Apr 30, 2018 22:15 UTC
  • Jumanne, Mei Mosi, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 14 Shaabani 1439 Hijria sawa na tarehe Mosi Mei 2018 Milaadia.

Duniani'. Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Siku kama ya leo miaka 800 iliyopita alizaliwa Ibn Yunus, fakihi, tabibu na mwanahesabati mashuhuri wa Kiislamu. Alijufunza masomo ya kawaida ya zama zake kutoka kwa baba yake na wasomi wengine wa wakati huo. Mwanazuoni huyo mashuhuri wa Kiislamu baada ya kuhitimu masomo yake, alifundisha katika shule na vyuo kadhaa mjini Cairo Misri pamoja na kuandika vitabu kuhusiana na masuala tofauti ya kielimu. Mbali na taaluma za fik'hi, tiba na hesabati alikuwa na ujuzi mkubwa pia katika uwanja wa muziki. Miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msomi huyo wa Kiislamu ni kitabu kinachoitwa al-Asraar as-Sultaniyya kinachozungumzia masuala ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, sawa na tarehe Mosi Mei 1915, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland. Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.

Vita vya Kwanza vya Dunia

Miaka 14 iliyopita katika siku kama hii, tarehe Mosi Mei 2004, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo. Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya. Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27.

Image Caption