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsia aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. ***
