May 01, 2018 22:03 UTC
  • Jumatano tarehe Pili Mei 2018

Leo ni Jumatano tarehe 15 Shaabani 1439 Hijria sawa na tarehe Pili Mei 2018.

Siku kama ya leo mika 1184 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (af) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa na Qaim, kwa maana ya msimamishaji mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa Imam Askari (as). Alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake huyo mtukufu na kisha kughibu machoni pa walimwengu kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu ambapo atadhihiri tena ulimwenguni wakati muwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri humu duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhuma na uonevu. 

Siku kama ya leo miaka 499 iliyopita, alifariki dunia mchoraji na msanifu majengo maarufu wa Italia Leonardo da Vinci. Alizaliwa mwaka 1452 na umahiri wake ulidhihiri haraka katika nyanja mbalimbali za sanaa. Miongoni mwa michoro maarufu ya Leonardo Da Vinci ni The "Last Supper" na "Mona Lisa". 

Leonardo da Vinci

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 12 Ordibehesht 1358 Hijria Shamsia, mwanachuoni na mwanafikra mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Murtadha Mutahhari, aliuawa shahidi na kundi lililo dhidi ya mapinduzi la Furqan hapa nchini. Tukio hilo lilitokea katika kipindi cha chini ya miezi mitatu tangu kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa Iran. Shahidi Mutahhari alijistawisha kielimu kutoka kwa maulamaa wakubwa wakiwemo Ayatullahil Udhma Burujerdi, Allamah Tabatabai na Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ayatullah Murtadha Mutahhari ameandika makumi ya vitabu nyanja mbalimbali.

Ayatullah Murtadha Mutahhari

Na katika siku kama ya leo miaka 7 iliyopita Usama bin Laden kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda aliuawa na vikosi vya Marekani huko nchini Pakistan. Usama aliyekuwa mmoja wa waasisi wa al-Qaeda alizaliwa Machi mwaka 1957 huko Riyadh nchini Saudi Arabia na kusoma katika Chuo Kikuu cha King Abdul-Aziz. Kundi la kigaidi la al-Qead linahusishwa na mauaji mengi duniani likiweko shambulio ya Septemba 11mwaka 2001 na mashambulio ya mabomu dhidi ya balozi za Marekani Dar es Salaam Tanzania na Nairobi Kenya.

Usama bin Laden