Aya na Hadithi (16)
Assalaamu Alaykum wapezi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.
Kutokana na rehema zake zisizo na mwisho, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametufindisha dua nyingi tukufu na zenye thamani kubwa ambazo tunapasa kumuomba kupitia kwazo ili aweze kutupa heri ya dunia na Akhera. Wakati huohuo ametutahadharisha dhidi ya kuomba mambo yanayohusiana na dunia tu bila ya kuzingatia Akhera na hili ndilo jambo ambalo tunaelekezwa kwalo na Aya kadhaa za Qur'ani Tukufu ambapo huenda Aya jumuishi zaidi kati ya hizo ni hizi zinazofuata ambazo kwa pamoja tunazisikiliza kwa makini ili tupate kunufaika nazo katika maisha yetu ya kila siku. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya za 200 na 201 za Surat al-Baqarah: Na mkishatimiza ibada zenu basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi. Na wapo baadhi ya watu wanaosema: Mola wetu! Tupe (mema) hapa duniani; nao katika Akhera hawana fungu lolote. Na katika wao wapo wanaosema: Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema Akhera, na utukinge na adhabu ya Moto!

Kama mnavyoona wapenzi wasikilizaji, Aya ya kwanza inakemea mwanadamu kumuomba Mwenyezi Mungu mahitaji yake ya dunia tu bila kuzingatia ya Akhera na ya pili inatutaka tuzingatie maadili na taratibu muhimu za Qur'ani Tukufu katika uombaji dua nazo ni za kuomba mema ya dunia zote mbili, yaani ya humu duniani na ya huko Akhera. Katika upande wa pili, tunapozingatia Hadithi Tukufu tunaona kwamba kutokana na maadili haya ya kuvutia ya Qur'ani, nazo zinakemea vikali ukiukaji mipaka wa pande zote mbili. Hivyo zinakataza na kukemea kuiudhi nafsi kwa kutosheka tu na kuomba mahitaji ya Akhera, kama ambavyo pia zinakataza kuzingatia mahitaji ya dunia pekee. Kuhusiana na jambo hili, Sayyid Qutub ad-Deen ar-Rawandi (MA) amenukuliwa katika kitabu chake cha ad-Da'waat akisema: 'Imepokelewa kwamba Mtume Mtukufu (saw) aliingia nyumbani kwa mgonjwa mmoja na kumuuliza nini kilikuwa kimempata. Alisema: 'Uliposwali pamoja na sisi swala ya Magharibi na kusoma Surat al-Qaaria' nilisema: Ewe Mwenyezi Mungu! Kama nina dhambi mbele yako na unataka kuniadhibu kwayo huko Akhera, basi iharakishe humu duniani. Hivyo nikawa kama unavyoniona. Hapo Mtume (saw) akasema, ulisema vibaya. Ungesema: 'Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema Akhera, na utukinge na adhabu ya Moto'!
Kisha Mtume (saw) akamwombea na akapona.' Kuna Riwaya nyingine nyingi ambazo zinazungumzia na kukariri tukio hili na jinsi Mtume Mtukufu (saw) alivyoamiliana nalo. Imepokelewa katika Tafsiri ya Nuru at-Thaqalain kwa kunukuliwa kitabu cha al-Ihtijaaj ambapo Imam Ali (as) ananukuliwa akisema: 'Mtume (saw) alikuwa ameketi na kumuulizia mmoja wa masahaba zake. Wakamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Amekuwa nchini mfano wa kifaranga asiyekuwa na manyoya. Mtume akaenda kumtembelea na kumuona kama kifaranga asiyekuwa na manyoya kutokana na makali ya balaa. Akamuuliza, je, ulikuwa ukiomba dua fulani ulipokuwa na afya njema? Akasema: Nam, nilikuwa nikisema: Ewe Mwenyezi Mungu! Kwa adhabu yoyote utakayoniadhibu huko Akhera, nijaalie humu duniani. Hapo Mtume (saw) akamwambia: Ungesema: 'Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema Akhera, na utukinge na adhabu ya Moto'! Hapo sahaba huyo alitamka maneno hayo na ghafla akawa ni kana kwamba amesisimuka kutokana na maradhi sugu yasiyo na tiba, hali ya kuwa ni mzima wa afya na akatoka nje pamoja na sisi.'

Wapenzi wasikilizaji, Hadithi Tukufu zinatuongoza kwenye mifano iliyo wazi ya mambo mema ya humu duniani ambayo tunapasa kumuomba Mwenyezi Mungu atujaalie. Imepokelewa katika kitabu cha Bihar al-Anwaar kuwa mtu mmoja alimuuliza mjukuu mkubwa wa Bwana Mtume (saw) yaani al-Imam Hassan al-Mujtaba kuhusu tafsiri ya kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: '……Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema Akhera', naye (as) akasema: Ni elimu na ibada duniani na Pepo huko Akhera.'
Hapa, na kwa maneno yake haya, Imam Hassan al-Mujtaba (as) anaashiria suala ambalo watu wengi hughafilika nalo, kwa sababu kuna mema mengine yapi yaliyo juu ya elimu, maarifa na ibada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu duniani? Na bila shaka matunda ya maarifa ni utiifu na ibada. Hii ndiyo mifano bora zaidi ya mema ya humu duniani ambayo baraka zake hudumu hadi Akhera. Hadithi Tukufu pia zinatuelekeza kwenye mifano mingine ya Aya hii tukufu. Imam Abu Abdallah as-Swadiq (as) amenukuliwa katika kitabu cha al-Kafi akisema kuhusiana na maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu, 'Mola wetu! Tupe mema duniani na (tupe) mema Akhera': Ni kuomba radhi ya Mwenyezi Mungu na Pepo Akhera na maisha na tabia njema duniani.' Imam Swadiq (as) pia amenukuliwa katika Hadithi nyingine iliyopokelewa na as-Swaduq katika kitabu chake cha Maani al-Akhbar akisema katika kutafsiri maana ya Aya hii kwamba: 'Ni radhi ya Mwenyezi Mungu na Pepo huko Akhera na kupanuliwa riziki na maisha pamoja na maadili bora duniani.' Amepokelewa pia katika Hadithi nyingine iliyonukuliwa katika Tafsiri ya al-Ayyashi akisema kuwa kuomba ridhaa ya Mwenyezi Mungu ni moja ya mifano bora zaidi ya mambo mema humu duniani. Amesema (as) katika kutafsiri Aya hii: 'Ni radhi ya Mwenyezi Mungu, kupanuliwa (kuboreshewa) maisha na kuwa na marafiki wema duniani na Pepo huko Akhera.
********
Wapenzi wasikilizaji, tunafikia natija hii mwishoni mwa kipindi hiki ambapo tumekuwa tukijadili mifano ya mambo mema tunayopasa kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie humu duniani na huko Akhera kwamba, yanajumuisha masuala yote yanayoboresha maisha ya mwanadamu, na baraka zake hazina kikomo, bali zinaendelea kuwa pamoja naye katika maisha yake ya duniani na ya kudumu milele Akhera.
Na kwa natija hiyo ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.