Jumanne, Machi 20, 2018
Leo ni Jumanne tarehe Pili Rajab mwaka1439 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Machi mwaka 2018 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1218 iliyopita, alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu mjini Baghdad, Iraq. Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo, na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Aidha alipata kujifunza elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi. Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as). Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 999 iliyopita alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa. Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale. Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa.
Tarehe 20 Machi miaka 291 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.
Na siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, sawa na tarehe 29 Esfand 1329 Hijria Shamsia, baada ya vuta nikuvute na mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza na utawala kibaraka wa mfalme hapa nchini, hatimaye wabunge wa Bunge la Taifa na lile la Seneti walipitisha muswada wa kutaifisha sekta ya mafuta nchini. Kupitishwa muswada huo ilikuwa hatua muhimu katika mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mkoloni Mwingereza. Kufuatia kupasishwa sheria hiyo, Muswadiq aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Iran kwa kuungwa mkono wa wananchi na viongozi wa kidini hasa Ayatullah Kashani.
