Apr 11, 2018 00:02 UTC
  • Jumatano, Aprili 11, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 24 Rajab 1439 Hijria sawa na Aprili 11, 2018.

Siku kama ya leo miaka 1432 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw). Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui. Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili. Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa benderea mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.

Ngome ya Khaibar

Siku kama ya leo miaka 1100 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan  ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa. Mwanafalsafa huyo  mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya  Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.

bu Nasr Muhammad Farabi

Miaka 158 iliyopita katika siku kama ya leo, chombo cha kuzalisha baridi kilibuniwa na mwanakemia wa Kifaransa kwa jina la Ferdinand Carre. Kifaa hicho kilikuwa kikizalisha baridi kwa kutumia gesi ya ammonia. Ubunifu huo wa Carre ulikuwa hatua muhimu katika kuhifadhi dawa na vyakula ili visiharibike hususan katika maeneo yenye joto. Uvumbuzi wa msomi huyo hatimaye ulipelekea kutengenezwa kwa majokofu na vifaa vingine vikubwa vya kuzalisha baridi kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Ferdinand Carre

Katika siku kama ya leo miaka 33 alifariki dunia Enver Hoxha Rais wa zamani wa Albania. Hoxha alikuwa kiongozi wa wapiganaji wa mrengo wa kushoto baada ya Italia kuivamia na kuikalia kwa mabavu Albania mwaka 1939. Enver Hoxha alichukua madaraka ya nchi mwaka 1944 kwa kusaidiwa na jeshi la Urusi ya zamani baada ya kushindwa Italia katika Vita vya Pili vya Dunia. Rais huyo wa zamani wa Albania miaka miwili baadaye aliitangaza nchi hiyo kuwa ni Jamhuri ya Kikomonisti.

Enver Hoxha

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, siku moja tu baada ya mahakama moja ya Ujerumani kutoa hukumu dhidi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ziliwaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tehran. Jaji wa mahakama hiyo iliyopata umaarufu kwa jina la Mykonos aliathiriwa mno na misimamo ya Kizayuni na kutangaza kuwa viongozi wa Iran walihusika katika mauaji ya mpinzani wa utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekuwa akiishi Ujerumani. Iran ilikadhibisha madai hayo na ikajibu hatua ya nchi hizo kwa kuwaita nyumbani mabalozi wake wote katika nchi za Umoja wa Ulaya. Uamuzi wa mahakama ya Mykonos kwa hakika ulikuwa sehemu ya hujuma ya kisiasa ilikuwa ikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Takribani miezi kumi baadaye mabalozi wa Umoja wa Ulaya walianza kurejea hapa Tehran mmoja baada ya mwingine.