Jumamosi, 28 Aprili, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 11 Shaaban 1439 Hijria sawa na tarehe 28 Aprili 2018 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1406 kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa mtukufu Ali bin Hussein, mwana mkubwa wa kiume wa Imam Hussein A.S na mjukuu wa Mtume Muhammad SAW mjini Madina aliyejulikana kwa lakabu ya Ali Akbar. Ali bin Hussein ambaye alifanana sana na babu yake Mtume Mtukufu SAW, alinufaika sana na bahari ya maadili mema na mafunzo ya dini ya Kiislamu kwa kuwa pamoja na babu yake Imam Ali AS na baba yake Imam Hussein AS. Mtukufu Ali bin Hussein, alikuwa maarufu kwa jina la Ali Akbar yaani Ali mkubwa kutokana na jina lake kufanana na majina ya mdogo wake ambaye pia alikuwa na jina hilo la Ali.Ali Akbar alikuwa na nafasi muhimu katika mapambano ya baba yake dhidi ya dhulma na uasi wa utawala wa Bani Umayyah. Aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijiria baada ya kuingia katika medani ya vita na kupigana kishujaa katika mapambano ya jeshi la Yazid bin Muawiyah na Imam Hussein A.S na wafuasi wake. ***

Miaka 463 iliyopita katika siku kama ya leo, Kongamano la Augsburg lilifanyika katika mji wenye jina hilo huko nchini Ujerumani. Katika kongamano hilo, viongozi wa Kikatoliki chini ya uongozi wa Papa Paul IV (wa Nne) kwa mara ya kwanza waliunga mkono uhuru wa madhehebu ya Waprotestanti. Katika kongamano hilo pia ulichukuliwa uamuzi wa kurejeshwa mali za Waprotestanti walizokuwa wamenyang'anywa. Hata hivyo uamuzi huo haukutekelezwa na hivyo kuzusha vita vya miaka kumi kati ya Waprotestanti na Wakatoliki katika nchi mbalimbali za Ulaya. ***
Katika siku kama ya leo miaka 369 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Shaaban 1070 Hijria, Mohammad Taqi Majlisi maarufu kama Majlisi wa Kwanza, msomi na Arif mkubwa Muirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1003 Hijria Qamari katika mji wa Isfahan ambao zama hizo ulikuwa mji mkuu wa silsila ya watawala wa Safavi. Alizaliwa wakati Iran ilikuwa inashuhudia ustawi mkubwa wa kiutamaduni na kielimu. Familia ya Allamah Majlisi ilikuwa ya wasomi na wanazuoni kiasi kwamba alipata sehemu ya masomo yake kutoka kwa baba yake na jamaa zake wengine katika familia. Baada ya kujifunza fiqhi, itikadi na tafsiri katika darasa la Sheikh Bahai, alipata umashuhuri kama alim na arif mkubwa. Alikwea daraja la juu la masomo baada ya kutembelea mji wa Najaf al Ashraf nchini Iraq. Baad ya kurejea Isfahan alijishughulisha kufunza na alitambulika kwa umahiri wake katika fiqhi, hadithi, tafsiri na itikadi. ***
Katika siku kkama ya leo miaka 73 iliyopita, Benito Mussolini dikteta wa Kifashisti wa Italia aliuawa kwa kunyongwa na wazalendo wan chi hiyo. Mussolini alizaliwa Julai 29 mwaka 1883 kkatika familia masikini huko kaskazini mwa Italia. Baada ya kumaliza masomo yake ya Chuo Kikuu alianza kufanya kazi yya uandishi katika magazeti. Machi 23 mwaka 1919 Mussolini alistafidi na uasi na hali ya vurugu iliyojitokeza nchini italia na kuanzisha Chama cha Ufashisti na kuwa kiongozi wa chama hicho. Ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa 1922 ulimfanya Benito Mussolini kuwa Waziri Mkuu baada ya kumridhisha mfalme. ***
Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Marekani ililazimika kuondoka kwa madhila huko Vietnam baada ya kupata kipigo cha kuaibisha. Majeshi ya Marekani yaliingia Vietnam kwa shabaha eti ya kukabiliana na kasi ya kuenea ukomonisti na kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji waliokuwa maarufu kwa jina la Viet Cong huko Vietnam ya kaskazini. Katika vita hivyo Marekani ilitumia silaha zote zilizopigwa marufuku isipokuwa silaha za nyuklia. Wapiganaji hao wa mwituni walifanikiwa kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Marekani na tarehe 28 Aprili mwaka 1975 Rais Richard Nixon wa Marekani aliwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuondoka Vietnam. ***
Tarehe 8 Ordibehesht miaka 30 iliyopita watawala wa kizazi cha Aal Saud walikata uhusiano wa Saudi Arabia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya utawala wa Saudia kufanya mauaji ya umati ya mahujaji wa Wairani wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu mjini Makka katika siku iliyopewa jina la Ijumaa ya Damu hapo tarehe 9 Mordad 1366 Hijria Shamsia, uhusiano wa Iran na nchi hiyo ulifika kiwango cha chini zaidi na wanadiplomasia wa Iran nchini Saudia wakapunguzwa kwa kiasi kikubwa. Wanadiplomasia wa Saudia mjini Tehran walikuwa tayari wamekwishaondoka. Hatimaye uhusiano wa nchi hizi mbili ulikatwa kikamilifu tarehe 28 Aprili 1986. Safari za Wairani waliokuwa na hamu ya kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makka na Haram tukufu ya Mtume Muhammad (saw) mjini Madina pia zilisimamishwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Uhusiano wa nchi hizo mbili ulikatwa katika kipindi ambacho Saudi Arabia ilikuwa msaidizi mkubwa wa kifedha wa utawla wa Saddam Hussein katika vita vyake dhidi ya Iran na hatua hiyo ilichukuliwa sambamba na siasa za Marekani za kubana na kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.****
Miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, makundi ya Mujahidina wa Afghanistan hatimaye yalipata ushindi baada ya mapambano ya miaka 13 dhidi ya jeshi la Urusi ya zamani na serikali ya kibaraka ya nchi hiyo. Baada ya majeshi ya Urusi ya zamani kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka 13, hatimaye mwezi Februari mwaka 1989 wanajeshi hao wa Urusi walilazimika kuondoka Afghanistan. Hata hivyo kutokana na makundi hayo ya Kiafghani kutokuwa na mikakati mizuri na pia kutopata misaada kutoka nje, vikosi vya serikali ya Afghanistan viliendelea kubakia madarakani chini ya uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Urusi ya zamani. Aprili 28 Mujahidina walifanikiwa kuuteka kikamilifu mji wa Kabul na kuiondoa madarakani serikali kibaraka ya Afghanistan.***